Watumishi wa Ofisi ya
Waziri Mkuu wameaswa kufanya kazi kwa uadilifu kwa kuzingatia maadili na utendaji
katika Utumishi wa Umma wakati wa Maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma.
Hayo yamesemwa na Katibu
Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera na Uratibu Dkt. Hamisi
Mwinyimvua alipokutana na wafanyakazi wa ofisi yake Dodoma kwa lengo la
kuiadhimisha Wiki hiyo inayofanyika kila mwaka kuanzia Juni 16-23 Barani Afrika
ambapo kauli mbiu ya mwaka huu ni
“Kuimarisha Ushirikishwaji wa Jamii katika Utoaji Huduma: Vijana washirikishwe
kuleta Mabadiliko Barani Afrika”.
“Kila mtumishi wa umma
anapaswa kuwa mwadilifu na mchapakazi hivyo niwaombe watumishi wote muwe mfano
kwa kuwa waadilifu katika utendaji wenu kwa kuzingatia sheria zote za utumishi
wa umma ili kuisaidia Serikali na kuwafikia wananchi kiujumla.”alieleza
Dkt.Mwinyimvua
Katika kuiadhimisha wiki
hii ya utumishi wa Umma ni wakati pekee wa kujitathimini eneo la kiutendaji na
kuona maeneo yenye mapungufu ili yafanyiwe maboresho kwa haraka lengo likiwa
kuondokana na mazoea yaliyokuwepo na kuendana na kasi ya Serikali ya Awamu ya
Tano.
Kwa upande wake, Mkurugenzi
wa Utawala na Rasilimali watu, Issa Nchansi amewataka watumishi kuzingatia mambo nane muhimu yaliyoainishwa
katika Kanuni za Maadili ya Utendaji katika Utumishi wa Umma ikiwemo; Utoaji wa
huduma bora, Utii kwa Serikali, bidii ya kazi, kutoa huduma bila upendeleo,
uwajibikaji kwa umma,kuheshimu sheria, matumizi sahihi ya taarifa na uadilifu
sehemu ya kazi.
Naye, Katibu Mkuu (Waziri
Mkuu na Bunge) Bi. Maimuna Tarishi aliwaomba watumishi wote kuzingatia kauli
mbiu ya mwaka huu kwa kuwawezesha vijana kielimu, kiuchumi na kijamii ili
waweze kuzalisha na kuwa tegemeo la taifa.
“Niwaombe watumishi wote
kuiangalia hili kundi la vijana wanaoajiriwa na Serikali kwa kuwatia moyo na
kuwaunga mkono katika utekelezaji wa kazi zao” alisisitiza Tarishi
Sambamba na hili, Katibu
Mkuu, Tarishi alisema kuwa ili kuwe na
utendaji wenye matokeo lazima kuitumia wiki hii kukumbushana majukumu na nafasi
zetu katika kuitumikia serikali.
“Tuwe na utendaji wenye
matokeo na si kuhesabu siku, miezi hadi mwaka bali tuwajibike kwa uadilifu kila
muda tuwapo Serikalini.”
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.