Na. OWM,
Dodoma.
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wadau wa
lishe nchini kuungana na kuongeza juhudi
katika kupambana na aina zote za utapiamlo ili kufikia viwango vinavyokubalika
kimataifa, hivyo amemtaka kila mdau wa lishe kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha
tatizo la utapiamlo linapungua katika jamii ya watanzania, kwakuwa utapiamlo ni
miongoni mwa vikwazo vya kutimiza dhamira ya Serikali ya awamu ya tano ya
kujenga uchumi wa viwanda na kuufikia
uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Amesema ili Matokeo
mazuri ya hali ya lishe yapatikane nchini lazima kazi za kuboresha hali ya lishe zifanyike kwa ushirikiano kupitia sekta na miradi inayotekelezwa ya lishe na amebainisha kuwa bila ya kuwa na lishe bora na afya njema yenye kusaidia kuongeza uwezo wa Uelewa na
ubunifu katika kuhimili ushindani wa kiuchumi, nchi haitafika kwa wakati kwenye
uchumi wa kati na wa viwanda uliokusudiwa.
Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi,
Oktoba 3, 2019) wakati akifungua mkutano wa mwaka wa Wadau wa Lishe uliofanyika
kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma. Amesema ni muhimu kila mdau wa lishe kuendelea
kushirikiana katika utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Lishe wa Miaka Mitano,
kwa kutoa elimu ya lishe kwa wananchi wote.
“Pamoja na kuwa kuna
sababu nyingi za msingi zinazochangia hali duni ya lishe, ni ukweli usiofichika
kuwa, ili kupata matokeo bora ya hali ya lishe nchini, ni lazima tuhakikishe
tunafanya kazi kwa pamoja kupambana na sababu hizo. Pamoja na tafiti
kuonesha kwamba tumepunguza viwango vya udumavu na upungufu wa damu bado
viwango vyake havikubaliki kimataifa. Vilevile, tuna viwango vya utapiamlo
ambavyo vimezidi kuongezeka na havikubaliki kimataifa ikiwemo uzito uliozidi
kwa wanawake wenye umri wa kuzaa.”
Amesema hali hiyo ni hatari kwa nchi ambayo
inayokabiliwa na aina nyingine za utapiamlo unaosababishwa na lishe duni kama
udumavu, utapiamlo mkali na wa kadiri ambapo athari zake ni kubwa katika ukuaji
wa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.
“Hii ni ishara tosha kwamba tunatakiwa
kuongeza juhudi za pamoja katika
kupambana na aina zote za utapiamlo ili kufikia viwango vinavyokubalika
Kimataifa.”
Amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau
itaendelea kutoa kipaumbele kwa maeneo ambayo yameathirika zaidi na ambayo
yanatekeleza miradi inayolenga kupunguza udumavu kwa watoto, matatizo ya
upungufu wa vitamin na madini.
Kipaumbele kitatolewa katika kuimarisha
matibabu ya utapiamlo mkali na wa kadiri, kupunguza tatizo la uzito uliokithiri
na viriba tumbo na tatizo la upungufu wa damu kwa wanawake na watoto ili kuhakikisha
kuwa miradi hiyo inaleta matokeo chanya katika maeneo hayo.
Amesema kuwa pamoja na ushirikiano mzuri wa wadau wa lishe ukiwepo lakini ushirikiano huo hautakuwa na tija mipango yoyote wanayojiwekea haiwezi kuleta
matokeo chanya bila kuitengenezea mikakati thabiti ya utekelezaji ikiwa ni
pamoja na kutenga rasilimali za kutosha, ambapo wataalamu hao waibue mikakati
itakayoweza kutumika katika kupunguza tatizo la utapiamlo.
Pia, Waziri Mkuu amewataka waajiri wote
waandae fursa na kuwaalika mahala pa kazi maafisa lishe ili kuongeza ufahamu wa
watumishi kuhusu lishe bora. Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya
Rais-TAMISEMI zimetakiwa ziweke mipango ya kuhakikisha maafisa lishe wanaalikwa
kutoa elimu sambamba na ufundishaji shuleni.
Kwa upande wake,Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri
Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Jenista Mhagama amesema
bila kuwa na nguvu kazi yenye lishe na afya bora Taifa haliwezi kufanikiwa
kwenye masuala ya elimu, kilimo, viwanda hivyo hali hiyo inaweza kukwamisha
jitihada za Serikali ya awamu ya tano ya kujenga uchumi wa viwanda.
“Kwa hali iliyopo sasa ni wazi kuwa bado tuna
kazi kubwa ya kufanya ili kuondokana na utapiamlo nchini. Juhudi za pamoja
zinahitajika ili kuweza kufikia malengo tuliyojiwekea katika Mpango Jumuishi wa
Taifa wa Lishe (2016/17 – 2020/21), ambayo ni pamoja na kupunguza udumavu kwa
watoto wenye umri chini ya miaka mitano kufikia asilimia 28 na uzito uliozidi
kufikia asilimia 30.”
Amesema Serikali inatambua kuwa lishe ni suala
mtambuka linalotegemea jitihada za sekta mbalimbali, ambapo tayari Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa miaka mitano
kuanzia mwaka 2015/16 hadi 2020/21 umejumuisha masuala ya lishe ili kutoa
muongozo katika utekelezaji wa afua mbalimbali za masuala ya lishe.
Naye, Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda
amesema katika jitihada za kupambana na umasikini ni vema wadau wote wa lishe
nchini waungane katika kutoa elimu ya
lishe bora kwa wananchi wote, ambapo amemshauri Waziri Mkuu aibebe agenda ya
lishe, ambapo Waziri Mkuu amekubali.
Waziri Mkuu huyo Mstaafu ameongeza kuwa, mila
potofu nazo zimechangia suala la utapiamlo kwa sababu katika familia nyingi
nchini husuani katika kuchagua aina za vyakula maalum wanavyopaswa kula
wanawake, wanaume pamoja na watoto hali inayopelekea familia kuwa na tatizo la
utapiamlo.
Awali, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya
Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndungulile amesema udumavu
umepungua kutoka asilimia 34.4 mwaka 2015 na kufikia asilimia 31.5 mwaka huu.
Dkt. Ndungulile alisema licha kupungua kwa
udumavu, changamoto iliyopo kwa sasa ni suala la unyonyeshaji kwa watoto walio
na umri wa chini ya miezi sita, wanaonyenyeshwa ni asilimia 58 tu, huku
asilimia 30 ya Watoto wenye umri wa zaidi ya miezi sita hawalishwi
vizuri.”Theruthi moja ya wanawake nchini wana viribatumbo na utapiamlo wa lishe
iliyopitiliza. Ni muhimu kuwa na uwiano katika afua tunazopanga
kwa kuangalia aina zote za utapiamlo na makundi yote yaani wanawake, watoto
wadogo na wachanga, wazee, vijana na wanaume“
Mkutano
huo wa kutathmini utekelezaji wa Mpango
Shirikishi wa Taifa kuhusu Masuala ya Lishe umehudhuliwa na washiriki 300, wakiwemo wadau wa lishe wa
ndani na nje ya nchi, viongozi wa juu wa
Wizara zinazojihusisha na masuala ya lishe, Waheshimiwa Wabunge, Washirika wa
Maendeleo, Taasisi za Elimu ya Juu na Utafiti, Taasisi zisizo za Kiserikali
pamoja na sekta binafsi, ambapo Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na
Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania imeandaa Mkutano huo.
MWISHO.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.