*Ni baada ya Serikali na wananchi kulinda rasilimali za nchi
IMEELEZWA
kuwa jitihada za Serikali za kulinda rasilimali za nchi na ushirikiano
kutoka kwa wananchi zimesababisha ongezeko kubwa la idadi ya wanyama
pori, hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi yenye wanyama wengi barani
Afrika.
Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa ameyasema hayo leo (Ijumaa, Juni 29, 2018) katika
hotuba yake aliyoitoa bungeni wakati wakuahirisha Mkutano wa 11 wa Bunge
jijini Dodoma.
Amesema
ili kuitumia vema fursa ya kuwa na vivutio vingi ikiwemo wanyamapori
wengi na kuleta tija kwa nchi, Serikali imeendelea kuandaa utambulisho
wa Tanzania Kimataifa (Destination Branding), lengo likiwa ni
kuitambulisha Tanzania kama kituo mahsusi cha utalii duniani.
“Tunalenga kuvutia
wageni wa kimataifa waje kuitembelea Tanzania, kuongeza wigo wa
kutangaza vivutio na kufanya vivutio vya utalii vifahamike duniani. Pia,
Serikali inakamilisha mchakato wa kuanzisha Channelmaalum katika Television ya Taifa (TBC1) kwa ajili ya kutangaza utalii,” amesema.
Waziri
Mkuu amesema maandalizi ya kuanzisha studio ya kutangaza utalii kwa
njia ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) yanaendelea vizuri,
ambapo studio hiyo itawezesha kutambua, kufuatilia na kuwasiliana moja
kwa moja na watu wanaofuatilia Tanzania na vivutio vyake.
Pia,
Serikali inakusudia kuanzisha chombo kitakacho simamia fukwe za bahari,
mito na maziwa lengo la hatua hiyo ni kuimarisha utalii wa fukwe Bara
na Visiwani kwa kujenga hoteli, maeneo ya mapumziko na michezo
mbalimbali.
Wakati huo huo,
Waziri Mkuu amezungumzia jitihada zinazofanywa na Serikali katika
kukabiliana na changamoto ya migogoro ya matumizi ya ardhi miongoni mwa
watumiaji kwa kuunda timu ya kisekta ikijumuisha watendaji wa sekta
mbalimbali zinazohusika kwenye masuala hayo.
Sambamba
na hilo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeandaa mipango ya matumizi ya
ardhi, kupima mipaka ya vijiji, kutunga na kurekebisha sera, sheria na
kuandaa mipango mbalimbali ya kuboresha matumizi na utawala wa ardhi.
Kadhalika,
Waziri Mkuu amesema Serikali imeandaa mipango ya kupanga, kupima na
kumilikisha kila kipande cha ardhi nchini. “Ni matumaini yangu kwamba
programu hii ikitekelezwa, ardhi itatoa mchango mkubwa katika maendeleo
ya kiuchumi na kijamii na pia kudhibiti migogoro ya ardhi,”.
Waziri
Mkuu amesema katika mwaka wa fedha 2018/19, Serikali itaendelea kutatua
migogoro inayojitokeza na pia kutoa elimu kwa umma ili watumiaji wote
wa ardhi waweze kuzingatia mipango ya matumizi ya ardhi inayoandaliwa
katika vijiji.
Amesema
katika juhudi za kudhibiti migogoro kwenye maeneo mbalimbali ya
utawala, jumla ya vijiji 11,256 kati ya vijiji 12,545 vilivyopo nchini
vimepimwa, hiyo ni sawa na asilimia 90 ya vijiji vyote, huku lengo
likiwa ni kupima mipaka ya vijiji vyote na kuvipatia vyeti vya kijiji
kwa kushirikiana na wadau wa maendeleo.
“Hatua
hii itasaidia kwa kiwango kikubwa kutatua migogoro ya mipaka kati ya
vijiji. Ili kuharakisha kasi ya upimaji nchini, Serikali itaendelea
kutumia makampuni binafsi ya upimaji na upangaji makazi kwa vibali
maalum,”.
Akizungumzia
kuhusu hifadhi ya mazingira, Waziri Mkuu amesema misitu inaendelea
kukatwa hovyo kwa sababu mbalimbali ikiwemo matumizi ya nishati ya mkaa
na kuni, ili kukabiliana na tatizo hilo Serikali itaendelea kuhamasisha
matumizi ya nishati mbadala kote nchini.
Amesema
Serikali itashirikiana na sekta binafsi kuweka utaratibu mahsusi wa
kuwawezesha na kuwaratibu wajasiramali wanaojishughulisha na nishati
mbadala ili kuwa na uzalishaji wa kutosha wa nishati hiyo na iweze
kusambazwa katika maeneo yote nchini.
Aidha,
Serikali itaendelea kuboresha na kukamilisha Mkakati wa Tungamotaka
(National Biomass Energy Strategy) na kusambaza kwa wadau nchini ili
kuratibu vyema upatikanaji na matumizi ya nishati hiyo.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.