NA.
MWANDISHI WETU
Waziri wa Nchi Ofisi ya
Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Uwekezaji nchini Mhe. Angellah Kairuki
amewahakikishia wafanyabiashara na Wawekezaji kuwa Serikali itaendelea
kuwawekea mazingira mazuri ya Uwekezaji nchini.
Pia, Amesema Serikali imejipanga
kuboresha mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na wawekezaji ili kuwavutia
wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kwa kuwekeza katika sekta mbalimbali zenye
tija katika kuliingizia pato taifa.
Ameyasema hayo hivi karibu alipokuwa
akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kuhitimisha ziara yake ya siku
6 katika Wilaya 6 za mkoa wa Pwani ikiwemo; Bagamoyo, Kibaha, Kisarawe,
Mkuranga, Mafia na Rufiji pamoja na Halmashauri ya Wilaya ya Chalinze.
Akieleza
lengo la ziara hiyo
Mhe.Kairuki amesema mkoa wa Pwani ni miongoni mwa mikoa yenye uwekezaji
mkubwa
katika sekta mbalimbali; Uvuvi, kilimo na ufugaji na amefanya ziara
hiyo ili kujionea mazingira pamoja na kusikiliza changamoto
zinazowakabili
Wawekezaji wa ndani na nje ya nchi.
Akitoa majumuisho ya ziara
hiyo Mhe. Kairuki amezitaja changamoto zilizojitokeza katika maeneo mengi
aliyotembelea kuwa ni ukosefu wa maji ya kutosha, ubovu wa barabara, ucheleweshwaji
wa vibali vya kazi, kukosa umeme wa uhakika na utitiri wa tozo.
Mbali ya changamoto hizo,
Mhe. Kairuki ametaja vikwazo vingine kuwa ni kutotengwa kwa maeneo ya
uwekezaji, Taasisi wezeshi kutokuwa karibu na wawekezaji, ukosefu wa mitaji ya
uhakika na utoaji wa adhabu zisizo za lazima.
Ameongeza kuwa uelewa mdogo
wa wawekezaji katika kujiunga na Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC) ni moja
ya changamoto na kuwataka wawekezaji kwa hiari yao waone umuhimu wa
kujiandikisha katika kituo hicho ili kutumia fursa zinazopatikana.
“Wawekezaji tunawakaribisha
TIC ili mjue fursa ziliopo nchini zaidi na kuona namna mnavyoweza kunufaika na
kituo hiki,”alisisitiza Waziri Kairuki.
Ameongoza kuwa, ipo haja ya
kila Halmashauri kuendelea kutenga maeneo ya uwekezaji ili kutoa fursa zaidi
kwa watu kuwekeza na kuhakikisha miundombinu muhimu inakuwepo.
“Natoa rai kwa kila
Halmashauri kuhakikisha kila kijiji kinatenga walau heka 20 za maeneo ya
uwekezaji na kuwasilisha taarifa zao TIC” alisema Waziri.
Aidha, Waziri Kairuki
amewataka wawekezaji kuzingatia sheria na taratibu za uwekezaji nchini ili
waweze kunufaika na mitaji yao waliyowekeza.
“Endeleeni kuwekeza pasipo
kuvunja sheria na kanuni zilizopo ikiwa ni kulipa kodi au kulipa vibali
mbalimbali mfanye hivyo tena kwa wakati ili isitokee mmewekeza kwa mitaji mikubwa
halafu ikawa kwa hasara,”alisisitiza Waziri Kairuki
Aliwahakikishia wawekezaji
kuwa, Serikali ya Awamu ya Tano, inatambua mchango wao na imedhamiria
kuhakikisha inaboresha miundombinu muhimu ikiwemo uwepo wa nishati ya umeme ya
uhakika, barabara bora, upatikanaji wa maji safi, kuboresha mifumo ya mawasilino
na upatikanaji wa huduma bora za mamlaka zinazosimamia masuala yanayohusu uwekezaji
nchini.
AWALI
Waziri Kairuki alifanya
ziara yake ya kikazi katika Mkoa wa Pwani kwa siku 6 na kuzitembelea Wilaya 6 ambapo jumla ya viwanda 22
alivifikia ikiwemo; Kiwanda cha KEDS, EUROPLASTIC, Samaki investment, KAMAL
LTD, Hiill Packaging Company, Tan Choice, Global Packaging Ltd, Hester
Bioscience Africa ltd, Chilambo Investment, Sabai Cash nut Processing, SHAFA
Investment, Everwell Cable, Ice Drop ltd, Lodhia Group ltd, Waja Mabati na Waja
General, Abajuko Enterprises, Tanpesca na kiwanda cha maziwa cha Mather
Dairies. Aidha alipata fursa ya kutembelea mashamba ya uwekezaji mbalimbali
pamoja na Shamba la Utunge, Sah janand, shamba la Utamaduni, Kigomani na shamba
la kuku la AKM.
Wawekezaji wa maeneo hayo
walipata fursa za kueleza changamoto wanazokabiliana nazo pamoja na mapendekezo
kwa Serikali ya namna bora ya kuendelea kuwa na ushirikiano ili kufikia dhamira
ya Serikali ya kuwa na Tanzania ya Viwanda.
|
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.