WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haitamsamehe mtu yeyote
atakayejihusisha na ubadhilifu wa mali za fedha za Ushirika nchini.
“Kwa
Serikali hii ya awamu ya Tano tutachua hatua kali kwa wezi wa mali na
fedha za ushirika na tunaendelea kufanya usafi wa wabadhilifu hadi
tupate viongozi waadilifu,”.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Jumamosi, Julai Mosi, 2017), katika
Maadhimisho ya Siku ya Ushirika Duniani (SUD), iliyoadhimishwa kitaifa
mjini Dodoma kwenye ukumbi wa Jakaya Kikwete.
Amesema
miongoni mwa changamoto zinazoukabili Ushirika nchini ni pamoja na wizi
na ubadhilifu wa rasilimali za Ushirika unaofanywa na baadhi ya
viongozi na wanachama wasiokuwa waaminifu.
Waziri
Mkuu amesema changamoto nyingine ni baadhi ya viongozi wa vyama vya
Ushirika kutoheshimu miongozo ya vyama vyao na kujifanyia mambo kwa
maslahi yao binafsi.
Amesema
katika kukabiliana na changamoto hizo Serikali itaendelea kutimiza
wajibu wake na kuweka mazingira rafiki ya kustawisha Ushirika nchini ili
kutoa fursa ya Ushirika kushamiri na kuwawezesha Watanzania kumiliki
uchumi wa nchi yao.
“Haikubaliki
hata kidogo kuona sekta hii inayosadifu maisha ya Mwafrika hamnufaishi
ipasavyo , hivyo naelekeza Tume ya Maendeleo ya Ushirika nchini
ihakikishe kuwa vyama vya Ushirika vinaendeshwa kisayansi na kwa mujibu
wa sheria,” amesema.
Pia
amezielekeza Kamati za Ushauri za Mikoa na Wilaya nchini, ziingize
agenda ya Maendeleo ya Ushirika kama moja ya agenda muhimu inayopaswa
kujadiliwa na kuwekewa maazimio ya utekelezaji. Pia wawe na takwimu za
vyama vya Ushirika na Wanaushirika.
Hata
hivyo Waziri Mkuu amezielekeza mamlaka zote zinazohusika na Ushirika
nchini zijiwekee malengo yanayopimika ya namna ya kuboresha sekta ya
Ushirika.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu ameelekeza kwamba masuala yote yanayohusu Ushirika wa
kilimo nchini lazima yaratibiwe na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi.
Aidha,
Waziri Mkuu amezielekeza Wizara za Kilimo, Mifugo na Uvuvi na Ofisi ya
Rais-TAMISEMI zifanye mapitio kubaini elimu na ujuzi katika ngazi zote
za Ushirika kwa ajili ya kuwaandalia kozi za muda mfupi za kuongeza
ujuzi au kubainisha aina ya watumishi wanaohitajika kwenye sekta hiyo.
Pia
amewaagiza Maofisa Ushirika nchini kuhakikisha wanasimamia vizuri
uchanguzi wa Vyama vya Ushirika vya Msingi (AMCOS) na kuwaondoa wagombea
wote waliowahi kuwa viongozi, ambao waliondolewa madarakani kutokana na
ubadhilifu wa mali na fedha za Ushirika.
Awali,
Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba alisema wizara
itaendelea kusima na kuchukua hatua kwa viongozi wote wa vyama vya
Ushirika watakaobainika kufuja mali na fedha za Ushirika.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.