Wednesday, October 30, 2019
WAZIRI MKUU AREJEA NCHINI
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa, leo Oktoba 29, 2019 amerejea nchini akitoka Baku
nchini, Azerbijan ambako alimwakilisha Rais Dkt. John Pombe Magufuli
katika mkutano wa 18 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Nchi
zisizofungamana na upande wowote.
Baada
ya kuwasili katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere,
Waziri Mkuu amepokelewa na Naibu Spika wa Bunge Dkt. Tulia Ackson
Mwansasu pamoja na viongozi wengine wa Mkoa wa Dar es salaam.
Awali,
Mheshimiwa Majaliwa alimwakilisha Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika
Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Mataifa ya Afrika na Urusi
uliofanyika katika mji wa Sochi nchini Urusi.
Monday, October 28, 2019
KAMATI YA BUNGE YAIPONGEZA OFISI YA WAZIRI MKUU KWA MKAKATI WA AJIRA NA UWEZESHAJI VIKUNDI VYA VIJANA
Na; Mwandishi Wetu
Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria imeipongeza Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu kwa mikakati iliyoweka katika kuwajengea uwezo vijana kujiajiri na uwezeshwaji kiuchumi kwa vijana kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Vijana “Youth Development Fund” na Mikopo kupitia mapato ya ndani ya halmashauri.
Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya vijana katika Mkoa wa Morogoro, Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria Mhe. Najma Giga ameipongeza Serikali kwa mikakati iliyokuja nayo katika kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira kwa vijana kwa kuwajengea mazingira wezeshi na yanayowahamasisha kuanzisha miradi mbalimbali ya kiuchumi.
“Matokeo ya utekelezaji wa mikakati hiyo tumeona kwa kiasi kikubwa imewawezesha vijana kutambua taratibu rasmi za kupata mikopo yenye riba nafuu na ambayo imewasaidia kuazisha miradi ya kiuchumi,” alisema Mheshimiwa Giga.
Aliongeza kuwa Serikali iendelee kutenga bajeti zaidi ya uwezeshwaji wa vikundi vya vijana kwa kuwa vina tija na vinapunguza tatizo la ajira kwa vijana kwa kiasi kikubwa.
Sambamba na hayo Kamati hiyo iliitaka Ofisi ya Waziri Mkuu kuendelea kutoa maelekezo katika halmashauri zote kuelimisha vijana zaidi ili waweze kutambua taratibu za kupata mikopo kupitia mfuko wa maendeleo ya vijana na asilimia 10 ya mikopo ambayo utolewa kwa Vijana 4%, Wanawake 4% na Wenye Ulemavu 2% kupitia mapato ya ndani ya halmashauri.
Akitoa maelezo ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde ameihakikishia Kamati ya Bunge kwamba Serikali itaendelea kuviwezesha kiuchumi vikundi vya vijana katika mkakati wa kuhamasisha vijana kujiajiri lakini pia kuwajengea uwezo wa kiuchumi vijana ili nao pia washiriki kikamilifu katika mnyororo mzima wa uchumi wa viwanda ambapo matarajio ni kwamba ifikapo mwaka 2025 zaidi ya asilimia 40 ya nguvukazi iwe imeajiriwa kwenye sekta ya viwanda.
“Serikali iliazisha mfuko wa maendeleo ya vijana na programu mbalimbali ili kuwawezesha wananchi hususan vijana kuweza kupata mahitaji ya mitaji ya kuanzisha shughuli za kiuchumi zitakazo waingizia kipato,” alisema Mavunde
Akitolea mfano mafunzo ya kilimo cha kisasa kwa vijana kutumia teknolojia ya kitalu nyumba ni mkakati mzuri ambao Serikali imekuja nao katika kutatua tatizo la ajira kwa vijana kupitia sekta ya kilimo.
Aidha, Naibu Waziri Mavunde aliwahamasisha vijana kuandaa maandiko ambayo yataelezea shughuli zenye tija wanazotaka kuzifanya katika kujileta maendeleo ili waweze kupata mikopo kupitia Mfuko wa Maendeleo ya vijana na Mikopo kupitia mapato ya ndani ya halmashauri itakayowasaidia kuendesha shughuli zao.
