WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amemwagiza Naibu Waziri Ofisi ya Rais Tawala za
Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) afuatilie sababu za mikoa ya Tanga
na Njombe kutotekeleza sheria ya kutoza asilimia tano ya ushuru
unaotokana na mazao ya misitu.
Amesema
makampuni yanayonunua nguzo lazima yahakikishe yanazingatia sheria ya
nchi ikiwemo ulipaji wa kodi zilizowekwa kwa mujibu wa sheria na kampuni
zote zilizonunua nguzo bila ya kulipa kodi zifuatiliwe na zilipe kodi
yote waliyoikwepa.
Waziri
Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Septemba 26, 2019) wakati
alipotembelea kiwanda cha kutengeneza nguzo za umeme cha Qwihaya
kilichoko Mafinga wilayani Mufindi akiwa katika siku ya tatu za ziara
yake ya kikazi mkoani Iringa.
“Naibu
Waziri TAMISEMI hakikisha unakwenda mkoani Njombe na uaanze kuzungumza
na mkuu wa mkoa, tunataka kujua kwa nini hawajaanza kutekeleza sheria ya
kutoza asilimia tano ya ushuru unaotokana na mazao ya misitu hali
iliyosababisha wanunuzi kumbilia huko na kuacha kununua mazao hao katika
mkoa wa Iringa.”
“Tunataka
tujue ni nani huyo anayewakataza wasilipe kodi na tuangalie
anamahusiano gani na viongozi wa mkoa huo. Ukaangalie makampuni hayo
yanamahusiano gani na viongozi hao hadi wasilipe kodi na tutajua kama
kampuni hizi ni zao au za ndugu zao.”
Waziri
Mkuu amesema Serikali itahakikisha inawabana wafanyabiashara wote
walionunua nguzo kwenye mikoa hiyo ambao hajalipa asilimia tano ya
ushuru unaotokana na mazao ya misitu ili waweze kulipa kiasi chote
walichokikwepa..
Amesema
Serikali inahitaji kodi kwa ajili ya maendeleo ya wananchi na haoni
sababu ya mikoa hiyo kushindwa kutoza kodi iliyowekwa kwa mujibu wa
sheria. Kitendo cha mikoa hiyo kutotoza kodi hakikubaliki na
wafanyabiashara wote waliochukua nguzo bila ya kulipa kodi hiyo watalipa
kodi yote kuanzia walipioanza kuchukua nguzo.
Waziri
Mkuu amesema Serikali imeweka mikakati ya wafanyabiashara wafanye
biashara zao katika mazingira bora na kwa kuzingatia sheria za nchi na
pia Rais Dkt. John Magufuli amezuia nguzo zote za umeme kuagizwa kutoka
nje ili kuwawezesha wafanuyabiashara wa ndani kuuza nguzo pamoja na
wananchi kupata ajira.
“Hata
tulipokuwa tunanunua nguzo kutoka nje zilikuwa zinatoka hukuhuku na
walichokuwa wakifanya ni kuzichukua huku na kuzipeleka nchi jirani na
kuziweka kwa wiki kisha wanabadilisha vibao na kuzirudisha tena nchini.”
Awali,
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Ally Happi alimweleza Waziri Mkuu kwamba wateja
wa mazao ya misiti wameanza kupungua na kwenda mikoa ya Tanga na Njombe
kwa kuwa katika mikoa hiyo haijaanza kutekeleza sheria ya kutoza
asilimia tano ya ushuru unaotokana na mazao ya misitu, hivyo ameiomba
Serikali iwasaidie.
Kwa upande wake,
Meneja wa Kiwanda cha kutengeneza nguzo za umeme cha Qwihaya, Benedicto
Mahenda alisema kiwanda hicho kilianzishwa 2007 kwa ajili ya uchakataji
wa mbao na 2016 kilianza kuzalisha nguzo za umeme wakiwa na mtambo
wenye kuzalisha nguzo 100 kwa siku. Kiwanda kimeajiri watumishi 350.
Meneja
huyo alisema katika kuitikia wito wa Rais Dkt. Magufuli wa kujenga
uchumi kupitia sekta ya viwanda, walifanya mabadiliko kwa kujenga
kiwanda kikubwa na cha kisasa cha kuzalisha nguzo za umeme chenye uwezo
wa kuzalisha nguzo 1,500 kwa siku.
Alisema
malighafi za kiwanda hicho wanazipata kutoka katika shamba la miti la
Sao Hill lililoko chini ya Wakala wa Misitu Tanzania (TFS) na kwenye
mashamba ya wakulima wadogo. Soko kubwa la bidhaa zao ni TANESCO kupitia
utekelezaji wa miradi ya REA.
Pia,
Meneja huyo alimshukuru Rais Dkt. Magufuli kwa uamuzi wake wa kuzuia
nguzo zisitoke tena nje ya nchi na kutumia nguzo zinazozalishwa na
viwanda vya ndani. “Tunamshukuru sana Mheshimiwa Rais kwa kutuamini na
kututia moyo wawekezaji wa ndani na kutuonyesha soko la kuuza bidhaa
zetu.”
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.