Na; Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya
Waziri Mkuu anayeshughulika Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu
amezindua taarifa ya utafiti wa viashiria na matokeo ya ukimwi wa mwaka 2016 –
2017 (Tanzania HIV Impact Survey) tarehe 13 Aprili, 2019 Jijini Dodoma.
Akizungumza wakati wa hafla
hiyo alieleza kuwa utafiti huo ni kielelezo tosha kuwa Serikali imeendelea kupambana
na ugonjwa wa Ukimwi kwa kuonesha juhudi za kupungua kwa kiwango cha maambukizi mapya na kupungua kwa vifo
vinavyotokana na Ukimwi.
“Tafiti zinaonesha maambukizi
mapya ya VVU yamepungua kutoka watu 80,000 mwaka 2012 hadi kufikia watu 72,000
kwa mwaka katika mwaka 2017, vilevile takimu zinaonesha kupungua kwa vifo vinavyotokana
na Ukimwi kutoka watu elfu 70 kwa mwaka katika 2010 hadi kufikia vifo elfu 32
kwa mwaka katika kipindi cha mwaka 2017,” alieleza Mhagama
Alisema kuwa katika
kuthibitisha hilo, kiwango cha maambukizi ya Ukimwi nchini kinazidi kupungua
ambapo mwaka 2012 matokeo ya utafiti kama huo yalionesha kuwa kiwango cha
maambukizi kilikuwa ni asilimia 5.1 kwa watu wenye umri kati ya miaka 15 hadi
49 na matokeo ya mwaka 2016 – 2017 kiwango cha maambukizi kwa watu wenye umri
wa miaka 15 hadi 49 ni asilimia 4.7.
Waziri Mhagama alieleza kuwa
matokeo ya utafiti huo yanaonesha kuwa watu waliopima afya zao kwa hiari wanaongezeka
kutoka tafiti moja hadi nyingine, kati ya watu hao wanawake waliopima ni wengi
kuliko wanaume.
Sambamba na hilo, amewapongeza
wanawake kwa ujasiri na moyo wa kujali afya zao, pia kuwahimiza wanaume kujitokeza
kwa wingi kupima ili wafahamu hali zao za kiafya.
Hata hivyo, Waziri Mhagama
ametaka kila Mkoa na Halmashauri zote nchini kujadili matokeo ya utafiti huo
kwa undani katika kamati za VVU na Ukimwi kuanzia ngazi ya Mkoa, Wilaya, Kata
na Vijiji ili kuelewa hali ilivyo katika maeneo yao na kuandaa mipango
madhubuti ya kudhibiti ongezeko la maambukizi mapya ikiwemo kuongeza upatikanaji
wa huduma stahiki kwa watu wanaoishi na VVU (WAVIU).
Aidha, alitoa wito kwa
watanzania kujitokeza kwa wingi na kupima afya zao, pia jamii kuelimishwa na
kuhamasishwa juu ya umuhimu wa kutumia dawa za kufubaza Virusi vya Ukimwi kwa
watu wanaoishi na VVU (WAVIU).
Aliongeza kwa kuagiza
TACAIDS na Baraza la Watu wanaoishi na Ukimwi (NACOPHA) kuongeza jitihada dhidi
ya unyanyapaa na ubaguzi.
Kwa Upande wake Naibu Waziri
wa Afya, Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Harusi Said Suleiman alisema kuwa
taarifa ya utafiti huo itasaidia watunga sera na waratibu wa miradi kufuatilia
na kufanya tathmini ya miradi iliyopo kuandaa mikakati mipya kuhusiana na
masuala ya Ukimwi hapa nchini.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa
Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania Bara (TACAIDS), Dkt. Leonard Maboko alisema
kuwa Tume ya Kudhibiti Ukimwi Tanzania imekuwa ikiratibu zoezi hilo la utafiti
kila baada ya miaka mine na tafiti tatu zimeshafanyika mwaka 2003 – 2004, 2007 –
2008 na 2011 – 2012.
Pia, Kaimu Mtakwimu Mkuu wa
Serikali, Dkt. Albina Chuwa alisema kuwa malengo ya msingi ya utafiti utafiti
huo yalikuwa ni kutoa makadirio ya mwaka ya Kitaifa ya maambukizi mapya ya VVU
miongoni mwa watu wenye umri wa miaka 15 hadi 64, na kutoa makadirio ya hali
halisi ya upimaji wa VVU Kitaifa na Kimkoa.
“Utafiti wa aina hii ni wa
kwanza kufanyika hapa nchini kwa kuwa umeangalia vitu vingi na umeshirikisha
watu wa rika lote na viashiria vingine tofauti na tafiti nyingine zilizofanyika
hapo awali,” alisema Chuwa.
Utafiti wa Viashiria vya Ukimwi
na Matokeo yake wa Mwaka 2016 – 2017, ulitekelezwa kwa kushirikiana baina ya
Ofisi ya Takwimu (NBS), Ofisi ya Mtakwimu Mkuu Zanzibar na ICAP Tanzania,
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Wizara ya Afya –
Zanzibar na Tume ya Kudhibiti Ukimwi Zanzibar (ZAC), Maabara ya Taifa ya Afya
za Jamii, Uhakiki, Ubora na Mafunzo, Mpango wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi
(NACP), na Kitengo Shirikishicha Ukimwi, Kifua Kikuu na Ukoma, Zanzibar
(ZIHTLP) kwa kushirikiana na wadau kutoka shirika lisilo la Kiserikali Centers
for Disease Control and Prevention (CDC).
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.