*Mwanafunzi wake aibuka nafasi ya saba Kitaifa masomo ya lugha na sanaa
*Yaupandisha mkoa kutoka nafasi ya pili hadi nafasi ya kwanza Kitaifa
*Mkuu wa Mkoa wa Lindi atuma salamu kwa mikoa mingine ijipange
WAHENGA
walisema ‘penye nia pana njia’ usemi huu umejidhirisha katika matokeo
ya kidato cha sita kwa mwaka huu wa 2019, baada ya shule zote Mkoani
Lindi zikiongozwa na shule ya Sekondari ya Nyangao kufanya vizuri katika
matokeo hayo na kuufanya mkoa kushika nafasi ya kwanza katika mpangilio
wa ubora wa ufaulu nchini.
Ni
ukweli usiopingika kwamba hakuna aliyetarajia kuona mkoa wa Lindi
ukiibuka kidedea kwani kwa miaka mingi mikoa ya kusini ukiwemo Lindi
ilisifika kwa kuwa nyuma kielimu kutokana na matokeo yasiyoridhisha
yaliyokuwa yanapatikana.
Matokeo duni kielemu yalichangia kudorora kwa maendeleo ya mikoa hiyo kwa kiasi kikubwa.
Jitihada
mbalimbali zilizofanyika kwa ushirikiano wa Serikali, wazazi na wadau
wa maendeleo kuhakikisha mikoa hiyo inaondoka katika kundi la kuongozwa
zimezaa matunda kufuatia matokeo mazuri.
Hamasa
kubwa inajengwa kwa wazazi na walezi kutambua umuhimu wa elimu kwa
watoto wao kwa ajili ya faida yao na Taifa kwa ujumla. Kampeni kuhusu
kipaumbele cha elimu ndio ukombozi katika kupambana na umaskini imeleta
matokeo chanya mkoani Lindi.
Mara
baada ya uhuru Hayati Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Julius Nyerere
alihakikisha kuwa, Watanganyika wanakuwa na elimu ili waweze kujikomboa
kutoka utumwa wa wakoloni na kujiongoza katika kujieletea maendeleo
kwenye maisha yao.
Akizungumzia
kuhusu matokeo hayo Mkuu wa mkoa wa Lindi, Godfrey Zambi alisema kuwepo
kwa dhamira ya dhati iliyooneshwa na viongozi wa Serikali katika ngazi
mbalimbali, wanasiasa na wananchi wa mkoa wa Lindi ili kuboresha na
kuinua kiwango cha ufaulu imeanza kuonekana, ambapo kwa sasa mkoa
unaongoza matokeo kidato cha sita na kufaulisha wanafunzi wote.
Alisema
anamshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuwezesha mkoa huo kufanya vizuri katika
nyanja mbalimbali za kimaendeleo ikiwe kuongezeka kwa kiwango cha
ufaulu. Hali hiyo imetokana na mikakati mbalimbali iliyofanywa kati ya
walimu, wanafunzi na Serikali.
Alisema
hatua ya kwanza waliyoichukua ni kutafuta sababu za mkoa kutofanya
vizuri kielimu, baada ya kuzibaini waliweka mikakati ya kutatua
changamoto hizo kwa kusimamia mahudhurio ya wanafunzi kwa sababu
kulikuwa na utoro pia ukaguzi kwa walimu pamoja kuandaa majaribio ya mara kwa mara.
“Pia
tulikuwa tunafanya mikutano ya kujadili na kuweka mikakati ya kuinua
kiwango cha elimu katika mkoa wa Lindi kwa ushirikiano baina ya Serikali
na wadau wa masuala ya elimu. Tulikubaliana kufanya ziara za mara kwa
mara mashuleni pamoja na kuanzisha vituo kwa ajili ya wanafunzi
wanaojiandaa na mitihani.”
