WAZIRI MKUU Kassim
Majaliwa amempokea Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Lee Nak-yon
ambaye amewasili nchini leo saa 12:30 jioni (Jumamosi, Julai 21, 2018) kwa ziara ya
kikazi ya siku tatu.
Kwenye uwanja wa ndege,
Waziri Mkuu huyo wa Jamhuri ya Korea alipokelewa pia na Waziri wa Mambo ya Nje,
Dk. Augustine Mahiga, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Eng. Isack
Kamwele, Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, Naibu Waziri wa Viwanda,
Biashara na Uwekezaji, Eng. Stella Manyanya na viongozi wa mkoa wa Dar es
Salaam.
Waziri Mkuu Lee Nak-yon
anatembelea Tanzania ikiwa ni hatua ya kuimarisha uhusiano wa kidiplomasia
baina ya nchi hizi mbili. Hii ni mara ya kwanza kwa kiongozi wa ngazi ya juu wa
nchi hiyo kufanya ziara ya kiserikali tangu nchi hizo zianzishe mahusiano ya
kidiplomasia mwaka 1992.
Pia ameambatana na ujumbe
wa maafisa wa Serikali, wabunge na wafanyabiashara wakubwa ambao watashiriki
Kongamano la Kibiashara baina ya Korea na Tanzania (Korea-Tanzania Business
Forum) lililopangwa kufanyika kesho kutwa (Jumatatu, Julai 23, 2018) kwenye
hoteli ya Serena, jijini Dar es Salaam.
Kesho (Jumapili, Julai 22,
2018), Waziri Mkuu Lee Nak Yon atakuwa na mazungumzo rasmi ya kiserikali na
mwenyeji wake pamoja na viongozi kadhaa wa Serikali na pia kwa pamoja
watashuhudia uwekaji saini mkataba wa kuondoa hitaji la viza kwa watu wenye hati
za kusafiria za kidiplomasia na za utumishi (diplomatic and service passports).
Pia ataenda Ikulu
kumsalimia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe
Magufuli, atatembelea Makumbusho ya Taifa, Hospitali ya Mnazi Mmoja na kituo cha
utunzaji taarifa cha NIDA kilichopo Kibaha.
Anatarajiwa kuondoka
nchini Jumatatu jioni, Julai 23, 2018.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.