*Ni utekelezaji wa agizo la Rais Magufuli
la Januari 2019
*Maeneo yote kutolewa kwa wananchi,
vijiji 920 kubaki ndani ya hifadhi
Serikali imeridhia kufuta mapori tengefu 12 yenye ukubwa wa
ekari 707,659.94 ambayo yamepoteza sifa na imeamua yagawiwe kwa wananchi kwa
ajili ya shughuli za makazi, kilimo na mifugo.
Uamuzi huo umefikiwa
leo (Jumatatu, Septemba 23, 2019) kweye kikao cha Baraza la Mawaziri kilichoongozwa
na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Dkt. John Joseph Pombe Magufuli,
Ikulu jijini Dar es Salaam.
Akitoa taarifa mara
baada ya kikao hicho, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Mawaziri wa kisekta wakiongozwa na
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Bw. William Lukuvi walichambua
na kuandaa taarifa ya mapendekezo ya utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi
nchini iliyowasilishwa katika kikao cha Baraza la Mawaziri cha leo.
“Mawaziri walichambua na kubaini kuwa vijiji vyenye
migogoro ni 975 na siyo 366 kama ilivyotangazwa awali, Baraza limeamua kwamba vijiji
920 vitabaki ndani ya hifadhi, mipaka irejewe upya, vipatiwe vyeti vya ardhi
vya kijiji pamoja na kupangiwa mipango ya matumizi bora ya ardhi,” amesema na
kuongeza kuwa orodha ya vijiji hivyo itatangazwa baadaye.
Waziri Mkuu amesema Serikali
imeridhia Misitu ya Hifadhi saba yenye ukubwa wa ekari 46,715 iliyopoteza sifa
itolewe kwa wananchi kwa ajili ya shughuli za makazi, kilimo na mifugo ili kuwaondolea
kero za uhaba wa ardhi.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeridhia
kumega hifadhi za misitu 14 kwa ajili ya kilimo na mifugo na kufuta mashamba 16
yasiyoendelezwa ili yapangiwe matumizi ya kilimo na mifugo.
“Vijiji
55 vilivyobaki vinaendelea kufanyiwa tathmini ya kina maeneo yaliyobaki ndani ya hifadhi na kuwasilisha mapendekezo yake kwa
ajili ya uamuzi. Uchambuzi na taarifa itatolewa,” amesema na kuongeza kuwa
orodha ya maeneo ya vijiji, mapori ya wanyama, misitu na mashamba yaliyofutwa
itatangwa baadaye.
Pia
amesema Baraza limeamua ardhi ya mita 500 zilizotengwa kama buffer zone (eneo kinga) kwenye maeneo
ya vijiji vinavyopakana na hifadhi za wanyama ziachiwe vijiji husika na
wananchi wasiondolewe kwenye maeneo hayo.
Ameyataja
maamuzi mengine yaliyofikiwa kwenye kikao hicho kuwa ni Ofisi ya Makamu wa Rais
imetakiwa ikamilishe mwongozo utakaobainisha matumizi ya ardhi ndani ya hifadhi
ya mita 60 za mito, vyanzo vya maji, maziwa na
bahari.
Maamuzi
mengine ni kuzitaka Wizara na taasisi zote za Serikali zilinde maeneo yao kwa
kuweka alama za kudumu zinazoonekana; na kwamba wananchi hawaruhusiwi kuvamia
maeneo mapya na hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi ya uvamizi wowote
kuanzia leo.
Januari, mwaka huu, Rais Magufuli
alitoa maagizo kwa Mawaziri nane wa
sekta zinazohusika na matumizi ya ardhi wachambue na kuandaa taarifa ya
mapendekezo ya kutatua migogoro ya matumizi ya ardhi nchini.
Maagizo hayo yalikuwa ni pamoja na: Kutoviondoa
vijiji na vitongoji 366 vilivyomo ndani ya hifadhi; Kubainisha maeneo ya
hifadhi ambayo yamepoteza sifa ili yaweze kugawiwa kwa wananchi kwa shughuli za
ufugaji na kilimo na kuhakiki na kurekebisha mipaka baina ya hifadhi za misitu,
wanyama na makazi.
Mengine ni kumega baadhi ya hifadhi
za Taifa, mapori tengefu na misitu, kuwagawia wafugaji na wakulima; Kufanya
mapitio ya sheria mbalimbali zinazohusiana na matumizi ya ardhi; Kupitia upya
Sheria ya Vyanzo vya Maji inayozungumzia uhifadhi ndani ya mita 60; Kuwasilisha
mapendekezo ya kufutwa mashamba yasiyoendelezwa na kugawa kwa wananchi kwa
ajili ya uzalishaji wa mazao ya kilimo na mifugo na kuendelea kulinda na
kuhifadhi maeneo ya hifadhi za misitu, wanyamapori na vyanzo vya maji.
(mwisho)
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.