Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera Bunge Kazi Vijana Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari wakati wa mkutano wa kutangaza tarehe ya kuanza rasmi kufanya kazi kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma(PSSSF) leo Jijini Dodoma.Kulia ni Mkurugenzi mkuu wa SSRA Dkt. Irene Isaka.
Na Mwandishi wetu
Serikali imetangaza rasmi kuanza kutumika kwa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumsihi wa Umma (PSSSF) kuanzia Agosti 1, mwaka huu.
Akizungumza na vyombo vya habari leo Jijini Dodoma, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu,Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amesema kuwa, Serikali imekamikisha maandalizi yote muhimu ya utekelezaji wa Sheria ya PSSSF na imeridhika kwamba Mfuko huo unaweza kuanza kutekeleza majukumu yake.
"Napenda kutangaza rasmi kwamba, kwa mamlaka niliyonayo chini ya kifungu cha 1(1) cha Sheria ya PSSSF nimeteua tarehe 1 Agosti, 2018 kuwa ndiyo tarehe rasmi ya kuanza kutumika kwa Sheria ya PSSSF", alisisitiza mhe. Mhagama
Waziri Mhagama amefafanua kuwa, kutokana na hatua hiyo wafanyakazi wote watakaoajiriwa katika sekta ya umma watasajiliwa katika Mfuko wa PSSSF na wale watakaoajiriwa katika sekta binafsi watasajiliwa katika Mfuko wa NSSF.
Anaongeza kuwa, Wanachama wote ikiwa ni pamoja na wastaafu na warithi waliopo katika mifuko inayounganishwa watahamishiwa katika mfuko wa PSSSF na haki na stahili zao zitaendelea kutolewa na mfuko huo bila kuathiriwa kwa namna yeyote ile.
Akizungumzia rasilimali, vitega uchumi, madeni, mifuko ya hiari na mikataba iliyokuwa chini ya mifuko inayounganishwa Waziri Mhagama amesema itahamishiwa katika Mfuko mpya wa PSSSF.
Pia Waziri Mhagama amewatoa hofu ya kupoteza ajira watumishi wote wa mifuko iliyounganishwa kwa kuwa watahamishiwa katika mfuko mpya ambako uongozi wa mfuko huo utawapangia majukumu yao kwa kuzingatia muundo wa taasisi.
Kuondoa sintofahamu Serikali kupitia Mamlaka ya Usimamizi ya Mifuko ya Hifadhi za Jamii (SSRA) imeandaa mkakati maalumu wa kutoa elimu kwa umma kuhusu sheria na kanuni za PSSSF ili kuhakikisha kwamba wanachama na wadau wote wa sekta ya hifadhi ya jamii wanakuwa na uelewa sahihi wa sheria hizo na mabadiliko yaliyofanyika.
Mbali na hayo, Waziri Jenista ameteua wajumbe wa Bodi ya Mfuko huo ambao ni Bi. Leah Ulaya, Bw. Rashidi Mtima, Dkt. Aggrey Mlimuka, Bi. Stella Katende, Bw. Thomas Manjati, Bw. Henry Katabwa, Bi. Suzan Kabogo pamoja na Bw. Jacob Mwinula.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.