*Ni katika ukusanyaji wa mapato na nidhamu ya matumizi
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka watendaji wa Serikali katika ngazi zote
wawajibike ipasavyo kwenye ukusanyaji wa mapato na kuwa na nidhamu
katika matumizi ya fedha na rasilimali za Taifa.
Pia,
Waziri Mkuu amesema Serikali itaimarisha ukaguzi katika ngazi zote na
ufuatiliaji wa karibu wa miradi ya maendeleo na kufanya tathmini za mara
kwa mara ili kuhakikisha kwamba miradi na kazi zitakazofanyika
zinawiana na thamani ya fedha (Value for money) za umma zinazotolewa na
Serikali.
Waziri
Mkuu ametoa agizo hilo leo (Ijumaa, Juni 29, 2018) katika hotuba yake
aliyoitoa bungeni wakati wa kuahirisha Mkutano wa 11 wa Bunge jijini
Dodoma.
Vilevile,
Waziri Mkuu amesema taasisi zote za Serikali zinasisitizwa kutumia
mifumo ya kieletroniki kukusanya mapato na wafanyabiashara wote
wanahimizwa kutumia mashine za EFD na kulipa kodi kwa hiari.
Amesema
Serikali imedhamiria kuhakikisha kwamba malengo ya ukusanyaji wa mapato
na matumizi yanazingatia bajeti iliyoidhinishwa na Bunge. “Viongozi na
watendaji wote wanapaswa kuzingatia sheria, kanuni na taratibu za
matumizi ya fedha za umma katika eneo la ukusanyaji wa mapato,”.
Waziri
Mkuu amesema Serikali itasimamia ipasavyo utekelezaji wa bajeti
sambamba na kuongeza uwajibikaji na nidhamu ya matumizi ya fedha
zilizoelekezwa katika vipaumbele mbalimbali kama ilivyoidhinishwa na
Bunge.
Amesema
katika utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya mwaka 2018/2019, Serikali
itashirikiana na sekta binafsi, wadau wa maendeleo na wananchi wote kwa
ujumla ili kufikia malengo yaliyokusudiwa.
Waziri
Mkuu ameongeza kuwa katika mwaka 2018/2019, Serikali imepanga kutumia
jumla ya sh. trilioni 32.48. Kati ya fedha hizo, sh. trilioni 20.47
zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya kawaida sawa na asilimia 63 ya
Bajeti na sh. trilioni 12.01, sawa na asilimia 37 ya bajeti yote
zimetengwa kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
Katika hatua nyingine,
Waziri Mkuu ametoa wito kwa wadau wa kilimo, mifugo, uvuvi na sekta
nyingine watumie fursa mbalimbali zinazopatikana katika utekelezaji wa Awamu ya Pili ya Mpango ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo (ASDPII),ili kutimiza ndoto ya Taifa kufikia uchumi wa kati unaoongozwa na viwanda ifikapo mwaka 2025.
Aidha,
Waziri Mkuu ameziagiza taasisi zote zinazohusika na utekelezaji
wa ASDP II, ziimarishe usimamizi na ufuatiliaji ili utekelezaji wa
mpango huo uwe na mafanikio makubwa.
Amesema
mpango huo unaweka mkazo katika maeneo makuu manne, ambayo ni usimamizi
endelevu wa matumizi ya ardhi na maji katika kilimo; kuongeza tija na
faida katika kilimo, mifugo na uvuvi; kukifanya kilimo kiwe cha
kibiashara na kuongeza thamani ya mazao na kuwajengea uwezo wadau wa
sekta katika uratibu, ufuatiliaji na tathmini.
Juni 4, 2018, Rais Dkt. John Magufuli alizindua Awamu ya Pili ya Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo nchini (ASDP II), ikiwa na lengo la kuongeza
tija na uzalishaji katika mnyororo wote wa thamani ili kuvipatia
malighafi viwanda vitakavyoanzishwa na kupata ziada ya kuuza katika
masoko ya nje ya nchi na kupata faida kubwa.
.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.