Na; Mwandishi
Wetu
Serikali kupitia Ofisi ya
Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imefanikiwa kuwawezesha
vijana wapatao 18,000 kunufaika na mafunzo ya Kilimo cha kisasa kwa teknolojia
ya kitalu nyumba (Green house).
Hayo yamesemwa na Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na
Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alipotembelea na kukagua maendeleo ya
mafunzo hayo kwa vijana katika Wilaya ya Chemba na Kondoa, Jijini Dodoma.
Alisema kuwa Serikali
kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu iliamua kuanzisha Programu ya kukuza ujuzi nchini
kwa lengo la kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa kutosha ambao utakaowasaidia
kufanya shughuli zenye tija na zitakazowawezesha kujikwamua kuichumi.
“Programu hii ya Kilimo cha
kisasa kupitia teknolojia ya Kitalu Nyumba ni sahihi kwa vijana kwa kuwa aina
hiyo ya kilimo kitawahamasisha vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa kupenda na
kushiriki kwa wingi kwenye kilimo cha aina hiyo,” alisema Mhagama
Alieleza kuwa mradi huo
ulikusudia kutekelezwa kwenye Halmashauri zote nchini ambapo awamu ya kwanza
imefanikiwa kuwafikia vijana katika Mikoa 12 na Halmashauri 83 walioweza kupata
ujuzi na stadi za kazi ikionesha jitihada za Serikali katika kutatua changamoto
ya jira kwa vijana.
“Jumla ya vijana 100 katika
kila halmashauri wameweza kujifunza kati yao vijana 20 wamejifunza namna ya
kujenga vitalu nyumba na vijana 80 wamejifunza shughuli za kilimo katika kitalu
nyumba,” alisema Mhagama
Aliongeza kuwa mradi huo
umewajengea vijana hamasa katika kujishughulisha kwenye kilimo kwa kuwa
wataweza kulima katika eneo dogo na kupata mazao kwa wingi ambayo wataweza
kuuza nje ya nchi ama kwenye viwanda vilivyopo nchini.
“Sehemu kubwa ya mazao
mtakayozalisha kwenye vitalu nyumba kama vile Mbogamboga, Matango, Nyanya, Hoho
ni rahisi kupata soko nje ya nchi na kilimo cha aina hiyo akisubiri msimu huu
ni wa kupanda mazao fulani,” alisema Mhagama
Aidha Waziri Mhagama alitoa maagizo kwa viongozi
wa Halmashauri zilizonufaika na mradi huo kuhakikisha wanasimamia ipasavyo
shughuli zinazoendelea, ikiwemo kuwapatia vijana fursa za mitaji kupitia Mikopo
ya halmashauri itakayo wawezesha vijana kutengeza vitalu nyumba vyao binafsi sambamba
na kuwahamasisha kuanzisha viwanda vidogo vitakavyokuwa vinazalisha malighafi
zitokanazo kwenye vitalu nyumba hivyo.
“Halmashauri zote
zilizonufaika na mradi huu zihakikishe zinatengeneza mfumo madhubuti utakao
hakikisha mradi huo unakuwa endelevu pamoja na kuwahamasisha vijana wengi ili waweze
kunufaika na mafunzo hayo,” alisisitiza Mhagama.
Kwa upande wake Mkuu wa
Wilaya ya Chemba, Mhe. Simon Odunga aliahidi Mhe. Waziri kusimamia ipasavyo
mradi huo ikiwemo kuwawezesha vijana na kuwahamasisha vijana wengine kushiriki
kwa wingi kwenye teknolojia hiyo ya Kilimo cha Kitalu nyumba.
“Tutaunga mkono jitihada za
Serikali katika kuwawezesha vijana, tunaahidi kutunza mradi huu ili kusaidia
wananchi wa chemba kuweza kunufaika nao,” alisema Odunga
Naye mmoja wa vijana walionufaika
na mafunzo hayo Bw. Juma Ramadhani alisema kuwa mafunzo hayo yamekuwa chachu
kwao na yatawasaidia kuondokana na umaskini kwa kuwa wameweza kujifunza njia
bora za kilimo.
“Tunamshukuru Mhe. Rais,
Dkt. John Magufuli kwa kutuletea mradi huu inaonesha namna Rais wetu
anavyotupigania vijana, tunahaidi kutumia ujuzi tuliopata kuwaelimisha vijana
wenzetu ili na wao waweze kunufaika pia,” alisema Ramadhani
Katika ziara hiyo Waziri wa
Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na
Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama aliweza kutembelea na kukagua maendeleo ya
mafunzo kwa vijana kupitia Teknolojia ya kilimo cha Kitalu Nyumba (Green House)
katika Wilaya ya Chemba na Kondoa.
MWISHO
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.