Saturday, October 27, 2018

TUTAENDELEA KUSHIRIKIANA NA SEKTA BINAFSI-MAJALIWA


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Serikali inathamini uwepo wa sekta binafsi nchini na kwamba inaendelea kushirikiana nayo katika kuboresha maendeleo ya Taifa.

Ameyasema hayo leo (Jumamosi, Oktoba 27, 2018) wakati alipokutana na bodi mpya ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania kwenye makazi wa Waziri Mkuu, jijini Dar es Salaam.

Waziri Mkuu ampongeza Mwenyekiti wa taasisi hiyo Bw. Salum Shamte na wajumbe wa bodi hiyo kwa kuchaguliwa kuingoza taasisi hiyo. Bodi hiyo mpya ilikwenda kujitambulisha.

“Serikali inadhamira ya dhati ya kushirikiana na taasisi hii kwa sababu ndio muwezeshaji wa kuifanya Tanzania kufikia uchumi wa kati kupitia sekta ya viwanda ifikapo 2025,” amesema.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa taasisi hiyo Bw. Shamte amesema sekta binafsi inatambua juhudi za Serikali katika kuboresha mazingira ya biashara nchini Tanzania.

“Sisi tupo tayari kushirikiana na Serikali kwa kuwabana wafanyabiashara ambao wanaenda kinyume na maadili na sheria, ila tunaomba Serikali ishirikiane nasi katika utekelezaji wake.”

Pia, Bw. Shamte ameiomba Serikali iendelee kutoa vivutio kwa biashara zinazoanza ili kuhamasisha uwekezaji kwa kuwa baadhi yake zimeonesha gharama kubwa za uzalishaji.

(mwisho)

No comments:

Post a Comment

Note: Only a member of this blog may post a comment.