Mkurugenzi wa Kitengo cha Dharura na Majanga,
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto, Dkt. Eliasi
Kwesi, akiendesha kikao leo Jijini Dodoma,
cha maandalizi ya zoezi la Kupima
Utayari wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kukabiliana na
magonjwa ya mlipuko mipakani, litakalofanyika mpakani mwa Tanzania na Kenya
kwenye eneo la Namanga, kuanzia tarehe
11 hadi 14 Juni.
Na. OWM, DODOMA.
Kufuatia nchi za Kanda ya Afrika Mashariki kuwa katika hatari ya
kuathirika na magonjwa ya mlipuko kama Homa ya Bonde la Ufa, Mafua Makali ya
Ndege na Ebola, na kwa kuwa magonjwa hayo husambaa kutoka nchi moja kwenda nchi
nyingine, Tanzania inatarajia kuandaa zoezi la Kupima Utayari wa nchi wanachama
wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Kukabiliana na magonjwa ya mlipuko mipakani, litakalofanyika
mpakani mwa Tanzania na Kenya kwenye eneo la Namanga, kuanzia tarehe 11 hadi 14 Juni mwaka huu.
Zoezi
hilo, litazingatia Dhana ya Afya moja ambayo hujumuisha sekta ya afya ya binadamu, wanyamapori, mifugo
na mazingira katika kujiandaa, kufuatilia na kukabili magonjwa
yanayoathiri binadamu. Jumla ya washiriki 150
ambao watatoka Sekretarieti ya Afrika Mashariki, Kenya na Tanzania washiriki 130
kutoka ngazi ya taifa, mkoa na wilaya katika mpaka wa Namanga; pamoja na nchi
nyingine wanachama ambapo watakuwa watazamaji ikiwa ni Uganda, Burundi, Rwanda na
Sudani Kusini wanatarajiwa kushiriki zoezi hilo.
Akiongea,
mjini Dodoma leo, katika kikao cha maandalizi ya zoezi hilo kwa ngazi ya Taifa,
Mkurugenzi wa Kitengo cha Dharura na Majanga, Wizara ya Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee, na Watoto, Dkt. Eliasi Kwesi, amefafanua kuwa zoezi hilo linalenga kufanyia majaribio ya
utekelezaji wa Mipango ya Dharura ya Taifa na Kanda, Miongozo ya Utendaji na
kuwapa washiriki fursa ya kujifunza namna sekta zingine zinavyotekeleza
majukumu katika kuzuia na kupunguza madhara pamoja na kujiandaa kukabiliana na
maafa ya magonjwa ya mlipuko.
“Zoezi hili tunalenga kutathmini utaratibu wa
kutuma kikosi cha taifa cha dharura cha kukabili lakini pia kuhakiki matumizi ya maabara zinazohamishika,
kutathmini uwezo wa uchunguzi na usimamizi wa magonjwa ya mlipuko kwa vituo
vilivyopo mpakani kwa magonjwa ya mifugo na binadamu; kupima hatua za kujiandaa
kukabiliana katika viwanja vya kimataifa vya Jomo Kenyatta na Kilimanjaro.”
Alisisitiza Dkt. Kwesi.
Kwesi
alibainisha kuwa zoezi litaandaliwa kwa kuhusisha mlipuko wa virusi
vinavyoshabihiana na Homa ya Bonde la Ufa katika eneo la mpakani, ambapo
washiriki watahitajika kuonesha utayari wa kukabiliana na ugonjwa huo kwa kuzingatia mfumo wa Afya Moja.
Zoezi
hilo linafanyika nchini Tanzania kufuatia Kikao cha 11 cha Kawaida cha Mawaziri
wa Sekta ya Afya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kilichofanyika mwezi Machi,
2015, ambapo kilielekeza Sekretarieti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kuandaa
Zoezi la Nadharia la kukabiliana na magonjwa ya mlipuko katika mpaka wa
Tanzania na Kenya kwenye eneo la Namanga. Zoezi hilo ambalo litafanyika hapa
nchini linaratibiwa na Sekretarieti ya
Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa kushirikiana na nchi wanachama kwa ufadhili wa
Shirika la Maendeleo la Ujerumani la GIZ
na Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa.
MWISHO.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.