WAZIRI
MKUU Kassim Majaliwa amewataka Watanzania washirikiane katika kuulinda
na kuutetea Muungano wa Tanzania pamoja na Mapinduzi Matukufu ya
Zanzibar na kamwe wasiruhusu watu kuingiza sumu ya kutaka kuwagawa.
Ameyasema
hayo jana (Ijumaa, Januari 17, 2020) wakati akizungumza kwa nyakati
tofauti na wananchi katika mikutano iliyofanyika wilaya ya Kati na
wilaya ya Kusini alipokuwa katika ziara yake ya kikazi mkoa wa Kusini
Unguja.
“Watanzania
tusikubali mtu yeyote kutugawa kwa sababu sisi undugu wetu ni wa damu,
hivyo ni vema tukaendelea kuudumisha muungano wetu tusiruhusu watu
kuingiza sumu ya kutaka kutugawa kwani watu hao hawana tija.”
Waziri
Mkuu ambaye awali alikagua miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa maabara
ya sayansi katika shule ya sekondari ya Bwejuu, mradi wa kilimo cha
kisasa Jozani na kuzindua jengo la mama na mtoto Bambi. Amesema hayo
yote ni matunda ya muungano hivyo, hawana budi kuendelea kuudumisha.
Akikagua
maendeleo ya ujenzi wa maabara ya sayansi katika shule ya sekondari ya
Bwejuu, Waziri Mkuu ametoa muda wa miezi mitatu kwa mkandarasi
anayejenga maabara hiyo awe amekamilisha kazi hiyo.
Pia, Waziri Mkuu alimwagiza Mkuu
wa Mkoa wa Kusini Unguja, Bw. Ayoub Mohammed Mahmoud ahakikishe
watumishi wanatenga muda wa siku nne kwa wiki kwa ajili ya kwenda
kuwahudumia wananchi katika maeneo yao hususan ya vijiji.
Vilevile,
Waziri Mkuu aliagiza Maafisa kilimo wahamishiwe vijijini ili waweze
kuwasimamia vizuri wakulima ikiwa ni pamoja na kuwashauri namna bora ya
kulima kwa kufuata kanuni na matumizi mazuri ya pembejeo.
Kadhalika,
Waziri Mkuu alisisitiza umuhimu wa kutoa huduma kwa wananchi wote bila
ya kujali dini, kabila, rangi wala itikadi za chama kwa kuwa lengo la
Serikali ni kuhakikisha wananchi wote wananufaika na kuhudumiwa bila ya
kubaguliwa kwa namna yoyote.
Awali,
viongozi mbalimbali wa vyama vya upinzani wakiwemo wa vyama vya CUF,
NRA, UPDP, NSSR-MAGEUZI waliipongeza Serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa
Tanzania (SMT) pamoja na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kwa
kuimarisha huduma za kijamii.
Viongozi
hao walisema kuwa wapo tayari kushirikiana na Rais Dkt. John Pombe
Magufuli pamoja na Rais Dkt. Ali Mohammed Shein kwa sababu viongozi hao
wanafanya kazi kubwa na nzuri ya kuwahudumia wananchi.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.