Na; Mwandishi Wetu
Naibu Waziri, Ofisi ya
Waziri Mkuu anayeshughulia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde (Mb)
amewataka vijana kuenzi mchango wa Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere
kwa kuwa wazalendo na wenye mshikamano katika kujenga Taifa.
Mhe. Mavunde amesema hayo
wakati wa hafla fupi ya kuwaaga vijana kutoka Mkoa wa Songwe, Arusha, Tanga, Kaskazini
Unguja na Kusini Unguja kabla ya kupanda Mlima Kilimanjaro ikiwa ni ishara ya
kumbukizi ya miaka 20 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwl. Nyerere iliyofanyika Mkoani
Kilimanjaro katika Hifadhi ya Taifa ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA).
Alisema kuwa vijana
wanapaswa kuwa wazalendo kwa kuiga kivitendo yale yote yaliyotendwa na waasisi
wa taifa hili, Mwl. Julius K. Nyerere na Hayati Mzee Abeid Karume kwa kuendelea
kudumisha upendo, amani na mshikamo kwa mustakabali wa Taifa.
“Vijana waliowengi kipindi
hiki wameweka pembeni uzalendo wa kulipenda taifa lao hali ambayo inatubidi
tujitahmini na kuenzi falsafa walizokuwa nazo waasisi wetu ambao waliweka
maslahi ya Taifa mbele wakati wote,” alisema Mavunde
Akitolea
mfano wa Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli,
namna
ambavyo amekuwa mstari wa mbele katika kuwatumikia wananchi kwa
kutekeleza masuala mbalimbali ya kitaifa wakati wote ili nchi isonge
mbele kimaendeleo.
Pia alitumia nafasi hiyo
kuwapongeza vijana waliopanda mlima huo awamu ya kwanza na awamu hii ya pili
kwa kuonesha ushujaa na uzalendo kwa Taifa lao ikiwemo kuwa mabalozi wazuri
katika kutangaza sekta ya utalii.
Aidha, Naibu Waziri Mavunde
alitoa wito kwa vijana kuacha kukaa kwenye vijiwe na kujihusisha kwenye mambo
yasio na tija, bali wajishughulishe kwenye miradi mbalimbali itakayo wawezesha
kiuchumi na kusaidia kukua kimaendeleo, kwa kuwa waasisi wa taifa walikuwa
wachapakazi, waadilifu na wabunifu ambao ni mfano mzuri wa kuigwa.
“Hakuna nchi yoyote dunia
ambayo inaweza kuendelea pasipo kuhusisha nguvu kubwa ya vijana katika
maendeleo ya taifa,” alieleza Mavunde
Aliongeza kuwa ili kufikia
malengo kwenye uchumi wa viwanda ni lazima vijana wazingatie uzalendo, utaifa na bidii katika kazi.
Kwa upande wake, Mkuu wa
Wilaya ya Moshi, Mhe. Kippi Warioba alisema kuwa kitendo cha vijana hao kushiriki
katika kupanda Mlima huo ni jambo muhimu kwa taifa na inaashiria namna
gani vijana wameanza kutambua historia ya waasisi wa taifa lao.
Naye, Kiongozi wa Vijana hao
waliopanda Mlima Kilimanjaro Bw. Augustine Gusha aliunga mkono maelezo
yaliyotolewa na Naibu Waziri na alitumia nafasi hiyo kuwasihi vijana kudumisha
amani ya nchi wakati wote.
Katika Mbio za Mwenge wa
Uhuru Mwaka 2019, Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Maendeleo ya Vijana
inaratibu shughuli ya kupanda Mlima Kilimanjaro kwa Vijana 100 kwa ajili ya
kumbukizi ya Miaka 20 ya Kifo cha Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage
Nyerere. Awamu ya kwanza vijana walipanda mlima huo tarehe 26 Machi, 2019 na
awamu ya pili 26 Julai, 2019. Awamu ya Tatu itakuwa mwezi Oktoba.
MWISHO
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.