*Asisitiza kwamba
hakuna mbadala wa elimu bora
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameiagiza Tume ya Vyuo
Vikuu Tanzania (TCU) itafute mbinu bora zaidi na
kuvijengea uwezo vyuo vikuu binafsi ili visaidie kuongeza udahili.
“Tume itafute
mbinu bora zaidi ikiwa ni pamoja na kuvijengea uwezo vyuo vikuu binafsi ili
visaidie kuongeza udahili. Ni wakati muafaka kwa Tume kujipambanua kwenye
uwezeshaji na ushauri ili kuondoa taswira hasi miongoni mwa jamii kwamba kazi
kubwa ya TCU ni kuvifungia vyuo vikuu badala ya kuvisaidia kutatua changamoto
zinazovikabili,” amesema.
Waziri Mkuu
ametoa agizo hilo leo, (Jumatano, Julai 17, 2019) wakati
akifungua maonesho ya 14 ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia yanayoendelea kwenye
Viwanja vya Mnazi Mmoja, jijini Dar es Salaam. Maonesho hayo yatafungwa Julai
20, mwaka huu.
Amesema Serikali
inatambua kwamba vyuo vikuu binafsi ni washirika muhimu wa maendeleo ya sekta
ndogo ya elimu ya juu nchini. “Naomba nieleweke vizuri kwamba hakuna mbadala wa
elimu bora bali nasisitiza Tume ivisaidie vyuo vikuu kufikia viwango
vinavyotakiwa na siyo kuwapunguzia viwango vya matakwa ya usajili,” amesema.
Akitoa
ufafanuzi kuhusu idadi ndogo ya wahitimu wa elimu ya juu, Waziri Mkuu amesema takwimu
za kimataifa za ushiriki wa elimu ya juu zinaonesha kwamba kufikia mwaka 2017
ni asilimia moja hadi tatu tu ya Watanzania kwa kila Watanzania 100 wenye umri
chini ya miaka 25 wanapata elimu ya Chuo Kikuu.
“Idadi hii
ni ndogo zaidi ya majirani zetu wa Kenya wenye asilimia nne, Zambia asilimia nne
na Namibia asilimia 14. Bado tunayo kazi kubwa sana ya kufanya. Natoa maelekezo
kwa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia iongeze jitihada na mikakati ya
kuboresha uwiano huu ambao upo chini ikilinganishwa na majirani zetu,”
alisisitiza.
Amesema ili
kuongeza idadi ya Watanzania wanaopata nafasi ya elimu ya juu, ni lazima
tupange mikakati yetu kama nchi kwa kushirikiana na sekta binafsi, ambao ni
wadau wakubwa katika elimu ya juu. “Taarifa nilizonazo ni kwamba, kati ya
wahitimu wote wa vyuo vikuu kwa mwaka, asilimia 25 wanatoka katika vyuo vikuu
binafsi. Mchango huu si mdogo, na ningetamani uongezeke zaidi,” amesema.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amewapa changamoto wakuu wa vyuo vikuu nchini
wabadilishe mtazamo wao juu ya upimaji wa ufanisi wa wahitimu na badala yake upimaji
wao ujielekeze kwenye kutoa suluhisho na kubadilisha maisha ya Watanzania badala
ya kutumia machapisho ya kitaaluma.
“Kipimo cha
ufanisi katika taaluma ilikuwa ni machapisho ya kitaaluma, ambapo mengi ya hayo,
jamii pana haifaidiki nayo. Sasa ni wakati mwafaka kutafakari iwapo kipimo
hicho kinatosheleza. Kwa vyuo vikuu ambavyo mmehudhuria hapa leo, naomba niwape
mtazamo tofauti. Kipimo cha ufanisi wa wanataaluma wa Tanzania, kuanzia sasa
kinafaa kiwe ni kiasi gani taaluma yao inawafikia na kubadilisha maisha ya
wananchi, na kiwango cha bidhaa na hatimiliki (patents) zilizozalishwa na kusajiliwa
na wasomi wetu waliopo vyuo vikuu.”
Amesema matarajio ya Serikali ni kuona kwamba tafiti na vipimo vya ufanisi kwenye vyuo vikuu viwe ni kiasi gani vyuo hivyo vinatoa bidhaa mbalimbali za kuleta ajira pamoja na kukabiliana na matatizo ya kijamii. “Ningefurahi iwapo kuanzia sasa kipimo cha ufanisi wa vyuo vikuu vyetu iwe katika kupima jitihada za vyuo vyetu kuisaidia Serikali katika azma yake ya kufikia kwenye uchumi wa kati,” amesema.
“Huu ni wakati muafaka kuanza kupima ufanisi wa wakuu wa vyuo
kwa kuangalia kiasi gani mazao ya Chuo Kikuu hicho yamewafikia wananchi na pia
katika utekelezaji wa mikakati ya maendeleo ya Serikali, hasa mapinduzi ya
viwanda,” amesisitiza.
Mapema, akielezea kuhusu
maonesho hayo, Mwenyekiti wa TCU, Prof. Jacob Mtabaji aliwataka wahitimu wa
kidato cha sita wanaoomba kujiunga na vyuo vikuu, wasome kwa umakini mwongozo
uliowekwa kwenye tovuti na wasikubali kupitia mawakala wanaodai kuwa wanaweza
kufanya usajili kwa niaba yao. Pia aliwataka wazingatie kalenda ya udahili.
Akielezea changamoto za elimu ya juu nchini, Prof.
Mtabaji alisema kuna uhaba wa wahadhiri wenye sifa stahiki katika vyuo vikuu
vingi na akawaomba wakuu wa vyuo hivyo wawasomeshe wahadhiri katika ngazi
mbalimbali ili wakirudi wajiunge na vyuo husika.
Naye Mkurugenzi
Mtendaji wa TCU, Prof. Charles Kihampa alisema taasisi 81 za elimu ya juu
zimeshiriki maonesho hayo ambapo taasisi 15 ni za nje ya nchi na taasisi 66 ni
za hapa nchini.
Akitoa shukrani, Mwenyekiti wa Kamati ya Watendaji
Wakuu wa Vyuo Vikuu na Vyuo Vikuu Vishiriki (CVCPT), Prof. Raphael Chibunda
alisema anaishukuru Serikali ya awamu ya tano kwa uboreshwaji uliofanywa kwenye
upatikanaji na upelekwaji kwa wakati wa fedha kutoka Bodi ya Mikopo. “Zamani,
sauala hili hiloi likuwa ni chanzo cha migomo mingi vyuoni lakini kwa sasa
limekwisha,” alisema.
Pia
aliishukuru Serikali kwa kukubali kurudisha jukumu la udahili wa wanafunzi
katika Seneti za Vyuo Vikuu kwani hapo nyuma lilikuwa sehemu ya mgogoro baina
ya TCU na vyuo vikuu.
(mwisho)
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.