Kwa nyakati tofauti vijana wa Mkoa wa Morogoro wameishukuru Serikali kwa uwezeshaji kupitia Mfuko wa maendeleo ya vijana na kuomba kuwezeshwa zaidi ili kukidhi matarajio yao ya uanzishwaji wa viwanda katika kuunga mkono jitihada za Serikali ya Tano katika uchumi wa viwanda.
Saturday, October 26, 2019
WAZIRI MKUU AMWAKILISHA RAIS DKT. MAGUFULI KATIKA MKUTANO WA 18 WA NAM
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa leo Oktoba 26, 2019 anatarajiwa kumwakilisha Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika Mkutano wa 18 wa Wakuu wa nchi na Serikali wa nchi zisizofungamana na upande wowote (NAM) kutoka Afrika na kwingineko duniani utakaofanyika Baku, Azerbaijan.
Mkutano huo unalenga kujadili namna ya kutatua changamoto za kisiasa, kiuchumi na kijamii zinazokabili nchi wanachama wa NAM katika nyakati za sasa, pamoja na na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maslahi ya nchi wanachama wa umoja huo.
Waziri Mkuu aliwasili nchini Azerbaijan jana (Ijumaa, Oktoba 25, 2019) na alipokelewa na Naibu Waziri Mkuu wa Azerbaijan, Bw. Ali Ahmadov pamoja na viongozi wengeine wa Serikali hiyo. Mapokezi hayo yalifanyika katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Heydar Aliyev.
Ajenda za mkutano huo ni kupokea ripoti za mkutano wa maandalizi wa Mawaziri, kupokea ripoti ya mkutano wa maandalizi wa Maafisa Waandamizi, uchaguzi wa nchi zitakazokuwa wajumbe katika ofisi ya uratibu wa shughuli za NAM, New York kwa kipindi cha mwaka 2019-2022.
Mbali na ajenda hizo, pia ajenda nyingine za mkutano huo ni kupokea ripoti za shughuli za umoja huo zilizotekelezwa chini ya Mwenyekiti wa NAM, Venezuela, mjadala mkuu, pamoja na kupitisha maandiko yatokanayo na mkutano.
Mheshimiwa Majaliwa ameambatana na Naibu Waziri Mambo ya Nje na Ushirkiano wa Afrika ya Mashariki, Dkt. Damasi Ndumbaro na Balozi wa Tanzania Nchini Urusi ambale pia ni Balozi wa Azerbaijan, Meja Jenerali Mstaafu, Simon Mumwi.
Awali, Waziri Mkuu alikuwa Sochi nchini Urusi ambako pia alimwakilisha Rais Dkt. John Magufuli katika Mkutano wa Uchumi kati ya Urusi na Afrika (Russia - Africa Economic Forum) na baadae Mkutano wa wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa Mataifa ya Afrika uliofunguliwa na Rais wa Urusi Vladimir Putin.
Friday, October 25, 2019
BIASHARA KATI YA TANZANIA NA URUSI IRATIBIWE-MAJALIWA
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwwa ameutaka ubalozi wa Tanzania nchini Urusi uratibu mipango ya wafanyabiashara wa Urusi wanaokusudia kuja nchini kuwekeza kwa kuwaunganisha na Taasisi na Wizara husika ili waweze kuwekeza mitaji yao kwa kuzingatia maslahi ya Taifa.
Ametoa agizo hilo jana (Alhamisi, Oktoba 24, 2019) baada ya kugundua uwepo wa wafanyabiashara wengi wa Urusi wanakusudia kuja Tanzania kwa ajili ya kuangalia maeneo ya uwekezaji pamoja na kutafuta wafanyabiashara wa Kitanzania watakaoungana nao katika uwekezaji wanaokusudia kuufanya.
“Tayari miadi imekwishawekwa ya kuwakaribiasha wawekezaji wa Urusi kuja Tanzania kwa ushawishi wa kwangu mwenyewe pamoja na ushawishi wa wafanyabiashara wa Tanzania, hivyo nisingependa wafanyabiashara hao wasumbuliwe au kukatishwa tamaa katika kutimiza nia yao hiyo.” Waziri Mkuu alisisitiza.
