*Awataka
Makatibu Wakuu wasimamie upandaji miti, maua
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekagua
ujenzi wa mji wa Serikali na kutoa maagizo 14 ambayo yataharakisha kukamilika
kwa kazi hiyo.
Ametoa maagizo hayo jana (Alhamisi, Januari 16, 2019) mara baada ya kukagua ujenzi wa
ofisi za wizara zote pamoja na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika
eneo la Ihumwa lililoko km. 17 kutoka jijini Dodoma.
Akizungumza baada ya kukagua ujenzi wa tenki
la maji lenye ujazo wa lita milioni moja, Waziri Mkuu alisema pamoja na spidi
anayoihimiza, bado wakandarasi wanapaswa kufanya kazi kwa kuzingatia ubora
unaotakiwa (quality).
“Kazi ya ujenzi ikamilike
tarehe 31 Januari 2019 kwa kasi na viwango vyenye ubora; mifumo ya ICT, umeme
na maji izingatiwe wakati wa ujenzi na zile sites
zenye upungufu wa nguvu kazi, vijana waongezwe na kazi ifanyike mchana na
usiku,” alisema.
Aliwataka waratibu wa zoezi la Serikali kuhamia Dodoma wakiwemo Wizara
husika na Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) wahakikishe kuwa wakandarasi ambao
hawajalipwa hususan vikosi vya ujenzi wanaojenga jengo la Wizara ya Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano wanalipwa.
Waziri Mkuu aliwataka Makatibu Wakuu wote wasimamie upandaji miti,
maua (hata landscaping) kwenye maeneo waliyopewa hasa katika kipindi hiki cha
mvua ili mandhari za ofisi zianze kuvutia.
“Wizara zifanye usafi ndani na nje wakati ujenzi
ukiendelea. Wizara kwa kushirikiana na TFS (Wakala wa Misitu) waendelee na
zoezi la upandaji miti na wataalam wa bustani wahusishwe mapema wakati huu wa ujenzi.
Lakini ninawaagiza Makatibu Wakuu wasimamie kwa karibu suala hili kwa sababu
eneo kubwa liko chini ya ofisi zao, hawa wakandarasi wakimaliza ujenzi watabomoa
mabati na kusafisha eneo la ujenzi tu,” alisema
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu ameagiza Wakala wa Ufundi na Umeme (TEMESA)
wahakikishe wanafungua ofisi ya muda katika Mji wa Serikali ili kurahisisha
usimamizi wa miundombinu inayowahusu.
Ametumia fursa hiyo kuwataka Wakala wa Majengo nchini
(TBA) wawasilishe taarifa ya maendeleo ya ujenzi kwa kila Wizara kwa kila hatua
inayoendelea.
Alisema ununuzi wa vifaa vya ujenzi kwenye wizara
mbalimbali hususan wakati wa ukamilishaji ujenzi, havina budi kununuliwa mapema
na vile vinavyounganishwa kama vile chuma za kenchi vifanyike kwenye eneo la
ujenzi (sites) ili vikaguliwe na TBA.
Kuhusu majengo ya ofisi ambayo kasi yake inasuasua
kama vile TAMISEMI, Madini na baadhi ya sites za Mzinga Holdings, Waziri Mkuu
Majaliwa amewataka Mawaziri na Makatibu Wakuu wachukue hatua stahiki kusimamia ujenzi
na kushauri ipasavyo.
Amesema wakandarasi kama Mzinga, SUMA JKT na NHC
waangalie namna ya kuwapa ajira za kudumu hususan zinazohusiana na ujenzi
mafundi wanaoshiriki shughuli za ujenzi Ihumwa.
Pia aliwataka Wakala wa Barabara Vijijini na Mijini
(TARURA) kwa kushirikiana na Wizara husika wahakikishe barabara za mji wa
Serikali zinatengenezwa angalau kwa kiwango cha changarawe ili zipitike kwa
urahisi katika kipindi cha mpito wakati taratibu za kudumu za kuweka lami
zikiendelea.
Ili kuokoa muda, Waziri Mkuu aliwataka wakandarasi
wahakikishe kazi zisizo za masharti kama vile kusuka nondo zitekelezwe kwa pamoja
wakati wa shughuli za ujenzi wa ujumla zikiendelea.
Akihitimisha, Waziri Mkuu alisema Ofisi ya Waziri Mkuu
ipatiwe taarifa ya idadi ya ajira iliyotengenezwa kutokana na ujenzi wa mji wa
Serikali hususan za wale ambao hawana ajira za kudumu kwa wakandarasi wanaotekeleza
ujenzi huo.
Waziri Mkuu
ameahidi kurudi Ihumwa Januari 31, mwaka huu ili akapokee funguo za ofisi za
wizara zote.
Mapema, akitoa taarifa ya ujenzi huo, Katibu
wa Kamati ya Kitaifa ya kuratibu zoezi la Serikali kuhamia Dodoma, Bw. Meshack
Bandawe alisema ujenzi wa tenki la maji lenye ujazo wa lita milioni umegharimu
sh. bilioni 3.6 na uko kwenye hatua za mwisho.
“Jiji la
Dodoma lina ziada ya maji ya lita za ujazo milioni 13.5, na kwa upande wa
umeme, kuna ziada ya megawati 20 kwa sababu uwezo wa kuzalisha umeme ni
megawati 48 na zinazotumika hadi sasa ni megawati 28 tu,” alisema.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.