NA;
MWANDISHI WETU
Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri
Mkuu (Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Bw. Andrew Massawe amekutana na
Wakurugenzi wa Taasisi zilizopo chini ya ofisi hiyo kwa lengo la kujadili kwa
kina maeneo watakayo shirikiana kwa pamoja katika mpango kazi wa mwaka 2019 –
2020 na kutoa maelekezo juu ya namna bora ya kuhudumia wananchi kulingana na
huduma zinazotolewa na taasisi hizo.
Akizungumza wakati akifungua
kikao hicho kilichofanyika katika ukumbi wa mkutano uliopo jengo la PSSSF
Jijini Dodoma, alisema kuwa Mwaka wa fedha 2019/2020 ni muhimu kukubaliana kwa
pamoja maeneo ambayo yatatekelezwa kwa ushirikiano ili kuimarisha utendaji wa
shughuli mbalimbali.
“Lengo kuu la kukutana kwetu
hapa ni kuangalia utekelezaji wa shughuli zilizopangwa kwenye mpango kazi wa
kila Taasisi katika mwaka huu wa fedha, na kubaini namna bora ya kutekeleza
maeneo hayo kwa ufanisi,” alisema Massawe.
Katibu Mkuu aliongeza kuwa kupanga
na kukubaliana maeneo ya ushirikiano katika utekelezaji wa mpango kazi
kutasaidia kuongeza tija katika utendaji wa kazi na majukumu ya kila siku.
“Ninapenda kuona tunakuwa mfano wa kuingwa kwa
kujijengea mwenendo mzuri wa kushirikiana katika utendaji ili kufanikisha
shughuli nyingi kwa wakati mmoja,” alisisitiza Massawe
Aidha, alitoa wito kwa wakuu
hao kuzingatia suala la mawasiliano na uhusianao kwa wadau na wateja
wanaowahudumia ikiwemo kufanyia kazi malalamiko yanayotolewa kwa wakati.
Kwa Upande wake Kaimu Mtendaji
Mkuu wa Wakala wa Afya na Usalama Mahala Pa Kazi (OSHA), Bi. Khadija Mwenda alieleza
kuwa ushirikiano na taasisi nyingine na wizara ni fursa pekee itakayo wawezesha
kutekeleza dhamira na mikakati waliyopanga ili kuleta maendeleo.
Naye Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko
wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Bw. Masha Mshomba alisema kuwa yapo maeneo mengi
ya kushirikiana kwa pamoja na mpango kazi wa mwaka ni sehemu ya utekelezaji wa maazimio
yatakayo wasaidia kuwa na ushirikiano endelevu katika maeneo mbalimbali.
Kikao hicho kiliudhuriwa na
Wakurugenzi na Wataalamu wa Mipango na Bajeti kutoka Mfuko wa Hifadhi ya Jamii
kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), Mfuko wa Taifa wa Hifadhi
ya Jamii (NSSF), Mfuko wa Fidia kwa Wafanyakazi (WCF), Wakala wa Usalama na
Afya Mahala Pa Kazi (OSHA) na Tume ya Usuluhishi na Uamuzi (CMA).
MWISHO
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.