Alisema Mkutano baina ya Wakuu wa nchi na Serikali kutoka Mataifa ya Afrika na Urusi uliomalizika jana Oktoba 24, 2019 ulilenga kujenga uhusiano mzuri zaidi katika nyanja mbalimbali hususani za kiuchumi.
Akizungumza baada kumalizika mkutano huo kwenye ukumbi wa Olympic Park wa Sochi nchini Urusi, Waziri Mkuu alisema Urusi imeutumia mkutano huo kueleza bayana maeneo ambayo wako tayari kushirikiana na Afrika katika kuwekeza kwa faida ya pande zote mbili.
Waziri Mkuu aliyataja maeneo hayo kuwa ni pamoja na uuzaji wa zana za kilimo kama vile matrekta, sekta ya mafuta na gesi pamoja na madini, Ujenzi wa miundombinu hasa reli, masuala ya elimu hasa utoaji wa nafasi za mafunzo nchini humo.
Alisema kwa upande wake Tanzania imejinadi vizuri ikIngozwa na yeye mwenyewe kwani alifanya mazungumzo na viongozi wa makampuni zaidi ya manane ya Urusi ili kuyashawishi yawekeze nchini na yote yalikubali kufika Tanzania mapema iwezekanavyo.
“Viongozi wa makapuni yote niliyopata nafasi ya kuzungumza nao wamesema wako tayari kuja nchini ili waweze kufanya mazungumzo na Serikali pamoja na wafanyabiashara wazalendo ambao wako tayari kuungana na wafanyabiashara hao katika kuwekeza nchini Tanzania.”
Waziri Mkuu alisema viongozi hao walimueleza maeneo ambayo wao wanaamini kuwa wanafanya vizuri na wangependa kupata kibali cha kuwekeza Tanzania baada ya mazungumzo yao na Serikali. Pia walieleza ni kwa namna gani Taifa litanufaika na uwekezaji wao.
Alisema, tayari wafanyabiashara binafsi 18 wa Tanzania walijitokeza kushiriki katika Mkutano huo na walifanya kazi kubwa na nzuri ya kuwahabarisha wenzao wa Urusi kuhusu mazingira mazuri ya kuwekeza yaliyopo nchini hasa baada ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais, Dkt. John Pombe Magufuli kuondoa kero, kanuni na taratibu ziliokuwa zikiyafanya mazingira ya uwekezaji kuwa magumu.
Awali, akizungumza kwenye Mkutano baina ya Wakuu wa nchi na Serikali kutoka mataifa ya Afrika na Urusi, Waziri Mkuu alisema kwa sasa Tanzania ni nchi sahihi kwa uwekezaji kwa wanaotaka kuwekeza barani Afrika kwani imedhamiria kukuza uchumi wake na kufikia wa kati ifikapo 2025 kwa kupitia sekta ya viwanda. Pia ni nchi yenye amani na utulivu.
“Nchi yetu imejaliwa kuwa na maliasili nyingi ambazo vilele ni malighafi kwa viwanda kama vile mazao ya kilimo, misitu, bahari, maziwa, madini na mbuga za wanyama ambazo ni kivutio cha watalii,” alifafanua Waziri Mkuu.
Leo Oktoba 25, 2019 Mheshimiwa Majaliwa ataondoka nchini Urusi kwenda nchi ya Azerbaijan ambako pia atamwakilisha Rais Dkt. John Pombe Magufuli katika Mkutano wa Nchi zisizofungamana na upande wowote. Mkutano huo ni wa siku mbili.
(mwisho)
Thursday, October 24, 2019
OFISI YA WAZIRI MKUU YATEMBELEA MIRADI YA KUBORESHA MAZINGIRA YA BIASHARA –LIC WILAYANI KAKONKO
Muonekano wa Jengo la Kituo cha biashara lililojendwa kwa ufadhili wa Mradi wa Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara Local Investment Climate (LIC)) unaoratibiwa na Baraza la Taifa la Biashara lililopo Wilaya ya Kakonko mkoa wa Kigoma.
|
Mkaguzi wa ndani kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. Omari Saidi akikagua na kuchukua taarifa za mashine ya kukoboa mpunga iliyojengwa kwa ufadhili wa Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara Local Investment Climate (LIC)) wakati wa ziara ya kitengo hicho kuona utekelezaji wake wilayani Kakonko Mkoa wa Kigoma.