Kiongozi
huyo aliongeza kuwa hakuna mkoa uliondikiwa kuwa wa mwisho, waliamua
kufanya jitihada mbalimbali ili kuuwezesha mkoa wao kusonga mbele
kimaendeleo na wameanza kuyaona mafanikio, hivyo mikoa mingine
inayodhani kuwa itakuwa ya kwanza kila wakati ijipange.
Alisema
kuwa katika mkoa wao kulikuwa na shule ya Sekondari ya Nyangao ambayo
ilikuwa imeshapotea katika ramani, lakini kutokana na jitihada
mbalimbali zilizofanywa na wadau wa elimu shule hiyo imeibuka na kuwa ya
kwanza Kitaifa. “Hili ni jambo la faraja.”
“Niwapongeze
walimu wote na wanafunzi kwani shule zote tisa za sekondari za kidato
cha tano na sita mkoani hapa zimefanya vizuri katika matokeo ya kidato
cha sita na kuufanya mkoa kuongoza mikoa yote. katika shule hizo nane ni
za Serikali na moja inamilikiwa na mtu binafsi.”
Shule zilizofanya vizuri
Shule
ya Sekondari ya Nyangao iliyopo Halmashauri ya wilaya ya Lindi imeshika
nafasi ya kwanza Kitaifa kati ya shule 134 zenye wanafunzi chini ya 40,
ambapo kati ya wanafunzi 25 waliofanya mtihani wa kumaliza kidato cha
sita wanafunzi 22 walipata daraja la kwanza huku watatu waliosalia
walipata daraja la pili.
Mwanafunzi
wa shule hiyo ya sekondari ya Nyangao, Karimu Kassimu Muhibu (HKL)
ameibuka katika namba saba kati ya wanafunzi kumi bora waliofanya vizuri
Kitaifa katika masomo ya lugha na sanaa.
Mbali
na shule ya Sekondari ya Nyangao kupata matokeo hayo, shule zingine za
sekondari za mkoa wa Lindi zilizopata matokeo mazuri ni shule ya kutwa
ya Nachingwea iliyokuwa na watahiniwa 64 kati yake 49 walipata daraja la
kwanza na waliosalia 15 walipata daraja la pili.
Shule
ya sekondari ya kutwa ya Liwale kati ya wafunzi 186 waliofanya mtihani
wanafunzi 43 walipata daraja la kwanza, 121 walipata daraja la pili na
wanafunzi 22 walipata daraja la tatu.
Shule
ya sekondari ya Mbekenyera iliyoko wilayani Ruangwa ambayo kati ya
wanafunzi 98 waliofanya mtihani huo, wanafunzi 37 walipata daraja la
kwanza, 56 walipata daraja la pili huku wengine watano waliosalia
walipata daraja la tatu.
Shule
ya sekondari ya Kilwa ambayo ilikuwa na jumla ya wanafunzi 103
walioifanya mtihani huo, wanafunzi sita walipata daraja la kwanza, 76
walipata daraja la pili huku weingine 21 wakipata daraja la tatu.
Ni
dhahiri kwamba matokeo hayo ni ishara nzuri inayoashiria kuwepo kwa
mwamko wa kutosha na kukubali mabadiliko makubwa ya kielimu miongoni mwa
wananchi wa mkoa wa Lindi
Inatarajiwa
kuwa hatua hizo zitachangia kuongezeka kwa wasomi katika jamii za
wakazi wa mkoa huo, ambao kwa vyovyote vile wanafunzi hawa watakuwa
mabalozi wazuri wa kuhamasisha umuhimu wa elimu kwa wenzao ambao bado
wanasoma katika ngazi mbalimbali zikiwemo shule za msingi.
Wanafunzi
waliofanya vizuri katika matokeo ya kidato cha sita wanatarajiwa hapo
baadae kusaidia mkoa wa Lindi na nchi kwa ujumla katika kupambana na
changamoto mbalimbali zikiwemo za upungufu wa walimu, madaktari, wauguzi
na watumishi wengi kwa kuwa baada ya kumaliza masomo yao watajiunga na
vyuo kusomea taaluma mbalimbali.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.