Na; OWM (KVAU), Dodoma
Waziri wa Nchi, Ofisi ya
waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu
Mhe. Jenista Mhagama amezitaka asasi mbalimbali zinazoshughulikia maendeleo ya
vijana kuwa chachu ya maendeleo nchini.
Akizungumza wakati wa ufunguzi
wa kongamano la wadau wa asasi za maendeleo ya vijana nchini walipokutana kwa
lengo la kukuza uelewa katika kutekeleza programu ya kuwawezesha vijana kati ya
Ujerumani na nchi za Afrika (African – German Youth Initiative), Waziri Mhagama
alisema kuwa, Serikali kupitia Sera ya Taifa ya Maendeleo ya Vijana na Sera ya
Taifa ya Ajira imekuwa ikihamasisha wadau mbalimbali kuanzisha Miradi na
Programu zinazowawezesha vijana kupata ujuzi na uzoefu wa kuwaweza kujiajiri au
kuajiriwa katika Sekta mbalimbali ili waweze kuchangia kwenye maendeleo ya nchi.
“Vijana ndio chachu kubwa ya
maendeleo endelevu, hivyo ni vyema wakatumia fursa zilizopo kuleta mabadiliko
yatakayo kuwa na tija na mchango kubwa katika maendeleo ya taifa.” alisisitiza
Mhagama
Aliongeza kuwa Serikali ya
Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt.
John Pombe Magufuli imeendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuhakikisha kuwa
vijana wanawezeshwa ipasavyo kushiriki katika shughuli za kiuchumi.
Pia alifafanua kuwa, Serikali imekuwa
ikishirikiana na wadau wanaoshughulika masuala ya maendeleo ya vijana katika kuwajengea
ujuzi na uelewa vijana juu ya maendeleo. Hivyo aliipongeza Taasisi ya vijana ya
Tanzania Youth Coalition katika kujenga ustawi na maendeleo endelevu kwa vijana
ambao ndio wanufaika wa fursa ya programu hiyo ya mabadilishano ya vijana na
Mataifa mengine.
Aidha, Waziri Mhagama alitoa
wito kwa vijana nchini kufanya kazi kwa bidii na kuendelee kudumisha uzalendo,
amani na utulivu.
Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi
Kiuchumi Bi. Beng’i Issa alieleza kuwa Programu ya mabadilishano ya vijana (Exchange Program) imekuwa na manufaa makubwa sana
katika kuwajengea uwezo vijana kupitia fani mbalimbali zinazoleta mabadiliko ya
chanya katika Taifa.
Naye, Mkurugenzi wa Tanzania Youth Coalition (TYC) Bw. Lenin Kazoba alisema
kuwa kongamano hilo litakuwa na manufaa kwa vijana na asasi zinazoshughulikia maendeleo
ya vijana kwa kuweza kujadili kwa pamoja fursa zitakazoleta maendeleo kwa
vijana na jamii inayowazunguka.
Programu ya mabadilishano ya vijana kati ya Nchi ya Ujerumani na
Tanzania ilizinduliwa rasmi tarehe 30 Juni, 2016 Mjini Bonn, Ujerumani na
Waziri wa Uchumi wa Ushirikiano na Maendeleo Mhe. Gurd Muller ambapo Serikali
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu ilikuwa moja
kati ya Nchi Tatu (3) Barani Afrika zilizopewa heshima kubwa ya kuchaguliwa
kutekeleza mradi huo kwenye hatua ya majaribio kupitia Tanzania Youth Coalition
(TYC). Zaidi ya vijana 4,015 wamefaidika kupitia program hiyo kwa kupata ujuzi
na uzoefu wa fani mbalimbali.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.