Thursday, February 1, 2018

WAZIRI MHAGAMA: MUSWADA WA SHERIA YA MFUKO WA HIFADHI YA JAMII KUNUFAISHA WATUMISHI WA UMMA

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza jambo wakati wa Mkutano wa Baraza Kuu la Taifa la Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Rayal Village Dodoma Februari 01, 2018.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Watu wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amesema kupitishwa kwa muswada wa Sheria ya Mfuko wa Hifadhi ya Jamii utasaidia kuwanufaisha watumishi wa umma kwa kurahisisha utoaji wa huduma kwa wakati na wenye tija.
Amebainisha hayo wakati wa Mkutano wa Baraza Kuu la Taifa la Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa (TALGWU) walipokutana Mjini Dodoma katika warsha ya siku tano kuanzia Januari 29 hadi Februari 02, 2018 kujadili masuala ya wafanyakazi nchini.
Waziri Mhagama alieleza kuwa, kupitiswa kwa muswada ni moja ya utekelezaji wa takwa la Ibara ya 11 kifungu kidogo cha kwanza cha Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ulipoona umuhimu wa kuweka mifumo ya hifadhi ili Watanzania wapate manufaa hasa siku za uzeeni.
“Maamuzi ya kuwa na Muswada huu umezingatia taratibu zote za kisheria ikiwemo Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Sera ya Hifadhi ya Jamii, Mkataba wa Shirika la Kazi Duniani unaoongoza katika maswala ya Hifadhi ya Jamii”.Alisisitiza Mhagama
Muswada huu umelenga kuunganisha mifuko ya Pensheni ambayo ni PSPF, LAPF, GEPF NA PPF ili kukidhi kilio cha muda mrefu cha wafanyakazi cha kuunganisha mifuko hiyo ili kupunguza gharama za uendeshaji na kuwa na mfumo madhubuti utakaohakikisha mwanachama anapata mafao kwa wakati.
“Muswada umebainisha kuwa jumla ya mafao 7 yatakayolipwa na mfuko huo itakuwa:  Fao la Pensheni, Warithi, Ulemavu, Uzazi, Ukosefu wa Ajira, Ugongwa na Fao la kufiwa.” alifafanua Waziri Mhagama.
Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa TALGWU Bw. Tumaini Nyamhokya aliipongeza Serikali kwa hatua hiyo na kueleza kuwa ni wakati mwafaka kwa Chama cha Wafanyakazi wa Serikali za Mitaa kuunga mkono juhudi za Serikali ikiwemo kuunganishwa kwa mifuko hii kwa manufaa ya wafanyakazi wote wa umma.
“Niwaombe watumishi wa umma wote kuunga mkono jitihada za Serikali za kuboresha maslahi ya watumishi na kwa asilimia 98 muswada huu umeyapitisha mapendekezo na ushauri uliotolewa na Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) na kuwekwa kwenye utekelezaji.”Alisema Nyamhokya.

Naye, Mwenyekiti wa Chama hicho Bw. Suleiman Kikingo alisema kuwa kuunganishwa kwa mifuko hiyo na kuwekwa kwa tozo ya asilimia tano kwa mfuko utakao bainika kushelewesha mafao ya mwanachama itasaidia kupunguza changamoto ya ucheleweshwaji wa mafao kwa wanachama.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.