*Ataka TRA wafanye sensa ya majengo kwenye miji
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka maafisa wa Mamlaka ya Kodi ya Mapato
nchini (TRA) wakusanye kodi za majengo kwa kuzingatia sheria na wasitoze
kodi ya majengo wazee wenye umri zaidi ya miaka 60.
"TRA
ijipange kukusanya kodi za majengo kuanzia Julai Mosi 2017. Katika
kutekeleza jukumu hilo, zingatieni sheria. Tusisikie mnawadai kodi ya
majengo wazee wenye umri zaidi ya miaka 60 kwa majengo wanayotumia kama
makazi yao," amesema.
Ametoa
agizo hilo leo (Alhamisi, Juni 22, 2017) wakati akizungumza na wananchi
na viongozi wa wilaya ya Chato waliohudhuria uzinduzi wa jengo la TRA,
wilayani humo, mkoani Geita.
Waziri
Mkuu amewataka maafisa hao wakusanye kodi ya majengo kwenye maeneo ya
mjini na siyo vijijini kwani kodi hiyo haiwahusu. "Msiende vijijini.
Nyumba za nyasi au za tembe hazihusiki. Tembeleeni nyumba za mijini.
Piteni kwenye mitaa, muainishe aina zote za nyumba zinazostahili
kulipiwa kodi. Mkishafanya sensa, wekeni utaratibu wa kuwawezesha
wananchi kulipia kodi hizo," amesema huku akishangiliwa.
Pia
amewataka wananchi wanaonunua bidhaa wadai risiti lakini wahakikishe
wanapewa risiti yenye kiwango halisi walicholipia. "Ukipewa risiti
uiangalie kama ina kiwango halisi cha fedha uliyotoa. Kuna watu wachache
wasio waaminifu wanaamua kukupa risiti lakini imeandikwa bei ndogo
kuliko ile uliyolipia, ukitoa laki moja anakuparisiti ya sh 10,000."
Mapema,
akitoa taarifa ya ujenzi wa jengo hilo la ghorofa moja, Kamishna Mkuu
wa TRA, Bw. Charles Kicheere alisema ujenzi huo ulianza Julai 12, mwaka
jana na ulikamilika Juni 12, mwaka huu.
"Ujenzi
wa jengo hili umegharimu sh. bilioni 1.4 na ulichochewa na ongezeko
kubwa la idadi ya walipakodi wa Chato kutoka watu 150 mwaka 2010/2011
hadi kufikia watu 600 mwaka 2016/2017", alisema.
Pia
alisema wamejenga ofisi hizo ili kuwapunguzia umbali wafanyabiashara wa
wilaya hiyo ambao walilazimika kwenda Geita mjini kupata huduma za TRA
ambako ni umbali wa zaidi km.120.
Alisema
hivi karibuni watakamilisha ukarabati wa ofisi za mikoa ya Mara,
Iringa, ikiwemo kujenga ofisi kwenye mikoa mipya ya Simiyu, Katavi,
Njombe na Manyara. "Pia tutajenga ofisi kwenye mkoa mpya wa kikodi wa
Kahama," alisema.
Alizitaja wilaya ambazo ziko mbioni kupatiwa ofisi zake kuwa ni Kondoa, Longido, Bunda na Arumeru.
Alisema katika mwaka ujao wa fedha, TRA imelenga kukusanya sh. trilioni 17.106 na watahakikisha wanafikia lengo hilo.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.