Wednesday, September 18, 2019

SERIKALI YAWAWEZESHA VIJANA 18,000 MAFUNZO YA KILIMO KUPITIA TEKNOLOJIA YA KITALU NYUMBA

Na; Mwandishi Wetu
Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu imefanikiwa kuwawezesha vijana wapatao 18,000 kunufaika na mafunzo ya Kilimo cha kisasa kwa teknolojia ya kitalu nyumba (Green house).
Hayo yamesemwa na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama alipotembelea na kukagua maendeleo ya mafunzo hayo kwa vijana katika Wilaya ya Chemba na Kondoa, Jijini Dodoma.
Alisema kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu iliamua kuanzisha Programu ya kukuza ujuzi nchini kwa lengo la kuwawezesha vijana kupata ujuzi wa kutosha ambao utakaowasaidia kufanya shughuli zenye tija na zitakazowawezesha kujikwamua kuichumi.
“Programu hii ya Kilimo cha kisasa kupitia teknolojia ya Kitalu Nyumba ni sahihi kwa vijana kwa kuwa aina hiyo ya kilimo kitawahamasisha vijana ambao ndio nguvu kazi ya Taifa kupenda na kushiriki kwa wingi kwenye kilimo cha aina hiyo,” alisema Mhagama
Alieleza kuwa mradi huo ulikusudia kutekelezwa kwenye Halmashauri zote nchini ambapo awamu ya kwanza imefanikiwa kuwafikia vijana katika Mikoa 12 na Halmashauri 83 walioweza kupata ujuzi na stadi za kazi ikionesha jitihada za Serikali katika kutatua changamoto ya jira kwa vijana.
“Jumla ya vijana 100 katika kila halmashauri wameweza kujifunza kati yao vijana 20 wamejifunza namna ya kujenga vitalu nyumba na vijana 80 wamejifunza shughuli za kilimo katika kitalu nyumba,” alisema Mhagama
Aliongeza kuwa mradi huo umewajengea vijana hamasa katika kujishughulisha kwenye kilimo kwa kuwa wataweza kulima katika eneo dogo na kupata mazao kwa wingi ambayo wataweza kuuza nje ya nchi ama kwenye viwanda vilivyopo nchini.
“Sehemu kubwa ya mazao mtakayozalisha kwenye vitalu nyumba kama vile Mbogamboga, Matango, Nyanya, Hoho ni rahisi kupata soko nje ya nchi na kilimo cha aina hiyo akisubiri msimu huu ni wa kupanda mazao fulani,” alisema Mhagama 
 Aidha Waziri Mhagama alitoa maagizo kwa viongozi wa Halmashauri zilizonufaika na mradi huo kuhakikisha wanasimamia ipasavyo shughuli zinazoendelea, ikiwemo kuwapatia vijana fursa za mitaji kupitia Mikopo ya halmashauri itakayo wawezesha vijana kutengeza vitalu nyumba vyao binafsi sambamba na kuwahamasisha kuanzisha viwanda vidogo vitakavyokuwa vinazalisha malighafi zitokanazo kwenye vitalu nyumba hivyo.
“Halmashauri zote zilizonufaika na mradi huu zihakikishe zinatengeneza mfumo madhubuti utakao hakikisha mradi huo unakuwa endelevu pamoja na kuwahamasisha vijana wengi ili waweze kunufaika na mafunzo hayo,” alisisitiza Mhagama.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Chemba, Mhe. Simon Odunga aliahidi Mhe. Waziri kusimamia ipasavyo mradi huo ikiwemo kuwawezesha vijana na kuwahamasisha vijana wengine kushiriki kwa wingi kwenye teknolojia hiyo ya Kilimo cha Kitalu nyumba.
“Tutaunga mkono jitihada za Serikali katika kuwawezesha vijana, tunaahidi kutunza mradi huu ili kusaidia wananchi wa chemba kuweza kunufaika nao,” alisema Odunga
Naye mmoja wa vijana walionufaika na mafunzo hayo Bw. Juma Ramadhani alisema kuwa mafunzo hayo yamekuwa chachu kwao na yatawasaidia kuondokana na umaskini kwa kuwa wameweza kujifunza njia bora za kilimo.
“Tunamshukuru Mhe. Rais, Dkt. John Magufuli kwa kutuletea mradi huu inaonesha namna Rais wetu anavyotupigania vijana, tunahaidi kutumia ujuzi tuliopata kuwaelimisha vijana wenzetu ili na wao waweze kunufaika pia,” alisema Ramadhani
Katika ziara hiyo Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama aliweza kutembelea na kukagua maendeleo ya mafunzo kwa vijana kupitia Teknolojia ya kilimo cha Kitalu Nyumba (Green House) katika Wilaya ya Chemba na Kondoa.
MWISHO


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.