Sunday, November 12, 2017

IDARA YA MAAFA YAWAJENGEA UWEZO WAJUMBE WA KAMATI YA SHERIA NDOGO YA USIMAMIZI WA MAAFA

Ofisi ya Waziri Mkuu imeendesha warsha ya siku moja kwa wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Sheria Ndogo inayohusu Dhana, Sheria na Mfumo wa Usimamizi wa maafa kwa lengo la kuwajengea uwezo wa masuala ya Menejimenti ya maafa nchini.

Akizungumza wakati wa warsha hiyo iliyofanyika Novemba 12, 2017 Makamu Mwenyekiti wa Kamati hiyo Mhe.William Ngeleja alieleza kuwa warsha hiyo itawajengea uwezo wajumbe wa Kamati hususani katika utekelezaji wa majukumu yao.

"Warsha hii ni muhimu kwa wajumbe wa kamati kwani itaongeza uelewa kuhusu sheria ya Usimamizi wa Maafa namba 7 ya mwaka 2015 pamoja na dhana nzima ya Menejimenti ya Maafa"

Akifanua mhe.Ngeleja amesema warsha hiyo itasaidia kuongeza tija katika utendaji wa kamati hasa katika kuishauri Serikali kuhusiana na masuala ya maafa.

Kwa upande wake Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagamaaliwaeleza wajumbe kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuimarisha uratibu wa usimamizi wa maafa nchini ili kujenga uwezo wa Kuzuia, Kujiandaa, Kukabili na Kurejesha hali pindi maafa yanapotokea hivyo warsha hii inatija kwa wajumbe wote.

"Warsha hii itasaidia kuongeza uelewa kwa wajumbe kuhusu namna bora ya kupambana na majanga yanapoytokea nchini na madhara yake, vyanzo na sababu za kutokea, hatua zinazochukuliwa na Serikali katika kuzuia, kupunguza  madhara, kujiandaaa , kukabili na kurejesha hali katika ubora zaidi" Alisisitiza Mhe. Mhagama.

Sambamba na hilo Mhe. Mhagama alibainisha kuwa Serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali ikiwemo kuimarisha uratibu wa usimamizi wa maafa nchini kwa kuanzisha Idara ya uratibu wa maafa inayotekeleza majukumu yake kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu zilizopo.

Pamoja na hatua hizo Serikali ina sera ya Taifa ya Usimamizi wa maafa ya mwaka 2004 ambayo inaeleza hatua na majukumu ya wadau mbalimbali katika shughuli za Manejimenti ya maafa na kutoa muongozo wa utekelezaji wake.

Aidha mmoja wa wajumbe wa kamati hiyo Mhe.Elibariki Kingu alipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kuendesha warsha hiyo na kushauri serikali kuwekeza zaidi katika kupambana na majanga yanayoweza kujitokeza hapo nchini.

AWALI
Mada zilizowasilishwa katika warsha hiyo zilijikita katika Dhana, Sheria na Mfumo wa Usimamizi wa Maafa hapa nchini ikiwa ni moja ya jukumu la Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Uratibu wa Maafa kwa kuwajengea uwezo wadau na wananchi kwa ujumla ili kuweza kuyakabili maafa pindi yanapotokea. Warsha ilikuwa ya siku moja iliyojumuisha wajumbe wote wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Sheria Ndogo kuhusu masuala ya Menejimenti ya Maafa iliyofanyika Bungeni Dodoma.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.