|
MAJALIWA AKIWA KATIKA PICHA YA PAMOJA YA WAKUU WA NCHI NA SERIKALI WA MATAIFA YA AFRIKA NA RAIS WA URUSI, VLADIMIR PUTIN
Wednesday, October 23, 2019
MAJALIWA AMWAKILISHA RAIS DKT. MAGUFULI MKUTANO WA UCHUMI KATI YA URUSI NA AFRIKA
Rais wa Urusi, Vladimir Putin akihutubia katika Mkutano wa uchumi kati ya Afrika na Urusi (Russia -Africa Economic Forum) kwenye Kituo cha Olympic Park, Sochi nchini Urusi, Oktoba 23, 2019. |
Rais wa Urusi, Vladimir Putin akihutubia katika Mkutano wa uchumi kati ya Afrika na Urusi (Russia -Africa Economic Forum) kwenye Kituo cha Olympic Park, Sochi nchini Urusi, Oktoba 23, 2019. |
MAJALIWA AKISALIMIANA NA RAIS WA URUSI VLADIMIR PUTIN
AFRIKA NI MUHIMU KWA MAENDELEO YA UCHUMI WA DUNIA-PUTIN
RAIS wa Urusi, Vladimir Putin amefungua Kongamano la Biashara baina ya Urusi na Afrika (Russia Business Forum) ambapo amesema Bara la Afrika ni muhimu katika maendeleo ya uchumi wa dunia na ni kivutio kikubwa kwa wafanyabiashara wa Urusi.
Ameyasema hayo leo (Jumatano, Oktoba 23, 2019) wakati akihutubia mkutano huo uliofanyika kwenye ukumbi wa Kituo cha Olympic Park katika mji wa Sochi nchini Urusi. Rais Putin amesema takwimu zilizotolewa na watalaamu wa masuala ya uchumi zinaonyesha kwamba pato la Afrika (GDP) litafikia dola trilioni 29 ifikapo 2050.
Amesema biashara kati ya Urusi na Afrika imeongezeka mara dufu katika kipindi cha miaka mitano iliyopita na kufikia dola za Marekani bilioni 20 na kwamba nchi yake inaunga mkono wazo la kuanzishwa eneo huru la biashara katika bara la Afrika ukiwa ni mkakati wa Umoja wa Afrika (AU) na kwamba itatoa ushirikiano ili kufanikisha wazo hilo.
Kadhalika, Rais Putin ameongeza kuwa nchi yake inatekeleza kwa vitendo mpango kuzifutia madeni nchi za Afrika na hadi sasa imeshafuta madeni ya zaidi ya dola za Marekani bilioni 20.
Amesema utoaji wa mafunzo ya taaluma mbalimbali umekuwa ni utamaduni wa ushirikiano kati ya Urusi na Afrika. “Hadi katikati ya miaka ya 80 nchi yake imejenga taasisi zipatazo 100 za mafunzo mbalimbali Barani Afrika na watu 500,000 wampata mafunzo katika taasisi hizo.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ameshiriki katika mkutano huo akimwakilisha Rais John Pombe Magufuli. Pamoja naye idadi kubwa ya Wakuu wa Nchi na Serikali katika Bara la Afrika wamehudhuria mkutano huo.
Miongozi mwa viongozi hao ni Rais Yoweli Museveni wa Uganda, Rais Paul Kagame wa Rwanda, Rais wa Misri na Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, Abdel Fattah al Sissi, Rais wa Afrika ya Kusini, Cyril Ramaphosa, Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, Rais wa Msumbiji Filipe Nyusi na viongozi wengine kutoka Bara la Afrika.
Kesho (Alhamisi, Oktobba 24, 2019) Waziri Mkuu anatarajia kushiriki katika mkutano baina ya Urusi na Wakuu wa nchi na Serikali wa Bara la Afrika.
