*Aagiza wafikishwe mahakamani kujibu tuhuma za ubadhilifu wa sh bilioni tatu
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewasimamisha kazi watumishi wanane wa
halmashauri ya wilaya ya Ulanga mkoani Morogoro na kuagiza wafikishwe
mahakamani kujibu tuhuma za ubadhilifu wa zaidi ya sh. bilioni tatu za
mapato ya ndani.
Amesema watumishi wa umma wanawajibu
wa kufanya kazi kwa bidii, maarifa na ubunifu. “Nawasihi nyote muache
kufanya kazi kwa mazoea, mbadilike na kuenenda sawa na matakwa na
maelekezo ya Serikali ya Awamu ya Tano na anayejiona hatoshi ajiondoe.”
Waziri
Mkuu amewasimamisha kazi watumishi hao leo (Jumatatu, Septemba 16,
2019) wakati akizungumza na watumishi na madiwani wa Halmashauri ya
wilaya ya Ulanga kwenye mkutano uliofanyika katika ukumbi wa halmashauri
hiyo uliopo mjini Mahenge.
Watumishi
hao kuwa ni pamoja na aliyekuwa Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo Yusuph
Semguruka ambaye kwa sasa amehamishiwa TAMISEMI, Rajabu Siriwa
(mwekahazina), Stanley Nyange, Jonson Mwenyembole, Isack Mwansokope,
Said Majaliwa, Charles Steven na Hezron Lopa.
Pia,
Waziri Mkuu ametumia kikao hicho kumrejesha kazini na kumpandisha kuwa
mkuu wa Idara ya Ukaguzi wa Ndani, Agustine Mwaria ambaye awali alikuwa
akikaimu nafasi na kuibua ubadhilifu huo. Baada ya kuibua ubadhilifu
huyo mtumishi huyo alisimamishwa kazi.
Waziri
Mkuu amewataka watumishi hao wazingatie sheria, kanuni na taratibu za
kiutumishi pamoja na kujiepusha na vitendo vya wizi kwa sababu
wanaoathirika baada ya wao kuchukuliwa hatua za kisheria ni wenza wao na
watoto.
Awali,Mkuu
wa wilaya ya Ulanga, Ngollo Malenya alisema wilaya hiyo inakabiliwa na
changamoto wa ubadhilifu wa fedha za umma hali inayosababisha kuwepo kwa
mpasuko kati ya watumishi na Baraza na Madiwani. Alisema watumishi
wanaotekeleza majukumu yao ipasavyo wanaandamwa.
(mwisho)
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.