Friday, January 5, 2018

WAZIRI MKUU AHIMIZA KILIMO CHA KAHAWA

*Asisitiza kahawa iuzwe kwa mfumo wa ushirika

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wananchi wa wilaya ya Songea mkoani Ruvuma wajikite kwenye zao la kahawa ili wawe na zao mbadala la biashara.

Ametoa wito huo leo (Ijumaa, Januari 5, 2017) wakati akizungumza na wakazi wa kijiji cha Lipokela na vijiji jirani, wilayani Songea mara baada ya kukagua shamba la kahawa la Aviv Tanzania lenye ukubwa wa hekta 1,990.

“Limeni kahawa ili mpate fedha sababu zao hili ni la biashara. Kahawa ni miongoni mwa mazao matano ya biashara ambayo Serikali ya awamu ya tano imeamua kuyawekea mkazo ili yaweze kuongeza tija kwa wakulima na kuinua uchumi wa Taifa”.

“Tumeamua kuweka mkazo kwenye mazao matano ya pamba, kahawa, chai, korosho na tumbaku kwa sababu yanaleta tija na kuliingizia Taifa fedha za kigeni,” alisema na kuongeza:

“Tumefanya tathmini na tumegundua udhaifu mkubwa mkubwa katika usimamizi wa mazao haya ndani ya Serikali kuanzia ngazi ya Halmashauri.”

Waziri Mkuu alisema ni lazima wananchi walime zao hilo na viongozi wahakikishe wananchi wananufaika za zao hilo. Hata hivyo, alionyeshwa kutoridhishwa na utendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Songea baada ya kuelezwa kuwa kampuni ya Aviv Tanzania imezalisha miche milioni moja lakini iliyochukuliwa na kusambazwa kwa wananchi ni miche isiyozidi 200,000.

“Kampuni hii imeamua kutoa miche ya bure kwa wakulima, wamezalisha miche milioni moja lakini hadi sasa imechukuliwa 200,000 tu. Kuna miche zaidi ya 800,000, imebaki, na tena wawekezaji hawa wanatoa elimu bure ya kulima na kuitunza mikahawa yako,” alisema.

Amewataka wakulima hao watenge ekari moja hadi tatu kwa kila kaya ili waweze kulima zao hilo. “Wana Lipokela tengeni ekari moja hadi tatu za kulima kahawa, tukifanya hivyo suala la fedha kupitia kahawa litakuwa limekamilika,” alisema.

Amesema itabidi zao la kahawa liundiwe mfumo maalum wa ununuzi ambao ni wa ushirika kwa kuzingatia vyama vya msingi (AMCOS) vilivyokuwepo.
Mapema, akitoa taarifa juu ya shamba hilo, Meneja wa Aviv Tanzania, Bw. Medu Medappa alisema lengo la kuanzisha mradi huo lilikuwa ni kuhakikisha wanapata shamba kubwa la kahawa aina ya Arabica nchini Tanzania lenye viwango vya kimataifa.

Alisema wamekwishatoa ajira kwa Watanzania wapatao 3,000 zikiwemo za moja kwa moja na za msimu.

Alisema kampuni hiyo imeweza kuchangia miradi ya maendeleo kwenye vijiji vinne jirani vya Lipokela, Lusonga, Liganga na Selekano. “Hadi mwaka 2017 tuliweza kukamilisha ujenzi wa zahanatio katika kijiji cha Lipokela, nyumba ya mwalimu katika vijiji vya Liganga na Lusonga, uchangiaji wa madawati kwenye vijiji vya Lipokela na Lusonga,” alisema.

Alisema wameweza kuanzisha scheme ya wakulima wadogo wa nje (outgrowers scheme) kwa wakulima 2,000 ambao wamegawanyika kwenye vikundi 36 katika vijiji 31 ndani ya mkoa wa Ruvuma.

Waziri Mkuu anaendelea na ziara yake ya kikazi mkoani Ruvuma kwa kutembelea wilaya ya Mbinga ambako atakagua miche kwenye taasisi ya TACRI, atatembelea kiwamda cha kukoboa kahawa cha Mbinga (MCCCO), kuzungumza na watumishi na madiwani na pia kuhutubia mkutano wa hadhara.

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.