Na; Mwandishi Wetu
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amazindua mafunzo ya stadi za kazi yanayotolewa kwa njia ya uanagenzi kwa vijana wapatao 5,875 katika Taasisi ya Don Bosco Net Tanzania.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo iliyofanyika Septemba 14, 2019 katika viwanja vya Don Bosco amesema kuwa Serikali inaendelea na jitihada za kuwawezesha vijana nchini kwa kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuhakikisha nguvu kazi hiyo inapata ujuzi unaotakiwa.
“Napenda kusisitiza kuwa suala la kujenga nguvu kazi yenye ujuzi na maarifa linahusisha juhudi za pamoja kati ya Serikali, Sekta Binafsi na Wadau wengine.”
Alieleza kuwa mafunzo ya ukuzaji ujuzi kwa njia ya Uanagenzi yatawawezesha vijana kutumia asilimia 40 ya muda wao kwa masomo ya nadharia darasani na asilimia 60 ya muda wao kwa masomo ya vitendo katika sehemu ya kazi.
Alifafanua kuwa Serikali inatambua changamoto ya ajira kwa vijana, hivyo ilidhamiria kuanzisha viwanda vidogo, vya kati na vikubwa vyenye uwezo wa kuajiri watu wengi na kuwawezesha kufanya kazi zenye staha.
“Nchi yetu inatakiwa kuhakikisha watu wake wanakuwa na ushindani kwa kuwapatia, maarifa, ujuzi na uwezo unaofaa katika soko la ajira la dunia ya karne ya 21.”
Aidha, alitoa wito kwa vijana hao kuhakikisha wanafanya vizuri katika mafunzo hayo yanatolewa kwa muda wa miezi sita katika fani mbalimbali maana watakuwa na fursa ya kuweza kujiajiri ama kuanzisha shughuli ambazo zitawaingizia kipato.
Sambamba na uzinduzi huo, Waziri Mkuu amelipongeza Shirika la Kazi Duniani (ILO) kwa kuadhimisha miaka 100 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1919 ambapo kwa bara la afrika linaadhimisha miaka 60.
Kwa Upande wake Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe.Jenista Mhagama alieleza kuwa katika mwaka huu wa fedha serikali imejipanga kuwafikia vijana 46,950 ambapo hadi sasa tayari vijana 36,726 wamefaidika na mafunzo hayo katika fani mbalimbali.
“Tumejipanga kuhakikisha tunawafikia vijana wengi nchini katika fani mbalimbali ikiwemo vijana 20,000 watakaopewa mafunzo ya uanagenzi na kati yao vijana 7,000 ni katika fani za ufundi na vijana 13,000 ni katika fani za kuongeza thamani ya mazao hususan ya kilimo ili kuendelea kuleta tija kwa makundi hayo,”
Aliongezea kuwa wamelenga kuwafikia vijana 10,000 katika mafunzo ya urasimishaji ujuzi, vijana 2,500 kupewa mafunzo ya vitendo mahali pa kazi (internship) na vijana 13,000 watapewa mafunzo ya kilimo cha kisasa.
Naye Makamu Mkuu wa Shirika la Don Bosco Net Kanda ya Afrika Mashariki, Padre. Augustine Sellam alisema kuwa mafunzo hayo yanayoratibiwa na Ofisi ya Waziri Mkuu ikishirikiana na Don Bosco yanalenga kuwapa vijana stadi zitakazowawezesha kujiajiri ama kuajiriwa ili kupunguza pengo la ujuzi.
Pia, Mkurugenzi wa Shirika la Kazi Duniani Kanda ya Afrika Mashariki, Dkt. Willington Chibebe alieleza kuwa Shirika hilo litaendelea kushirikiana na Serikali pamoja na wadau katika kuendeleza mwongozo wa kitaifa wa programu za uanagenzi ili kuongeza ujuzi zaidi kwa kizazi cha sasa.
MWISHO
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.