*Wamo 13 kutoka
ngome kuu ya CUF Matambarare
WANACHAMA 19 kutoka
vyama vya upinzani katika kata za Matambarare na Mnacho wilayani Ruangwa mkoani
Lindi, wamekabidhi kadi zao na kujiunga na Chama cha Mapinduzi (CCM).
Wanachama hao
kutoka vyama vya CUF na CHADEMA, walikabidhi kadi zao kwa Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa jana jioni (Jumamosi, Desemba 30, 2017) wakati alipokuwa akizungumza
na wakazi wa kijiji cha Matambarare Kusini kwenye mkutano wa hadhara
uliofanyika kijijini hapo.
Waziri Mkuu yuko kwenye
mapumziko ya mwisho wa mwaka, na ameamua kukagua miradi ya maji, ujenzi wa
zahanati na kuzungumza na wananchi katika wilaya hiyo.
Akiwa katika kijiji cha
Matambare Kusini, Waziri Mkuu alipokea wanachama 17 ambao kati yao 13 wanatoka
Chama cha Wananchi (CUF) na wanne wanatoka Chama cha Maendeleo na Demokrasia
(CHADEMA).
Akiwa katika kijiji cha
Ng’au kata ya Mnacho, wilayani humo, Waziri Mkuu alipokea wanachama wawili, Bw.
Swibert Mwambe kutoka CUF na Bw. Paskali Rogert wa CHADEMA.
Akizungumza kwa niaba ya
wenzake 17, Mzee Said Bakari Makungwa (maarufu kama Ustaadh Makungwa) alisema alikuwa
muasisi wa chama cha TANU pamoja na CCM mwaka 1977 kilipozaliwa, na alishika
nyadhifa mbalimbali hadi alipoamua kuondoka.
“Jamani nimerudi nyumbani,
na mtu akirudi nyumbani huwa haadhibiwi,” alisema Ustaadh Makungwa mwenye umri
wa miaka 80 na kuamsha kicheko kwenye mkutano huo.
Alisema yeye anataka
kuwakumbusha wananchi waliohudhuria mkutano mambo manne aliyoyasisitiza Baba wa
Taifa, hayati Mwl. Julius K. Nyerere ambayo ni watu, ardhi, siasa safi na
uongozi bora.
Kuhusu ardhi, alisema
wanaRuangwa wamepewa ardhi na Mwenyezi Mungu ili iwape mazao na madini. “Watu
ni sisi ambao tunapaswa tutumie vema rasilmali tuliyopewa katika ardhi,” alisema.
Kuhusu siasa safi, Ustaadh
Makungwa alisema: “Kuna siasa safi gani zaidi ya hii tuliyonayo sasa?
Utaitafuta wapi zaidi ya kwa Mheshimiwa Magufuli? Safari hii, kafikisha bei ya
korosho hadi sh. 4,045 kwa kilo moja. Nani kama Magufuli?” alihoji Mzee
Makungwa.
Kuhusu uongozi bora, Mzee Makungwa
alisema Mheshimiwa Magufuli ameonyesha njia akisaidiwa na Waziri Mkuu Kassim
Majaliwa. “Kazi ya viongozi ni kuonyesha njia. Sasa wewe kugeuka kushoto au
kulia unatafuta nini?” alihoji.
“Hebu niambieni Ruangwa ya
juzi na ya leo ziko sawa?,” alijohi na kujibiwa kwamba haziko sawa. “Mimi
nimerudi nyumbani, ninaomba msamaha pale nilipowaudhi. Kwa sababu ya umri
wangu, ninaijua vema historia ya CCM, njooni kwangu mchukue historia ya chama,”
alisema huku akishangiliwa.
Waziri Mkuu
anaendelea na ziara ya jimboni kwake kwa kuzindua kampeni ya kitaifa ya
upandaji miche bora na mipya.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.