Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi,
Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu inaratibu mafunzo maalum kwa mama wadogo yanayolenga
kuwawezesha kujitambua na kujithamini.
Mafunzo hayo yamefanyika katika
Ukumbi wa Halmashauri ya Uyui iliyopo Mkoani Tabora ambapo mama wadogo takribani 45 wamefundishwa
mada mbalimbali ikiwemo Ujasiriamali, kilimo biashara, taratibu za kuunda vikundi
vya uzalishaji mali, fursa za uwezeshaji wa vijana kiuchumi, malezi bora na familia,
afya na lishe.
Akizungumza wakati wa ufunguzi
wa mafunzo hayo Mkuu wa Wilaya ya Uyui Mhe. Gift Msuya amesema kuwa Serikali inatambua tatizo la mimba za utotoni na imeonesha dhairi
ufuatiliaji wa suala hilo kwa kuwachukulia hatua za kisheria wanaohusika na
vitendo hivyo.
“Takribani asilimia 45 ya
mabinti wanaoandikishwa kujiunga na kidato cha kwanza wanashindwa kumaliza
kidato cha nne kutokana na changamoto za mimba za utotoni, ndoa za utotoni na
umbali wa kupata huduma ya elimu.” alisema Msuya
Aidha, Msuya alieleza kuwa Halmashauri
yake imeanzisha kampeni ya “Nishike Mkono, Boresha Elimu Uyui” inayolenga
kuwainua watoto wa kike kwa kuwaboreshea mazingira ya elimu yatakayo wawezesha
kupata elimu bora.
Aliongeza kuwa Mkoa wa
Tabora umekuwa ukitekeleza kwa vitendo Mpango wa Kitaifa wa kutokomeza ukatili
dhidi ya wanawake na watoto wa mwaka 2017/18 – 2021/22 ambapo miongoni mwa
mikakati ya mpango huo ni kupunguza kiwango cha mimba kwa vijana wa kike.
Pia alitoa rai kwa vijana
walioshiriki mafunzo hayo, wakawe mabalozi wazuri kwa kufikisha elimu kwa
vijana wenzao ili wafahamu njia za kuepuka mimba zisizo tarajiwa na waweze
kuchangamkia fursa mbalimbali zitakazowawezesha kujikwamua kiuchumi.
Kwa upande wake Kaimu
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Vijana Bw. Julius Tweneshe alieleza kuwa Ofisi ya
Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu inaratibu programu ya mama
wadogo kitaifa inayokusudia kuwawezesha kupata mbinu na stadi za kujitambua, kuthubutu,
kufanya maamuzi sahihi na kujiwekea malengo katika maisha yao.
“Tutatumia mafunzo haya
kuhakikisha vijana wanachangamkia fursa za kiuchumi kupitia vikundi vya uzalishaji
mali ambavyo vitawasaidia kujipatia kipato na kuweza kutunza watoto wao.”
alisema Tweneshe
Naye Afisa Ustawi wa Jamii
wa Mkoa wa Tabora Bw. Baraka Mackona aliweza kuishukuru Ofisi ya Waziri Mkuu,
Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu kwa kuandaa mpango wa mafunzo hayo ya mama
wadogo kwa kuanza na Halmashauri ya Uyui na Kaliua.
“Tumeanza na halmashauri hizi
mbili kutokana na ukubwa wa tatizo, hivyo kuwajengea uwezo vijana wa kike
kutachangia kwa kiasi kikubwa kupunguza tatizo hili la mimba za utotoni.”
alisema Mackona
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.