WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amemuagiza Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Kigoma, Bw. Raphael Mbwambo afuatilie ujenzi wa jengo la ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Buhigwe, baada ya kutilia shaka makadirio ya ujenzi huo.
Amesema mbali na ujenzi wa ofisi hiyo ambayo msingi wake ulikadiriwa kutumia sh milioni 205 lakini Halmashauri imetumia zaidi ya sh, milioni 400, pia halmashauri hiyo imeweka makadirio makubwa ya ujenzi wa hospitali ya wilaya ambayo utekelezaji wake ni mgumu.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumatatu, Julai 30, 2018) wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri ya Buhigwe pamoja na wananchi wa wilaya hiyo baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa hospitali ya wilaya hiyo inayojengwa kwenye eneo la Ruheta.
“Kamanda wa TAKUKURU mkoa wa Kigoma fuatilia ujenzi wa jengo la ofisi ya Mkurugenzi wa Halmashauri ya Buhigwe na tunataka tujue ni nani aliyetengeneza makadirio hayo kwa sababu makadirio aliyoyafanya ni makubwa ulinganisha na mradi husika,” amesema.
Waziri Mkuu amesema “Hospitali mnayojenga ni ya kawaida, haiwezekani mkaweka makadirio kama hayo ya kujenga wodi moja kwa sh milioni 851 wakati kuna baadhi ya maeneo nchini Serikali imetumia sh. milioni 500 kujenga kituo cha afya chenye majengo zaidi ya matano,”.
Kufuatia hatua hiyo , Waziri Mkuu ameuagiza uongozi wa wilaya hiyo kupitia upya makadirio waliyoyaweka katika miradi mbalimbali ya ujenzi wanayoitekeleza kwa kuwa makadirio waliyoyaweka ni makubwa na yatakwamisha miradi yao.
Kadhalika, Waziri Mkuu amewataka wakuu wa idara wahakikishe wanasimamia vizuri majukumu ya idara zao na kuyatekeleza ipasavyo. “kila mtumishi wa wilaya hii awajibike kwenye eneo lake na si vinginevyo,”.
Awali, akimkaribisha Waziri Mkuu, Mkuu wa wilaya ya Buhigwe, Brigedia Jenerali, Marco Gaguti alisema wilaya hiyo inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo ya wahamiaji haramu, ambapo kwa kipindi cha mwaka mmoja wamekamata wahamiaji haramu 1,054.
Mkuu huyo wa wilaya alisema zoezi la kuwasaka wahamiaji hao limesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza uharifu pamoja na matukio ya utekaji wa kutumia silaha unaofanywa na raia wa nchi jirani wanaoingia nchini kinyume cha taratibu kwa kushirikiana na wananchi wasiokuwa waaminifu.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.