*Asema migodi
mingi iko Ruangwa kuliko Liwale, Nachingwea
WAZIRI MKUU
Kassim Majaliwa amemuagiza Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa, Bw. Joseph Mkirikiti
atafute jengo haraka kwa ajili ya ofisi ya madini wilayani humo.
Ametoa agizo
hilo jana mchana (Jumamosi, Desemba 30, 2017) baada ya kubaini kuwa Kaimu Afisa
Madini Mkazi wa Kanda ya Kusini, Bw. Ogesa Charles Tale anaishi Nachingwea
lakini anahudumia wilaya tatu za Ruangwa, Liwale na Nachingwea yenyewe.
Waziri Mkuu yuko kwenye
mapumziko ya mwisho wa mwaka, na ameamua kukagua miradi ya maji, ujenzi wa
zahanati na kuzungumza na wananchi katika wilaya hiyo. Alikuwa akizungumza na
wakazi wa kijiji cha Namungo, wilayani Ruangwa mkoani Lindi baada ya kukagua
migodi ya wachimbaji wadogo iliyopo kijijini hapo.
“Sisemi ahamie
hapa kwa sababu ni nyumbani, hapana. Ni kwa sababu najua ofisi yake iko
Nachingwea lakini shughuli nyingi za madini ziko Ruangwa kuliko Liwale na Nachingwea,”
alisema.
“Haiwezekani
uwe kule, halafu uwahudumie huku wananchi walio wengi. DC mpe ofisi akae hapa,
apite maeneo mengi ya huku na kuwasikiliza wachimbaji wadogo ambao ni wengi
zaidi. Kule mashimo ni moja moja, ataenda mara moja kwa wiki. Kuanzia sasa,
atakuwa Ruangwa ili afanye kazi kwa karibu zaidi na kundi kubwa la wachimbaji
wadogo,” alisema.
Mapema, kabla ya kuzungumza na wananchi Waziri Mkuu
alitembelea mgodi wa dhahabu wa Namungo na kukagua shughuli za uzalishaji
pamoja na mitambo inayotumiwa kwenye uchenjuaji wa mchanga wa dhahabu.
Akitoa maelezo
kwa Waziri Mkuu, Meneja Mitambo ya Uchenjuaji (Processing Plant) wa kampuni ya
Gemini inayomiliki mgodi huo, Bw. Emmanuel James alisema kwa sasa wamesimamisha
mitambo kwa sababu wanakabiliwa na tatizo la umeme mdogo licha ya kuwa wameweka
umeme wa njia tatu.
“Umeme upo wa
njia tatu lakini tatizo hautoshi, pia transfoma iliyopo ni ndogo na haihimili
umeme wa mgodini,” alisema.
Alipoulizwa
wametoa ajira kwa watu wangapi, Bw. James alijibu kuwa wametoa ajira zaidi ya
200, ambapo kati ya hizo, ajira 40 ni za moja kwa moja.
Naye Kaimu Afisa Madini Mkazi wa Kanda ya Kusini, Bw.
Ogesa Tale alimweleza Waziri Mkuu kwamba kuna mashimo zaidi ya 120
yanayomilikiwa na wachimbaji wadogo katika eneo hilo lakini mashimo 47 yanaendelea na uzalishaji na
mengine 32 yalifungwa ama kwa sababu za kiusalama ama kwa kuwa yamekamilisha kazi
yake na hayana faida tena.
Waziri Mkuu
anaendelea na ziara ya jimboni kwake kwa kuzindua kampeni ya kitaifa ya
upandaji miche bora na mipya milioni 10.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.