WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa wilaya ya Ruangwa wajiunge na Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) ili waweze kumudu gharama za matibabu bila kulazimika kuwa fedha taslimu.
Ametoa wito huo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa mji wa Ruangwa na vijiji vya jirani katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye viwanja vya CWT, mjini Ruangwa, mkoani Lindi.
“Leo hii nimetoa kadi za CHF kwa wazee 4,000 wa wilaya hii. Ninaishukuru Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa kwa kutenga fedha na kuwalipia wazee hawa ili wanufaike na bima hii ya afya kama ambavyo imeelekezwa kwenye Ilani ya Chama cha Mapinduzi.”
“Ninatoa wito kwa wananchi wengine walipie sh. 15,000 kwa mwaka ili wapatiwe kadi kwa ajili ya watu sita wa familia zao; yaani mhusika, mwenza wake na watoto wanne. Bima hii inasaidia kwa vile unapata matibabu hata kama huna fedha taslimu,” alisema.
Waziri Mkuu alikabidhi kadi kwa Mzee Issa Juma Ngalapa, mkazi wa kata ya Nachingwea pamoja na Mzee Suleiman Stola Lihepa wa kijiji cha Kilimahewa, kata ya Nachingwea kwa niaba ya wazee wote waliotakiwa kupatiwa kadi hizo.
Akitoa ufafanuzi juu ya mpango huo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa Bw. Andrea Chezue alisema mpango wa kutoa kadi za bima ya afya kwa wazee wameuita ‘CHF Endelevu’ kwa sababu walifanya tathmini na kubaini kuwa matibabu yao yana gharama, na yasipolipiwa, dawa zitaisha au wazee hao hawataweza kupatiwa huduma.
“Katika Halmashauri tulifanya utambuzi wa wazee wa kuanzia miaka 60 na kuendelea kwenye vijiji vyote na kubaini kuwa kuna wazee 4,000. Tukaamua Halmashauri iwalipie sh. 15,000 kwa kila wazee sita kama ilivyo katika kaya ili tuweze kuchangia gharama za matibabu yao,” alisema.
“Mzee akipatiwa kadi hii, inakuwa ni ya kudumu, anaitumia miaka yote. Si ya kulipia kila mwaka kama zilivyo zile nyingine. Hadi sasa tumeshatoa kadi kwa wazee 2,700 na tunaendelea kutengeza kadi hadi tukamilishe zote. Tumepanga kuwa kila mwaka, tutafanya utambuzi wa wazee katika vijiji vyote ili wale wanaofikisha umri huo, nao pia waingizwe kwenye mpango huu,” alisema.