WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali imedhamiria kumaliza tatizo la
upatikanaji wa mafuta ya kula nchini kwa kufanya mageuzi makubwa katika
zao la michikichi, alizeti na ufuta.
Ameyasema
hayo leo (Jumatano, Juni 27, 2018) wakati akizungumza na Balozi wa
Tanzania nchini Malaysia, Balozi Dkt. Ramadhan Dau ofisini kwake Mlimwa
jijini Dodoma.
’’Tunataka
kufanya mageuzi makubwa ya zao la michikichi, tunataka kuondoa miti ya
zamani na kupanda miche mipya. Tutafanya kampeni ya kuhamasisha upandaji
wa miche mipya ya michikichi ili tuondoe tatizo la upatikanaji wa
mafuta nchini,’’.
Waziri
Mkuu amesema licha ya kuwepo kwa michikichi mingi nchini ila uzalishaji
wake unafanyika kwa njia kienyeji, hivyo Serikali imedhamiria kuboresha
kilimo hicho kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili liweze kuleta manufaa
makubwa kwa Taifa na wakulima.
Amesema
mbali na zao la michikichi, pia Serikali imedhamiria kuboresha mazao
mengine ya mbegu za kukamua mafuta kama alizeti na ufuta, ambayo
itayafuatilia kuanzia hatua za awali za uandaaji wa mashamba hadi
masoko.
Kadhalika,
Waziri Mkuu amesema Tanzania bado ipo chini kwenye uzalishaji wa mbegu
za kukamulia mafuta na inahitaji wawekezaji katika mazao hayo, hivyo
amemuagiza Balozi wa Tanzania nchini Malaysia atafute wawekezaji hao.
’’Inawezekana
kujitosheleza kwa mafuta ya kula kwa sababu Tanzania tuna ardhi ya
nzuri yenye rutuba na watu ambao kilimo ndiyo shughuli yao kubwa. Na
hivi karibuni nitafanya ziara mkoani Kigoma kwenda kuhamasisha kilimo
cha michikichi,’’.
Kwa upande wake,
Balozi Dkt. Dau amesema Malaysia ndiyo nchi inayoongoza duniani kwa
kilimo cha michikichi na inatengeneza zaidi bidhaa 400 kutokana na zao
hilo, yakiwemo mafuta ya kuendeshea magari.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.