Thursday, October 3, 2019

WAZIRI MKUU AWATAKA WADAU WA LISHE NCHINI KUUNGANA KUTOKOMEZA UTAPIAMLO



Na. OWM, Dodoma.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amewataka wadau wa lishe nchini kuungana na kuongeza juhudi katika kupambana na aina zote za utapiamlo ili kufikia viwango vinavyokubalika kimataifa, hivyo amemtaka kila mdau wa lishe kuchukua hatua za makusudi kuhakikisha tatizo la utapiamlo linapungua katika jamii ya watanzania, kwakuwa  utapiamlo ni miongoni mwa vikwazo vya kutimiza dhamira ya Serikali ya awamu ya tano ya kujenga uchumi wa viwanda na  kuufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.

Amesema ili Matokeo mazuri ya hali ya lishe yapatikane nchini lazima  kazi za kuboresha hali ya lishe zifanyike  kwa ushirikiano kupitia sekta  na miradi inayotekelezwa ya  lishe  na  amebainisha kuwa bila ya kuwa na lishe bora na afya njema  yenye kusaidia kuongeza uwezo wa Uelewa na ubunifu katika kuhimili ushindani wa kiuchumi, nchi haitafika kwa wakati kwenye uchumi wa kati na wa viwanda uliokusudiwa. 

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo (Alhamisi, Oktoba 3, 2019) wakati akifungua mkutano wa mwaka wa Wadau wa Lishe uliofanyika kwenye ukumbi wa Hazina jijini Dodoma. Amesema ni muhimu kila mdau wa lishe  kuendelea kushirikiana katika utekelezaji wa Mpango Jumuishi wa Lishe wa Miaka Mitano, kwa kutoa  elimu ya lishe kwa wananchi wote.
                                         

Pamoja na kuwa kuna sababu nyingi za msingi zinazochangia hali duni ya lishe, ni ukweli usiofichika kuwa, ili kupata matokeo bora ya hali ya lishe nchini, ni lazima tuhakikishe tunafanya kazi kwa pamoja kupambana na sababu hizo. Pamoja na tafiti kuonesha kwamba tumepunguza viwango vya udumavu na upungufu wa damu bado viwango vyake havikubaliki kimataifa. Vilevile, tuna viwango vya utapiamlo ambavyo vimezidi kuongezeka na havikubaliki kimataifa ikiwemo uzito uliozidi kwa wanawake wenye umri wa kuzaa.”

Amesema hali hiyo ni hatari kwa nchi ambayo inayokabiliwa na aina nyingine za utapiamlo unaosababishwa na lishe duni kama udumavu, utapiamlo mkali na wa kadiri ambapo athari zake ni kubwa katika ukuaji wa watoto wenye umri wa chini ya miaka mitano.

“Hii ni ishara tosha kwamba tunatakiwa kuongeza juhudi za pamoja  katika kupambana na aina zote za utapiamlo ili kufikia viwango vinavyokubalika Kimataifa.”

Amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau itaendelea kutoa kipaumbele kwa maeneo ambayo yameathirika zaidi na ambayo yanatekeleza miradi inayolenga kupunguza udumavu kwa watoto, matatizo ya upungufu wa vitamin na madini.

Kipaumbele kitatolewa katika kuimarisha matibabu ya utapiamlo mkali na wa kadiri, kupunguza tatizo la uzito uliokithiri na viriba tumbo na tatizo la upungufu wa damu kwa wanawake na watoto ili kuhakikisha kuwa miradi hiyo inaleta matokeo chanya katika maeneo hayo.

Amesema kuwa pamoja na ushirikiano mzuri  wa wadau wa lishe  ukiwepo lakini  ushirikiano huo hautakuwa na tija  mipango yoyote wanayojiwekea haiwezi kuleta matokeo chanya bila kuitengenezea mikakati thabiti ya utekelezaji ikiwa ni pamoja na kutenga rasilimali za kutosha, ambapo wataalamu hao waibue mikakati itakayoweza kutumika katika kupunguza tatizo la utapiamlo. 