Tuesday, October 22, 2019
NAIBU WAZIRI MAVUNDE AZITAKA HALMASHAURI KUWAWEZESHA VIJANA KIUCHUMI KUPITIA ZABUNI ZA HALMASHAUR
Na; Mwandishi Wetu
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde amezitaka Halmashauri za Wilaya, Manispaa na Majiji nchini kuwawezesha Vijana kiuchumi kwa kutumia Vikundi na Kampuni za Vijana katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimaendeleo kwa kuzipa zabuni kampuni na vikundi hivyo kupitia utaratibu wa “force account” hasa katika utengenezaji wa madawati na ujenzi wa madarasa, matundu ya vyoo, zahanati na vituo vya Afya.
Naibu Waziri Mavunde kayasema hayo Wilayani Musoma wakati alipotembelea Chuo cha Ufundi cha Mt. Anthony ambapo jumla ya Vijana 240 wanasoma hapo fani mbalimbali kwa ufadhili wa Serikali kupitia Programu ya Ukuzaji Ujuzi Nchini iliyopo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu ambapo mwaka huu wa fedha 2019/2020 inatrajiwa kuwajengea uwezo Vijana 46,000 katika fani mbalimbali.
"Serikali inayo nia ya dhati ya kuhakikisha kwamba tunaijengea Ujuzi stahiki nguvukazi ya Taifa hili ili vijana wengi zaidi waweze kushiriki kikamilifu katika uchumi wa viwanda na kuwawezesha kujikwamua kiuchumi kupitia shughuli za uzalishaji mali.Mamlaka za Serikali za Mitaa ziwe kichocheo katika kuwawezesha Vijana kiuchumi kwa kutoa zabuni kwa vikundi na makampuni ya Vijana nchini kote hasa zile zinapitia katika mfumo wa manunuzi wa force account," alisema Mavunde
Akitoa salamu za Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Vicent Naano amewahakikishia Vijana hao kupata mikopo ya asilimia 4 na asilimia 2 kwa wenye ulemavu itokanayo na mapato ya ndani ya Halmashauri na kuwataka kuunda vikundi kutokana na fani zao za Ufundi.
Akizungumza kwa niaba ya Vijana wenzake wanafuika ya Programu ya kukuza Ujuzi, Bw. Baraka Emmanuel ameishukuru Serikali kwa kuwajali Vijana na kuwawezesha kupata Ujuzi kupitia mafunzo wanayoyapata hapo Chuoni ambayo pia yatawafanya waweze kujiajiri na kuajiri Vijana wengine.
Baadhi ya vijana wanaojifunza ufundi wa magari wakijishughulisha ikiwa ni sehemu ya mafunzo yao.
|
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Kazi, Vijana na Ajira Mhe. Anthony Mavunde akizungumza jambo na vijana wanaojifunza fani ya Ushonaji alipotembelea kujionea mafunzo ya vijana hao.
|
Mkuu wa Wilaya ya Musoma Dkt. Vicent Naano akieleza jambo wakati wa ziara hiyo.
|
URUSI: WAZIRI MKUU AKIENDELEA NA MAJUKUMU YAKE NCHINI URUSI
Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa akizungumza na Mwakilishi wa Kampuni ya Sinara Transport Machinary kwenye hoteli ya Marriot, Sochi nchini Urusi, Oktoba 22, 2019. |
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Mwakilishi wa Kampuni ya Sinara Transport Machinary kwenye hoteli ya Marriot, Sochi nchini Urusi, Oktoba 22, 2019. |
USAFIRI WA RELI KUIMARISHWA KATIKA MAJIJI-MAJALIWA
WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Mkuu
wa Kampuni ya Russian Railways, Bw. Alexander Misharin na kumweleza
kuwa Tanzania inahitaji sana kuimarisha usafiri wa ndani wa reli hasa
katika Majiji ya Dar es salaam, Mwanza, Dodoma, Arusha, Mbeya na Tanga.
Amesema
kampuni hiyo yenye uwezo mkubwa wa kujenga reli mpya, kukarabati reli,
kutengeneza injini za treni na mabehewa pamoja na ukarabati wake
inahitajika sana nchini ili kufanikisha mpango wa Serikali wa kuimarisha
reli za zamani za TAZARA, Reli ya Kati na kufugua reli ya Kaskazini
inayounganisha mikoa ya Dar es salaam, Tanga, Kilimanjaro na Arusha.
