Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe.
Jenista Mhagama amesema kupitishwa kwa muswada wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya
Jamii utasaidia kuwanufaisha watumishi wa umma kwa kurahisisha utoaji wa huduma
kwa wakati na wenye tija.
Amebainisha hayo wakati wa Mkutano
wa Baraza Kuu la Taifa la Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU)
walipokutana Mjini Dodoma katika warsha ya siku tano kuanzia Januari 29
hadi Februari 02, 2018 kujadili masuala ya wafanyakazi nchini.
Waziri Mhagama
alieleza kuwa, kupitiswa kwa muswada ni moja ya utekelezaji wa takwa la Ibara
ya 11 kifungu kidogo cha kwanza cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
ulipoona umuhimu wa kuweka mifumo ya hifadhi ili Watanzania wapate manufaa hasa
siku za uzeeni.
“Maamuzi ya kuwa na
Muswada huu umezingatia taratibu zote za kisheria ikiwemo Katiba yetu ya
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sera ya Hifadhi ya Jamii,
Mkataba wa Shirika la Kazi Duniani unaoongoza katika maswala ya Hifadhi ya
Jamii”.Alisisitiza Mhagama
Muswada huu
umelenga kuunganisha mifuko ya Pensheni ambayo ni PSPF, LAPF, GEPF NA PPF ili
kukidhi kilio cha muda mrefu cha wafanyakazi cha kuunganisha mifuko hiyo ili
kupunguza gharama za uendeshaji na kuwa na mfumo madhubuti utakaohakikisha
mwanachama anapata mafao kwa wakati.
“Muswada umebainisha kuwa jumla ya
mafao 7 yatakayolipwa na mfuko huo itakuwa: Fao la Pensheni, Warithi,
Ulemavu, Uzazi, Ukosefu wa Ajira, Ugongwa na Fao la kufiwa.” alifafanua Waziri
Mhagama.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa
TALGWU Bw. Tumaini Nyamhokya aliipongeza Serikali kwa hatua hiyo na kueleza
kuwa ni wakati mwafaka kwa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa kuunga
mkono juhudi za Serikali ikiwemo kuunganishwa kwa mifuko hii kwa manufaa ya
wafanyakazi wote wa umma.
“Niwaombe watumishi
wa umma wote kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha maslahi ya
watumishi na kwa asilimia 98 muswada huu umeyapitisha mapendekezo na ushauri
uliotolewa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) na kuwekwa kwenye
utekelezaji.”Alisema Nyamhokya.
Naye, Mwenyekiti wa Chama hicho Bw.
Suleiman Kikingo alisema kuwa kuunganishwa kwa mifuko hiyo na kuwekwa kwa tozo
ya asilimia tano kwa mfuko utakao bainika kushelewesha mafao ya mwanachama
itasaidia kupunguza changamoto ya ucheleweshwaji wa mafao kwa wanachama.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.