*Ahimiza
wananchi walinde minara ya mawasiliano popote pale ilipo
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema tangu Mfuko wa
Mawasiliano kwa Wote uanzishwe, Serikali imechangia shilingi bilioni 118 ili kuimarisha
huduma za mawasiliano ambapo wakazi zaidi ya milioni tano kwenye kata 703 zenye
vijiji 2,501 wameweza kufikiwa.
Ametoa kauli hiyo hilo leo (Jumanne, Aprili 30, 2019)
wakati akizungumza na mamia ya wakazi wa Dodoma waliohudhuria kilele cha
maadhimisho ya miaka 10 ya Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) yaliyofanyika
kwenye viwanja vya Mwl. Nyerere, jijini Dodoma.
“Ninayo furaha kubwa moyoni mwangu, ninaposhuhudia
mfuko huu ukitimiza miaka 10 huku sehemu kubwa ya nchi yetu ikiwa na
mawasiliano ya uhakika. Napenda niwakikishie kwamba Serikali itaendelea
kupeleka mawasiliano kwenye sehemu zilizobakia hapa nchini ili wananchi wote
waweze kunufaika na uwepo wa mawasiliano,” amesema.
Amesema Serikali inatambua mchango wa watoa huduma za
mawasiliano katika kufikisha huduma hiyo sehemu mbalimbali, kwani kwa sasa kuna
baadhi ya minara imejengwa kwa ushirikiano baina ya kampuni za simu. “Nitoe rai
kwa wananchi wahakikisha mnailinda minara ya mawasiliano, na tena mhakikishe
popote ilipo inalindwa kwa mguvu zote ili tusirudishe nyuma juhudi za maendeleo,”
amesisitiza.
Waziri Mkuu ameipongeza Bodi na menejimenti ya
mfuko huo kwa kupeleka vifaa vya TEHAMA katika shule zaidi ya 500 nchini pamoja
na kutoa mafunzo ya TEHAMA kwa walimu 800.
Mapema, akimkaribisha Waziri Mkuu kuzungumza na
hadhira hiyo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi
Atashasta Nditiye alisema mfuko huo umejenga vituo 10 vya TEHAMA huko Zanzibar
(Pemba na Unguja) ili viwe ni vituo vya mafunzo ya TEHAMA.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa
Mawasiliano kwa Wote, Mhandisi Peter Ulanga alisema mpaka
sasa takribani asilimia 94 ya Watanzania wanapata huduma za mawasiliano mijini
na vijijini.
“Kama unavyotambua kwa ukubwa wa nchi yetu,
bado kuna maeneo yenye changamoto za mawasiliano. Mfuko umekwishaainisha jumla
ya kata 234 ambazo zabuni yake inatarajiwa kutangazwa Mei 2019,” amesema.
Alisema Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote pamoja
na kupeleka huduma za mawasiliano vijijini umeweza kuanzisha matumizi ya TEHAMA
katika shule za msingi na sekondari nchini ikiwa ni utekelezaji wa majukumu yake kama yalivyoainishwa katika sheria
iliyoanzisha mfuko huo.
“Katika kipindi cha miaka 10, Mfuko umeweza
kupeleka vifaa vya TEHAMA katika shule za Serikali. Kupitia mradi wake wa
kuunganisha shule na mtandao wa Internet, mfuko huo umepeleka vifaa hivyo kwenye
shule za serikali 503, ambapo kila shule ilipata kompyuta tano. Aidha, printa
zaidi ya 150 zimeweza kutolewa katika shule za umma za msingi na sekondari,
alisema Mhandisi Ulanga.
Alisema kupitia mradi wa kuunganisha shule za umma
na mtandao wa internet, Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano na kampuni ya Satelaiti
ya Avanti Communications, imeweza kuunganisha shule 301 na mtandao wa internet.
Aidha,
Mhandisi Ulanga alisema Serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote kwa kushirikiana
na TAMISEMI na Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia umeweza kutoa mafunzo ya
TEHAMA kwa walimu 583 katika mwaka wa fedha 2017/2018 wa shule za umma kwa
ajili ya kuufanya mradi wa kupeleka vifaa vya tehama uwe endelevu.
“Lengo
hasa la mafunzo haya ni kutoa elimu ya kutatua matatizo ya awali katika vifaa
mbalimbali vya TEHAMA, ili kupunguza gharama za uendeshaji kwa vifaa vinavyopelekwa
shuleni na kuboresha namna ya kuandaa na kufundisha masomo mbalimbali. Mwaka
huu wa fedha 2018/2019 tumetoa mafunzo kwa idadi hiyo hiyo ya walimu,” alisema.
Alitumia
fursa hiyo kuwashukuru TAMISEMI, Wizara ya Elimu, Taasisi ya Teknolojia ya Dar
es Salaam (DIT) na Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM) kwa kufanikisha mafunzo hayo.
(mwisho)
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.