*Akaribisha wawekezaji kwenye TEHAMA, uchakataji
wa mazao ya kilimo na misitu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amefanya mazungumzo na Balozi wa Finland hapa
nchini, Mhe. Pekka Hukka na kumshukuru kwa jitihada za nchi hiyo kuisadia Tanzania
kuondokana na umaskini.
“Tunaishukuru Serikali ya Finland kwa misaada ambayo imeendelea kuitoa kama
njia ya kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tanzania za kuondoa umaskini
pamoja na kuongeza makusanyo ya mapato ili kukuza uchumi wa nchi yetu,” amesema
Waziri Mkuu.
Ametoa kauli hiyo leo (Alhamisi,
Mei 23, 2019) alipokutana na Balozi huyo anayemaliza
muda wake wa kazi hapa nchini, ofisini kwake bungeni jijini Dodoma.
Waziri Mkuu amemweleza balozi huyo kwamba Tanzania bado ina fursa za uwekezaji
na kwamba Serikali inaendelea kutengeneza mazingira rafiki na bora kwa uwekezaji.
“Sekta ambazo makampuni ya Finland yanaweza kuwekeza hapa nchini ni pamoja na
TEHAMA, nishati, usafiri, uchakataji wa mazao ya kilimo na misitu,” amesema.
Waziri Mkuu alimtakia heri Balozi Hukka ambaye anatarajiwa kuondoka nchini
mwishoni mwa mwezi huu kwenda Tunisia ambako ndiko kutakuwa na kituo chake
kipya cha kazi.
Kwa upande
wake, Balozi Hukka alisema ataondoka
Tanzania akiwa na kumbukumbu nzuri ambazo atazienzi na anataraji kukutana na Watanzania
wengine ili aendelee kukuza mahusiano yaliyokuwepo.
Alisema Serikali za Tanzania na Finland zilisaini mkataba wa programu
iitwayo Forestry and Value Chain Programme
(FORVAC) ambao unalenga kuongeza faida za kiuchumi na kijamii kwa kupitia sekta
ya misitu pamoja na kupunguza ukataji wa miti. “Malengo hayo yatafikiwa kwa
kukuza mnyororo wa thamani kwenye sekta ya misitu pamoja na kuimarisha mifumo
ya ufuatiliaji, sheria na sera katika sekta ya misitu,” alisema.
Finland inasaidia sekta ya misitu nchini Tanzania kupitia Programu ya Private Forestry Programme (PFP) ambayo ililenga
kuongeza mapato kwa wakazi wa vijijini katika Halmashauri 10 za Njombe TC,
Njombe DC, Makete, Ludewa, Kilombero, Mufindi, Kilolo, Madaba, Mbinga na Nyasa)
kwa kusaidia upandaji wa miti na kuongeza thamani ya mazao ya misitu.
Programu hiyo imesaidia kujenga uwezo kwa wahusika wote katika mnyororo
wa thamani wa biashara ya mazao ya misitu. Awamu ya kwanza ya programu hiyo
imesaidia kuongeza kipato cha familia zaidi ya 9,000 kwenye wilaya hizo.
Katika hatua
nyingine, Waziri Mkuu amekutana na Balozi
wa Uswisi hapa nchini, Mhe. Florence Mattli ambaye pia alienda kumuaga ofisini
kwake bungeni jijini Dodoma.
Waziri Mkuu
alimweleza balozi huyo dhamira ya Serikali ya Tanzania ya kudumisha ushirikiano
na Uswisi na kusisitiza kwamba iko tayari kufanya kazi na Balozi mpya wa Uswisi
atakayekuja kwa manufaa ya pande zote mbili.
“Ni muhimu sana
ushirikiano wa Tanzania na Uswisi ukadumishwa kwa kuzingatia pia masuala ya
biashara na uwekezaji hususan kwenye sekta za afya, kilimo, elimu na teknolojia,”
alisema Waziri Mkuu.
Alitumia fursa hiyo kuishukuru Serikali ya Uswisi kwa misaada ambayo
imeendelea kutolewa na nchi hiyo katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya
Tanzania za kuondoa umaskini hususan kwenye miradi ya afya, kilimo na uwekezaji
katika elimu na biashara kwa ajili ya kukuza uchumi.
Kwa upande wake, Balozi Mattli alisema Serikali ya
Uswisi imekuwa ikiunga mkono na kusaidia jitihada za kukuza uwazi na
uwajibikaji kwa watendaji wa Serikali na wale wasiokuwa wa Serikali kuzingatia
mazingira ya kitaasisi na kijamii yanayopiga vita masuala ya rushwa.
“Msaada huo wa kupambana na rushwa
umechangia kuimarisha ufanisi wa uendeshaji wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana
na Rushwa (TAKUKURU) na kukuza uelewa wa kijamii kuhusu masuala ya rushwa,”
alisema.
Alisema mwaka 2018, Serikali ya Uswisi
ilitoa dola za Marekani milioni 24 kusaidia Mpango wa Ukuzaji Ujuzi kwa Ajira
Tanzania, ambao ulianza kutekelezwa Agosti Mosi, 2018 kupitia Wizara ya Elimu,
Sayansi na Teknolojia.
“Mpango huo unalenga kuboresha
upatikanaji wa elimu bora kwa vitendo na kuimarisha mafunzo ya ufundi nchini.
Hivyo, mpango huo umechangia kuboresha matarajio ya vijana kwa kuwapatia ujuzi
katika kazi na ubunifu unaochangia kuondokana na suala la ukosefu wa ajira,”
alisema.
Alisema Serikali
ya Uswisi inasaidia maendeleo ya vijana kupitia Mpango wa Ajira ya Vijana (OYE)
ambao unalenga kuimarisha maisha ya vijana wa kiume na wa kike kwa kuwafundisha
fursa za ajira katika sekta za biashara, kilimo, nishati mbadala, usafi wa
mazingira na kuboresha ujuzi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Balozi wa Finland nchini, Mhe. Pekka Hukka kabla ya mazungumzo yao, ofisini kwa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma, Mei 23, 2019. |
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Balozi wa Switzerland nchini, Mhe. Florence Tinguely Mattli, ofisini kwa Waziri Mkuu, Bungeni jijini Dodoma, Mei 23, 2019. |
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisalimiana na Balozi wa Switzerland nchini, Mhe. Florence Tinguely Mattli kabla ya mazungumzo yao, Ofisini kwa Waziri Mkuu Bungeni jijini Dodoma, Mei 23, 2019. |
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.