WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
Serikali imefanikiwa kukusanya mikopo iliyoiva yenye thamani ya
shilingi bilioni 183.3 sawa na asilimia 116.2 ya lengo la kukusanya
shilingi bilioni 157.7.
“Natambua
kwamba baadhi ya wahitimu wamepata mkopo kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu
ya Juu, hivyo natumia fursa hii kuwakumbusha wale wote mlionufaika na
mkopo wa Serikali katika kutimiza ndoto zenu za kupata elimu ya juu,
mkumbuke kurejesha mikopo,” amesema.
Ametoa
kauli hiyo leo mchana (Ijumaa, Novemba 29, 2019) wakati akizungumza
kwenye mahafali ya 45 ya Chuo cha Usimamizi wa Fedha yaliyofanyika
kwenye ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam.
Amesema
lengo la Serikali ni kuhakikisha kuwa kila anayenufaika na mkopo
asaidie wengine walio nyuma yake ili nao waweze kufaidika na utaratibu
huo wa kukopa na kulipa. Alisisitiza kwamba bila kufanya hivyo, ni
ukweli usiopingika kuwa Serikali itashindwa kuwajengea uwezo wananchi
wake wa kupata fursa zinazojitokeza za elimu katika ngazi mbalimbali.
“Ikumbukwe
kuwa, maendeleo ya Taifa lolote yanategemea uwekezaji katika rasilimali
watu. Hivyo nitoe rai kuwa wote mliokopeshwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu
ya Juu mfanye hima kulipa,” alisema Majaliwa
Katika hatua nyingine, Waziri
Mkuu Majaliwa amewataka wahadhiri na wanachuo wa vyuo vikuu na vyuo vya
elimu ya juu vilivyopo Dar es Salaam wachangamkie fursa ya kupata
nyumba na vyumba vya kupangisha katika miradi ya ujenzi wa nyumba ya
NSSF, NHC na Watumishi Housing zilizopo Kigamboni.
Amesema
amemuagiza Mkurugenzi Mkuu wa NSSF atenge maghorofa ambayo yatakaliwa
na wahadhiri na wanafuzi wa vyuo vya elimu ya juu na vyuo vikuu tena
waache kuwatoza bei kubwa na badala yake wapange bei mpya za kupangisha
ambazo wanachuo watazimudu.
Ili
kufanikisha utekelezaji wa jambo hilo, Waziri Mkuu amesema amewashauri
viongozi wa taasisi za elimu ya juu za mkoa wa Dar es Salaam wafanye
mawasiliano na Watendaji Wakuu wa NSSF, NHC na Watumishi Housing ili
wafikie makubaliano ya namna ya kupangisha au kununua nyumba hizo.
Akizungumzia
suala la kuboresha usafiri kwa wanafunzi na watu wakaoishi kwenye
nyumba hizo, Mheshimiwa Majaliwa amesema tayari amekwishatoa
maelekezo kwa viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam wakiwemo Wakuu wa
Wilaya za Kigamboni na Temeke wakutane na uongozi wa Mamlaka ya Usafiri
wa Nchi Kavu (LATRA) ili wapange safari za mabasi ya abiria kutoka
Tuangoma, Mtoni Kijichi hadi eneo la Ferry Kigamboni.
Mheshimiwa
Majaliwa amewasihi wahadhiri na wanachuo wachangamkie fursa hiyo ili
waweze kupata nyumba bora za kupanga au kununua ili kuepuka adha ambayo
imewakabili kwa muda mrefu ya kupanga au kuishi katika nyumba duni.
Akiwaasa
wahitimu wa Mahafali hayo, Mheshimiwa Majaliwa alisema: “Mnao wanao
wajibu mkubwa wa kuhakikisha kuwa mnatumia vizuri elimu
mliyoipata chuoni ili kuchochea maendeleo ya kweli ya nchi yetu. Hivyo
basi, huko mnakoenda iwe ni kwenye Halmashauri, Mikoa, Wizara, taasisi
za umma na hata sekta binafsi, mkawe chachu ya mafanikio.”
“Aidha,
mtakapokuwa huko kwenye maeneo mbalimbali ya kazi, hakikisheni
mnajitanabaisha kwa weledi na ufanisi wa hali ya juu. Tunawatarajia
muwe mfano kwa kuwa waadilifu, waaminifu na wachapa kazi,” alisema
Mheshimiwa Majaliwa.
Aliwasihi
wahitimu hao kuwa watakapoingia kwenye utumishi wa umma au kwingineko
wakazingatie maadili na kujiepusha na tabia ya kujitafutia utajiri wa
harakaharaka. “Kafanyeni Kazi kwa uzalendo wa hali ya juu,” aliongeza
Mheshimiwa Majaliwa.
Mapema, akimkaribisha
Waziri Mkuu kuzungumza katika mahafali hayo, Waziri wa Fedha na
Mipango, Dkt. Phillip Mpango alisema ili Chuo cha Usimamizi wa Fedha
(IFM) kiweze kuwa chachu ya mabadiliko makubwa ya kiuchumi yanayoongozwa
na Dkt. John Pombe Magufuli, ni lazima uongozi wa chuo hicho utekeleze
sera ya elimu kwa vitendo na kuwa wabunifu katika kupitia upya mitaala,
ufundishaji na kufanya tafiti.
Waziri
Mpango amelitaka Baraza la Uongozi wa Chuo cha IFM na wanataaluma
waendelee kuwa wabunifu zaidi ili kuhakikisha kwamba fani
zinazofundishwa Chuoni hapo zinaendana na wakati huku wakizingatia
mahitaji ya nchi na wananchi wake pamoja na mabadiliko ya haraka ya
kitekinolojia yanayoendelea ulimwenguni.
Jumla ya wahitimu 2,775 wametunukiwa tuzo mbalimbali na wanafunzi 20 wa Shahada ya Usimamizi wa Fedha wamepongezwa.
(mwisho)
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.