WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali
imetenga sh. bilioni 4.3 ili kujenga vituo vya kuhifadhi damu (satellite blood
banks) kwenye mikoa 12.
Ameitaja mikoa hiyo kuwa ni Manyara, Katavi, Rukwa, Ruvuma na Njombe.
Mingine ni Tanga, Arusha, Pwani, Singida, Songwe, Geita na Simiyu.
Waziri
Mkuu ametoa kauli hiyo leo (Ijumaa, Juni 29, 2018) bungeni jijini Dodoma katika hotuba yake aliyoitoa wakati wa kuahirisha Mkutano wa 11 wa Bunge. Bunge limeahirishwa hadi Septemba 4, mwaka
huu.
Amesema lengo la mpango huo ni kuboresha upatikanaji wa damu hasa kwa
akinamama wanaopoteza damu nyingi wakati wa kujifungua. “Serikali imedhamiria
kupunguza vifo vya akinamama na watoto vitokanavyo na uzazi. Katika kutekeleza
azma hiyo, Serikali kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo inaendelea kufanya
ukarabati na ujenzi wa majengo ya upasuaji, maabara, wodi za wazazi, nyumba za
watumishi na wodi za watoto,” amesema.
Amesema kukamilika kwa majengo hayo, kutaboresha huduma za uzazi kwa
akinamama na watoto wachanga. “Hatua hii itawezesha upatikanaji wa huduma
kamili za uzazi na kupunguza vifo vya mama na watoto. Katika mwaka 2018/2019,
eneo litakalopewa kipaumbele ni kuimarisha upatikanaji vifaa na watumishi
katika vituo 208 vinavyoendelea kuboreshwa,” amesema.
Waziri Mkuu ametumia fursa hiyo kuwasihi watumishi wa afya, waongeze
juhudi ya kuhamasisha wananchi wajitolee damu na pia akawaomba wananchi nao wawe
na utamaduni wa kuchangia damu ili kuwezesha upatikanaji wa damu salama itakayohifadhiwa
kwenye benki hizo.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Serikali inaendelea kuimarisha huduma za kibingwa
nchini kwa kutenga shilingi bilioni 14 ili kuanzisha huduma ya kuchunguza mwili
bila upasuaji (PET Scan) katika taasisi ya Saratani ya Ocean Road.
Amesema kuanza kwa huduma hiyo kutapunguza asilimia 80 ya wagonjwa wa
saratani waliokuwa wanapelekwa nje ya nchi kwa ajili ya kipimo hicho na kwamba
Serikali itaweza takribani shilingi bilioni 5 kwa mwaka zilizokuwa zinatumika
kwa ajili ya kulipia wagonjwa waliokuwa wakienda nje ya nchi kwa ajili ya
kipimo hiki.
Amesema Serikali itasogeza huduma ya tiba ya saratani katika ngazi ya
Hospitali za Kanda ikiwa ni pamoja na Hospitali ya Bugando Mwanza, Hospitali ya
Kanda ya Kaskazini KCMC na Hospitali ya Rufaa ya Kanda za Nyanda za Juu Kusini,
jijini Mbeya.
“Vilevile, katika mwaka 2018/2019, Serikali itaimarisha upatikanaji wa
huduma za kibingwa katika hospitali za rufaa za mikoa kwa kuboresha miundombinu
ya kutolea huduma za afya ikiwa ni pamoja na majengo, vifaa tiba na madaktari
bingwa. Jumla ya shilingi bilioni 40 zimetengwa kwa ajili ya kuimarisha
hospitali hizi,” amesema.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali kwa kushirikiana na washirika wa
maendeleo kupitia Mradi wa Lipa Kulingana na Matokeo (Education Performance for
Results - EP4R) itaimarisha miundombinu kwenye shule zenye uhitaji mkubwa.
“Katika mwaka 2018/2019, Serikali itatumia shilingi bilioni 155.58 kwa
ajili ya ukarabati wa shule kongwe 25, ununuzi wa vifaa vya maabara, ujenzi wa
mabwalo 85, vyumba vya madarasa 2,000 na motisha kwa Halmashauri kutokana na
ufanisi katika utekelezaji wa vigezo vya EP4R,” amesema.
Amesema kwa sasa, Serikali inatarajia kuajiri walimu 4,785 wa shule za
msingi zenye uhitaji mkubwa na kwamba tayari imeshatangaza nafasi za ajira kwa
walimu 2,000 wa masomo ya sayansi, hisabati na lugha ambao watapangwa kwenye
shule za sekondari zenye uhitaji mkubwa.
Amesema kuwa Serikali imetangaza nafasi za ajira kwa mafundi sanifu
maabara 160 ambao nao pia watapangwa kwenye shule zenye uhaba wa wataalamu hao.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.