*Asisitiza wanaume wapime VVU ili wajue
hadhi zao, wasitegemee wake zao
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wakazi wa
Dodoma wajitokeze kwa wingi kuchangia damu ili iweze kutumika kuokoa maisha ya
wengine.
Ametoa kauli hiyo hilo leo (Jumanne, Aprili 30, 2019)
wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa Dodoma waliohudhuria kilele cha
maadhimisho ya miaka 10 ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) yaliyofanyika
kwenye viwanja vya Mwl. Nyerere, jijini Dodoma.
Amesema Serikali inaendelea na kampeni ya
kuhakikisha vituo vya afya na hospitali vinakuwa na akiba ya kutosha ya damu kwa
ajili ya wagonjwa wenye kuhitaji damu.
“Tunawasihi Watanzania waende kuchangia damu
ili benki ya damu iwe na akiba ya kutosha endapo mtu ataenda pale kufanyiwa upasuaji
na akapoteza damu nyingi, au awe amepata ajali au ameenda kujifungua, apate
damu kwa haraka kutoka kwenye benki yetu,” amesisitiza.
Akitumia wingi wa watu kwenye hafla hiyo,
Waziri Mkuu amesema: “Leo hii hapa Dodoma kuna hospitali kubwa ya Benjamin
Mkapa kule UDOM, tuna vituo vya afya kama kile cha Makole vyote vinahitaji
kutoa huduma hii lakini haitoshi. Tuliagiza kila penye mkusanyiko wa watu
wengi, lazima kujengwe banda la kupima afya na kuchangia damu.”
Akizungumziai kuhusu upimaji wa virusi vya
UKIMWI (VVU), Waziri Mkuu amesema kampeni inafanyika lakini kasoro iliyopo ni
kwamba wanaojitokeza kwa wingi kupima afya zao ni wanawake na wanaume hawapimi.
“Takwimu zilizopo zinaonyesha hivyo,” amesema.
“Mimi ndiye balozi wenu akinababa kwenye
kampebi ya kitaita ya upimaji VVU. Nataka niwahimize twende leo tukapime,
tusitegemee matokeo ya vipimo vya mke. Wengi mnasubiri matokeo ya mke, akisharudi
kutoka kupima na kusema niko safi, basi na wewe unaanza kufurahi unasema niko
safi, hapana!”
“Wanaume msijidanganye, nenda ukapime wewe
mwenyewe ujijue afya yako na mkeo naye apime ajijue ili nyumba nzima iwe na
uhakika kwamba mko salama. Kwa hiyo wanaume tukitoka hapa, twende tukapime,”
alisema.
Mapema, Mkuu wa Kitengo cha Damu Salama Mkoa wa
Dodoma, Dk. Leah Kitundya alimweleza Waziri Mkuu kwamba Hospitali ya Mkoa wa
Dodoma ina upungufu wa damu kwa sababu kuna matukio mengi yanayosababisha upungufu
wa damu,
“Tukisema kuwa tunakusanya chupa za kutosha,
tunahitaji tuwe na chupa 1,000 hadi 1,500 za damu lakini katika hali ya kawaida
huwa tunakusanya chupa za damu 850 hadi 950 tu,” alisema.
(mwisho)
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.