Pia, Waziri Mkuu amewataka waajiri wote waandae fursa na kuwaalika mahala pa kazi maafisa lishe ili kuongeza ufahamu wa watumishi kuhusu lishe bora. Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia na Ofisi ya Rais-TAMISEMI zimetakiwa ziweke mipango ya kuhakikisha maafisa lishe wanaalikwa kutoa elimu sambamba na ufundishaji shuleni.

Kwa upande wake,Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na wenye Ulemavu Jenista Mhagama amesema bila kuwa na nguvu kazi yenye lishe na afya bora Taifa haliwezi kufanikiwa kwenye masuala ya elimu, kilimo, viwanda hivyo hali hiyo inaweza kukwamisha jitihada za Serikali ya awamu ya tano ya kujenga uchumi wa viwanda.


“Kwa hali iliyopo sasa ni wazi kuwa bado tuna kazi kubwa ya kufanya ili kuondokana na utapiamlo nchini. Juhudi za pamoja zinahitajika ili kuweza kufikia malengo tuliyojiwekea katika Mpango Jumuishi wa Taifa wa Lishe (2016/17 – 2020/21), ambayo ni pamoja na kupunguza udumavu kwa watoto wenye umri chini ya miaka mitano kufikia asilimia 28 na uzito uliozidi kufikia asilimia 30.”


Amesema Serikali inatambua kuwa lishe ni suala mtambuka linalotegemea jitihada za sekta mbalimbali, ambapo tayari  Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa miaka mitano kuanzia mwaka 2015/16 hadi 2020/21 umejumuisha masuala ya lishe ili kutoa muongozo katika utekelezaji wa afua mbalimbali za masuala ya lishe. 

Naye, Waziri Mkuu Mstaafu Mizengo Pinda amesema katika jitihada za kupambana na umasikini ni vema wadau wote wa lishe nchini  waungane katika kutoa elimu ya lishe bora kwa wananchi wote, ambapo amemshauri Waziri Mkuu aibebe agenda ya lishe, ambapo Waziri Mkuu amekubali.

Waziri Mkuu huyo Mstaafu ameongeza kuwa, mila potofu nazo zimechangia suala la utapiamlo kwa sababu katika familia nyingi nchini husuani katika kuchagua aina za vyakula maalum wanavyopaswa kula wanawake, wanaume pamoja na watoto hali inayopelekea familia kuwa na tatizo la utapiamlo.

Awali, Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dkt. Faustine Ndungulile amesema udumavu umepungua kutoka asilimia 34.4 mwaka 2015 na kufikia asilimia 31.5 mwaka huu.

Dkt. Ndungulile alisema licha kupungua kwa udumavu, changamoto iliyopo kwa sasa ni suala la unyonyeshaji kwa watoto walio na umri wa chini ya miezi sita, wanaonyenyeshwa ni asilimia 58 tu, huku asilimia 30 ya Watoto wenye umri wa zaidi ya miezi sita hawalishwi vizuri.”Theruthi moja ya wanawake nchini wana viribatumbo na utapiamlo wa lishe iliyopitiliza. Ni muhimu kuwa na uwiano katika afua tunazopanga kwa kuangalia aina zote za utapiamlo na makundi yote yaani wanawake, watoto wadogo na wachanga, wazee, vijana na wanaume

Mkutano huo  wa kutathmini utekelezaji wa Mpango Shirikishi wa Taifa kuhusu Masuala ya Lishe umehudhuliwa na  washiriki 300, wakiwemo wadau wa lishe wa ndani na nje ya nchi,  viongozi wa juu wa Wizara zinazojihusisha na masuala ya lishe, Waheshimiwa Wabunge, Washirika wa Maendeleo, Taasisi za Elimu ya Juu na Utafiti, Taasisi zisizo za Kiserikali pamoja na sekta binafsi, ambapo Ofisi ya Waziri Mkuu kwa kushirikiana na Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania imeandaa Mkutano huo.
MWISHO.


EmoticonEmoticon

Note: Only a member of this blog may post a comment.