Waziri Mkuu Kassim Majaliwa leo (Jumanne, Novemba 28, 2017) amefungua kongamano la Kitaifa la maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani, lililofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Juliasi Nyerere jijini Dar es Salaam.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali haitawavumilia watu wote wanaotumia vibaya fedha za umma ambazo zinapaswa kuleta maendeleo kwa wananchi, zikiwemo na za Mfuko wa Udhamini wa Kudhibiti Ukimwi.
Amesema mfuko huo unalenga kufanikisha ukusanyaji wa fedha za kutosha amabazo ni muhimu kwa Taifa wakati huu tunapoazimia kumaliza ukimwi ifikapo mwaka 2030..
Waziri Mkuu alitoa kauli hiyo leo (Jumanne, Novemba 28, 2017) wakati akifungua kongamano la Kitaifa la maadhimisho ya siku ya ukimwi duniani, lililofanyika jijini Dar es Salaam.
“Nitoe wito kwa Bodi ya Mfuko huu na watendaji wake kuhakikisha wanasimamia kikamilifu fedha hizi ili ziweze kufanikisha malengo ya kuanzishwa kwa Mfuko huu. “
Waziri Mkuu amesema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dkt. John Magufuli itaendelea kutenga fedha za mfuko huo na kuhamasisha wananchi, wadau na sekta binafsi kuchangia mfuko huo muhimu.
Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Serikali imedhamiria kujenga nchi ya viwanda ili waweze kufikia uchumi wa kati, jambo ambalo haliwezi kufikiwa iwapo wananchi wake watakuwa hawana afya bora.
“Hatutaweza kufikia malengo haya kama Taifa iwapo watu wetu hawatakuwa na afya bora kwani nguvu kazi kwa ajili ya Tanzania ya Viwanda itatokana na wananchi wenye nguvu na afya bora.”
“ Hivyo kama Serikali tutahakikisha tunaendelea kutoa huduma bora za afya ili wananchi wetu waweze kuwa na afya bora. Tutaendelea kuwakinga wananchi wetu hususan ni vijana ili Taifa letu liwe na nguvu kazi ya kutosha hasa wakati huu tunapoanza mageuzi makubwa ya kiuchumi na kimaendeleo.”
Pia Waziri Mkuu amesema kwamba kwa sasa Watanzania wengi wana uelewa mkubwa wa ukimwi lakini changamoto iliyopo ni kubadili tabia na kuachana na tabia hatarishi zinazosababisha kupata maambukizo mapya.
Amesema jambo hilo ni hatari kubwa kwa nchi yetu kwa sababu bado wananchi wengi wanaendekeza tabia ya kuwa na wapenzi wengi tena kwa wakati mmoja na hakuna uaminifu katika ndoa.
Kauli mbiu ya maadhimisho hayo kwa mwaka huu “changia mfuko wa udhamini wa udhibiti ukimwi, okoa maisha”.
Kongamano hilo lilihudhuliwa na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-Walemavu Bibi Stella Ikupa Alex, Naibu Waziri Wizara ya Afya, Ustawi wa Jamii, Wazee, Jinsia na Watoto Dkt. Faustine Ndungulile, Makamishna wa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania (TACAIDS).
Wengine ni Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania (TACAIDS), Dkt Leonard maboko, Mwenyekiti wa Baraza la Wanaoishi na virusi vya Ukimwi (NACOPHA), wawakilishi wa wadau wa maendeleo na wadau wa ukimwi nchini.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.