Saturday, September 28, 2019

DANGOTE APEWA WIKI MOJA

NA.MWANDISHI WETU

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Uwekezaji Mhe. Angellah Kairuki ametoa muda wa wiki moja kwa Kiwanda cha kutengeneza saruji cha Dangote kuwasilisha taarifa ya utendaji ambazo kwa zaidi ya miaka miaka mitatu hawajaziwasilisha Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kama sheria na taratibu za nchi zinavyoelekeza.

Waziri Kairuki ambaye aliongozana na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt. Angeline Mabula Katika ziara yake ya kutembelea, kukagua maeneo mbalimbali ya uwekezaji na kuongea na wawekezaji na wafanyabiashara wa Mkoa wa Lindi Septemba 27,2019 ameuelekeza uongozi wa kiwanda hicho kuhakikisha kila baada ya miezi sita wanawasilisha taarifa za kiutendaji TIC.

Waziri Kairuki aliwaeleza masikitiko yake viongozi wa kiwanda hicho kwa kutowasilisha taarifa za utekelezaji wao ikiwemo zinazohusu historia ya mradi, mipango ya upanuzi, kodi wanazolipa, faida pamoja na changamoto wanazokabiliana nazo na ushauri wao.

"Nimesikitishwa sana na suala hili la kutopeleka taarifa zenu TIC ambapo inafahamika suala hilo ni la kisheria na lazima litekelezwe kwa wakati,hivyo kuanzia sasa nimewapa wiki moja mhakikishe taarifa hizo zinawasilishwa haraka,"alisisitiza Waziri Kairuki.

Aidha amewapongeza Dangote kwa uwekezaji huo mkubwa pamoja na kuanza ujenzi wa mradi wa kuzalisha umeme wao wenyewe megawati 25 ambao megawati 5 zitaingia kwenye gridi ya taifa.

Amewataka wawekeze na maeneo mengine siyo kwenye saruji tu na kuagiza TIC kupitia mikataba ya utendaji ya wawekezaji wote mahiri kuona ni wapi wanaweza kuwekeza zaidi.

Wakiwa Mkoani Lindi Waziri Kairuki na Mhe. Mabula walitembelea mgodi wa madini ya uno (graphite) uliopo katika Kijiji cha Matambalale Kusini Wilaya ya Ruangwamkoani Lindi na kuona shughuli za awali za mradi huo ambapo Meneja wa kampuni ya Lindi Jumbo inayochimba madini hayo Bw Paul Shauri amesema mgodi utajengwa kwa muda wa miezi tisa na wanatarajia kuwekeza zaidi ya dola za kimarekani milioni 30.

Akiongea mgodini hapo Dkt.Mabula ameziagiza Halmashairi zote vijiji vyenye maeneo ya uwekezaji kufanya zoezi la kuandaa mpango wa matumizi ya ardhi watenge maeneo ya uwekezaji wayahaulishe yawe mali ya kijiji ili mwekezaji akipatikana watimize masharti mengine tu.

"Hakuna sababu ya mwekezaji kuanza kuhangaika na mambo madogo kama hayo ambayo yanampotezea wakati ni lazima halmashauri zijipange ili kumwekea mwekezaji mazingira mazuri avutiwe kuwekeza"alisema Dkt.Mabula

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Ruangwa Hashim Mgandilwa akiwakaribisha Mawaziri hao amesema Serikali ione kuna sababu ya kuharakisha ujenzi wa miundombinu ikiwemo barabara za wilaya hiyo kwani kuna makampuni mengi makubwa yameonesha nia ya kuwekeza.

Amesema wilaya hiyo pia inakabiliwa na changamoto ya mipaka ya asili na kwamba suala hilo tayari linaendelea kutatuliwa kwa viongozi na watendaji kutoa elimu kwa wananchi.
Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na Sekta ya Uzalishaji Balozi Celestine Mushi akizungumza jambo wakati wa kikao hicho.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika masuala ya Uwekezaji Mhe.Angellah Kairuki akioneshwa namna mfumo wa TEHEMA unavyorahisisha utendaji kiwandani hapo na Mhandisi Brezil Omary  wakati wa ziara yake kiwandani hapo.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulika masuala ya Uwekezaji Mhe.Angellah Kairuki akisisistiza jambo kwa uongozi wa kiwanda cha kutengeneza Saruji cha Dangote kilichopo Mkoa Mtwara alipotembela kukagua na kusikiliza changamoto za wawekezaji mkoani humo.Katikati ni Mtendaji Mkuu wa kiwanda hicho Bw.Jagat Rathee.
Sehemu ya wajumbe waliposhiriki katika kikao cha majumuisho ya ziara ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji) Mhe.Angellah Kairuki wakati wa ziara yake katika kiwanda cha Dangote Mkoani Mtwara.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.