Waziri
Mkuu alizungumza na Mkurugenzi huo jana (Oktoba 22, 2019) kwenye hoteli
ya Marriot iliyopo Sochi nchini Urusi, ambapo alitumia fursa hiyo
kuikaribisha kampuni ya Russian Railways kuwekeza nchini hususani katika
sekta ya ujenzi, ufundi na mafunzo ikishirikiana na makampuni ya
Watanzania.
Waziri
Mkuu yuko nchini Urusi kuhudhuria mkutano baina ya Wakuu wa Nchi na
Serikali kutoka Mataifa ya Afrika na Urusi (Russia-Africa Summit),
unaotarajiwa kuanza leo Oktoba 23 hadi 24, 2019 katika jiji la Sochi. Waziri Mkuu anahudhuria mkutano huo kwa niaba ya Rais, Dk. John Pombe Magufuli.
“Katika
kipindi hiki ambacho Tanzania inajenga reli ya kiwango cha kimataifa
ya SGR pamoja na kufufua reli ya Kaskazini, inaikaribisha Kampuni ya
Russian Railways kwa mikono miwili ije ifanye mazungumzo rasmi na Wizara
husika. Pia Serikali inao mkakati wa kujenga reli mpya katika ukanda
wa Kusini kutoka Mtwara hadi Ruvuma ili kuiunganisha bandari ya Mtwara
na mikoa ya Kusini pamoja na nchi jirani za Malawi na Zambia.”
Alisema
Tanzania kwa sasa inahitaji sana kuimarisha usafiri wa ndani wa reli
hasa katika majiji ya Dar es salaam, Mwanza, Dodoma, Arusha, Mbeya na
Tanga hivyo endapo mazungumzo kati ya Wizara husika na kampuni hiyo
yataonekana kuwa na tija na yana maslahi kwa Watanzania, kampuniyo
itapewa fursa ya kuwekeza nchini.
Kadhalika,
Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwakumbusha wafanyabiashara wa
Tanzania, wito wa Rais Dkt. John Pombe Magufuli wa kuwataka watumie
fursa lukuki zilizopo nchini kuanzisha makapuni ya pamoja na makampuni
ya nje ili kuunganisha nguvu kwa kuendesha kwa pamoja makampuni
yatakayoanzishwa.
Alisema
utaratibu wa makampuni ya Tanzania kuanzisha makampuni ya pamoja na
makampuni ya nje utawapa Watanzania fursa ya kujipatia kipato pia
wataweza kulinda maslahi ya Taifa.
Kwa upande wake,
Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Russia Railways, Bw. Misharin
alimuhakikishia Waziri Mkuu kuwa kampuni yake iko tayari kushirikiana na
wafanyabiashara wa Kitanzania katika kuanzisha makapuni ya pamoja ili
kuipatia Tanzania tekinolojia ya masuala ya reli na kubadilisha ujuzi.
Awali,
Waziri Mkuu alizungumza na Wakurugenzi wa Kampuni ya kutengeneza
matrekta ya BTP, Bw. Alexsey Punkov na Bw. Ignat Dydyshkoa ambaye
alisema kuwa kampuni yake inakusudia kuwekeza nchini Tanzania katika
sekta ya kilimo kwa kuleta nchini mashine mbalimbali kama vile matrekta
na mitambo ya ujenzi wa barabara.
Viongozi wote wa
makampuni ya Urusi waliozungumza na Waziri Mkuu waliahidi kuja
Tanzania mwaka huu ili kujionea fursa mbalimbali za uwekezaji na kufanya
mazungumzo yenye lengo la kushirikiana na wafanyabiashara wa Kitanzania
katika uwekezaji wao wanaokusudia kuufanya nchini.
Mheshimiwa
Majaliwa pia alizungumza na Mkurugenzi Mkuu wa Kampuni ya Mafuta na
Gesi ya Zarubezhnefe, Bw. Sergey Kundryashov ambaye pia alionyesha nia
ya kutaka kuwekeza nchini Tanzania.
Katika
safari hiyo Waziri Mkuu ameambatana na Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki, Dkt. Damas Ndumbaro, Balozi wa
Tanzania nchini Urusi, Meja Jenerali Mstaafu, Simon Mumwi na Mkurugenzi
Mkuu wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), James
Matarajio.