Na; Mwandishi Wetu
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama amepongeza vijana kwa kuonesha niya njema ya kuendelea kumuenzi Baba wa Taifa sambamba na kuendeleza mambo mema yote aliyoyafanya enzi za uhai wake.
Ameyasema hayo Oktoba 6, 2019 wakati wa hafla ya kuwaaga vijana 60 waliopanda Mlima Kilimanjaro kwa ajili ya kuadhimisha kumbukizi ya miaka 20 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwl Julius Kambarage Nyerere iliyofanyika Marangu, Mkoani Kilimanjaro.
Waziri Mhagama alisema kuwa, Baba wa Taifa Mwl. Julius K. Nyerere alikuwa kiongozi mzalendo kwa nchi yake na aliyejali utu na usawa, hivyo ni jambo zuri kuona vijana wakiendelea kuenzi falsafa za mhasisi wa Taifa hili Mwl. J. K. Nyerere pamoja na Hayati Mzee Abeid Aman Karume ambao kwa kiasi kikubwa wamechangia katika suala zima la kudumisha umoja na msikamano wa Taifa.
“Kitendo hiki wanachofanya vijana kwa kupanda mlima Kilimanjaro ni jambo la kishujaa na uzalendo wa hali ya juu kwa Taifa ni matumaini yangu vijana wengi wataiga mfano huu mzuri,” alisema Mhagama
Alieleza kuwa, Baba wa Taifa Mwl. Julius K. Nyerere alifanya kazi kubwa ya kujenga misingi imara ya nchi kuwa na amani, umoja, mshikamano pamoja na misingi ya kuwa na uchumi wa kujitegemea.
“Vijana mnatakiwa kuendeleza na kuiga utendaji kazi wa Baba wa Taifa Mwl. Julius K. Nyerere alijitolea kwa mambo mengi ili kujenga Taifa, alikuwa mstari wa mbele katika kupambana na mambo mengi ikiwemo ujinga, maradhi na umaskini ili kila mtanzania awe na maisha bora. Hiyo ilikuwa ni ishara tosha kwa vijana kutambua namna Baba wa Taifa alivyolipigania nchi yetu,” alisema Mhagama
Aliongeza kuwa Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli pamoja na Dkt. Alli Mohammed Shein ni mfano tosha wa kuigwa na vijana, wanaonesha namna wanavyojitoa kwa ajili ya Taifa na kuhudumia wananchi pamoja na kukuza uchumi wa nchi.
Waziri Mhagama alifafanua kuwa, kuelekea kilele cha mbio za mwenge mwaka huu vijana hao waliopanda mlima Kilimanjaro watapata fursa ya kujumuika na vijana kutoka kwenye nchi jirani ikiwemo Angola, Zimbabwe, Msumbiji, Afrika Kusini, Uganda, Rwanda na Kenya katika kongamano la kujadili mchango wa Baba wa Taifa barani Afrika.
Aidha Waziri Mhagama alitoa wito kwa watanzania wote hususan vijana kuendelea kuenzi falsafa za waasisi wa taifa hili Baba wa Taifa, Mwl. Julius Kambarage Nyerere na Hayati Mzee Abeid Aman Karume kwa kutambua kuwa waasisi hao ni urithi tosha. Pia aliwasihii vijana kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuyaenzi yaliyofanywa na waasisi hao.
Sambamba na hayo alipongeza vijana ambao walijitolea kupanda mlima huo toka zoezi hilo lilipoanzishwa na Ofisi ya Waziri Mkuu ikiwa ni sehemu ya kuendelea kukumbuka falsafa za Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere. Pamoja na hayo alitoa shukrani kwa Wizara ya Maliasili na Utali, Uongozi wa Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA), Taasisi na Wadau kwa kushirikiana na Ofisi yake katika kufanikisha suala hilo muhimu kwa vijana.
Kwa Upande wake, Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii Mhe. Constantine Kanyasu alieleza kuwa suala la vijana hao kujitolea kupanda mlima Kilimanjaro ni kitendo cha kijasiri na kizalendo, itawajengea uwezo wa kuwa mabalozi wazuri wa vijana wenzao na pia wataweza kutangaza Mlima huo na vituo mbalimbali vya utalii vilivyopo nchini.
“Tumefanikiwa kuweka majina kwenye vituo 5 vilivyopo kwenye mlima huo ili kuwapa hamasa wanaopanda kutambua kuwa wanao uwezo wa kupanda hadi kileleni, kinachotakiwa ni kufuata ushauri utakao kuwa ukitolewa na waongozaji,” alisema Kanyasu
Naye Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mhe. Kippi Warioba aliwataka vijana kuendelea kutambua kuwa tunu za amani na umoja zilikuwa miongoni mwa falsafa kuu ya Mwalimu Nyerere ambapo matokeo yake ni umoja na mshikamano wa Taifa uliopo hadi sasa.
Pia Mkurugenzi wa Vijana katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bi. Mwanaidi Mohamed Ali alisema kuwa vijana wanapaswa kuendeleza yale yote yaliyofanywa na Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere pamoja na Hayati Mzee Abed Aman Karume ili waendelee kudumisha muungano.
Katika Mbio za Mwenge wa Uhuru Mwaka 2019, Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Idara ya Maendeleo ya Vijana inaratibu shughuli ya kupanda Mlima Kilimanjaro kwa Vijana. Jumla ya vijana 88 tayari wameshapanda mlima huo ikiwa ni kumbukizi ya miaka 20 ya kifo ca Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere.
Naibu Waziri wa Wizara ya Maliasili na Utalii Mhe. Constantine Kanyasu akieleza jambo wakati wa hafla hiyo ya kuwaanga vijana waliopanda Mlima Kilimanjaro kwa ajili ya kuadhimisha kumbukizi ya miaka 20 ya kifo cha Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere iliyofanyika Marangu, Mkoani Kilimanjaro. Kulia ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama, Mkuu wa Wilaya ya Moshi, Mhe. Kippi Warioba, Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Kilimanjaro Bw. Bwai Biseko na Kaimu Kamishna wa Hifadhi ya Mlima Kilimanjaro (KINAPA) Angela Nyaki.
|
Mkurugenzi wa Idara ya Maendeleo ya Vijana kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu Bw. James Kajugusi akifafanua jambo kuhusu ushiriki wa vijana hao kabla ya kuanza kupanda Mlima Kilimanjaro Oktoba 6, 2019 Mkoani Kilimanjaro. Kushoto ni Mkurugenzi wa Vijana katika Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bi. Mwanaidi Mohamed Ali.
|
Kiongozi wa Vijana waliopanda Mlima Kilimanjaro Dkt. Ally Matunzia akielezea jambo wakati Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista Mhagama alipowatembelea kwa lengo la kuwaaga kabla hawajapanda Mlima huo.
|
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akikabidhi Bendera ya Taifa kwa Kiongozi wa Vijana Dkt. Ally Matunzia kabla ya kuanza kupanda Mlima huo.
|
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Mhe. Jenista Mhagama akiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi mbalimbali na Vijana waliopanda Mlima Kilimanjaro ikiwa ni kuadhimisha Miaka 20 ya Kifo cha Baba wa Taifa Mwl. Julius Kambarage Nyerere.
|
EmoticonEmoticon
Note: Only a member of this blog may post a comment.