Thursday, June 28, 2018

SERIKALI KUBORESHA MFUMO WA HUDUMA ZA VIBALI VYA AJIRA NA UKAAZI NCHINI

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama akizungumza na waandishi wa habari alipokutana nao kuzungumzia azma ya Serikali ya kuboresha mfumo wa huduma za vibali vya ajira na ukaazi nchini hii leo Juni 28, 2018 Jijini Dodoma.

Baadhi ya waandishi wa habari wakifuatilia maelezo ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) walipokutana Bungeni Dodoma Juni 28, 2018

Baadhi ya waandishi wa habari wakifuatilia maelezo ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Uratibu, Kazi, vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama (hayupo pichani) walipokutana Bungeni Dodoma Juni 28, 2018.  
NA MWANDISHI WETU
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi (Idara ya Uhamiaji) imekusudia kufanya mabadiliko ya kimfumo ambayo yatahusisha utoaji wa vibali ya ajira nchini pamoja na vibali vya ukaazi ili kuhama kutoka mfumo wa zamani na kuwa na mfumo wa kielektroniki.

Maboresho hayo yanakwenda sambamba na matumizi ya TEHAMA, ambapo kutakuwa na utaratibu wa kuwa na kadi moja (smart card), ambayo itakuwa na taarifa za muhusika kuhusu kibali cha ajira pamoja na hati ya ukaazi.
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe.Jenista Mhagama alikukutana na waandishi wa habari hii leo Mjini Dodoma (Juni 28, 2018).
Waziri Mhagama alieleza kuwa, kuanzishwa kwa mfumo huo utasaidia kurahisisha upatikanaji wa taarifa za wageni nchini zenye uhakika na zitakazo patikana kwa wakati ili kudhibiti mianya yote rushwa kwa watendaji kwa kuwa taarifa zote zitapatikana katika kanzidata maalum.
“Uwepo na mfumo huu mpya utasaidia kuondokana na mianya yote ya rushwa kwa Watendaji wa Serikali pamoja na kurahisisha upatikanaji wa taarifa za wageni na malengo ya ujio wao hapa nchini kwani taarifa zote zitapatikana kwenye kanzidata maalum,”alisisitiza Mhagama
Kwa upande wake Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi Dk. Mwigulu Nchemba alieleza kuwa mfumo huu wa kadi moja utasaidia hutatua changamoto ya uchuleweshaji wa vibali ili kuondokana na usumbufu wa ufuatiliji wa vibali hivyo kwa wageni.

“Lengo kubwa la mabadiliko haya ni kuwa na kadi moja itakayomruhusu mgeni kufanya kazi kulingana na sheria na taratibu zilizopo na kuwaondolea usumbufu usio wa lazima na kuongeza ufanisi kwa watendaji wa Serikali,” alisisitiza Mwigulu
Aidha alitoa rai kwa Taasisi zote zinazotumia wageni kuhakikisha wanafanya uhakiki wa taarifa za wageni hao hususan uhalali wa kuwepo kwao pamoja na kazi wanazozifanya ili kuepuka udanganyifu unaoweza kujitokeza.
“Nitoe rai kwa Taasisi zote zinazotumia wageni katika ofisi zao kuhakiki na kujiridhisha taarifa za vibali vya ajira na ukaazi wa wageni hao ili kuepuka taarifa zisizo sahihi na kuhakikisha kila kila mgeni anakuwa na kibali halali kinachomruhusu kuwepo nchini,”alisisitiza Mwiguli

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.