TAARIFA KWA VYOMBO
VYA HABARI
SERIKALI
YAZIFUNGA SHULE ZOTE KUANZIA LEO SABABU YA CORONA
SERIKALI imesema shule zote za awali, msingi na
sekondari zitafungwa kwa siku 30 kuanzia leo Machi 17, 2020.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri
Mkuu Kassim Majaliwa leo (Jumanne, Machi 17, 2020) wakati akizungumza na
waandishi wa habari ofisini kwake Magogoni, jijini Dar es Salam.
Amesema wanafuzi wa kidato
cha sita walipaswa kuanza mitihani Mei 4, 2020 lakini nao pia watapaswa kusibiri
Wizara ifanye utaratibu mwingine kulingana na matokeo ya hali ya maambukizi.
Amesema mikusanyiko yote mikubwa ya ndani na nje isiyo
ya lazima imesitishwa kuanzia sasa ikiwemo shughuli za michezo, matamasha ya
muziki, mikutano mbalimbali ikiwemo ya shughuli za kisiasa, mahafali na shughuli
nyingine za kijamii.
Amezitaka wizara na taasisi zizitishe semina,
warsha, makongamano na mikutano yote hapa nchini ambayo inahusisha washiriki
toka nchi zenye maambukizi makubwa. “Watanzania wenye safari zisizo za lazima
kwenye nchi zenye maambukizi makubwa, wanashauriwa wasitishe safari hizo,” amesisitiza.
Akielezea hatua nyingine zinazochukuliwa na Serikali
ili kudhibiti ugonjwa huo, Waziri Mkuu amesema: “Serikali imesitisha michezo
yote inayokusanya makundi ya watu ikiwemo Ligi Kuu ya Tanzania Bara (VPL), Ligi
Daraja la Kwanza (FDL), Ligi Daraja la Pili (SDL) na aina nyngine. Wizara ya
Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo iziandikie taasisi zake.”
Pia amewataka Wakuu wa Mikoa na Wilaya wahakikishe
maeneo yote yaliyobainishwa na kutengwa (vituo vya huduma na ufuatiliaji) kwa
ajili ya kuwahudumia wagonjwa endapo watajitokeza katika maeneo yao yanakuwa na
mahitaji yote muhimu na yanahudumiwa ipasavyo.
Katika
hatua nyingine, Waziri Mkuu amesema Serikali
tayari imetoa shilingi milioni 500 kati ya sh. bilioni moja zilizokuwa
zimetengwa kwa ajili ya Mbio za Mwenge wa Uhuru zilizokuwa zianze Aprili 2,
mwaka huu.
“Rais Dkt. John Pombe Magufuli ameahirisha Mbio za
Mwenge wa Uhuru zilizokuwa zianze Aprili 2, mwaka huu na kuagiza shilingi
bilioni moja zilizokuwa zimeandaliwa kwa ajili ya shughuli hiyo, zipelekwa
Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa ajili ya
maandalizi ya kujiweka tayari kudhubiti maambukizi ya CORONA. Serikali tayari
imetoa shilingi milioni 500.”
Akielezea hatua zilizochukuliwa baada ya mgonjwa wa
kwanza kubainika kuwepo nchini Tanzania, Waziri Mkuu amesema Serikali imechukua
hatua kwa kumchukua mgonjwa huyo na kumhifadhi kwenye eneo maalum kwa ajili ya
kumpatia huduma (isolation).
“Pia, Serikali imefanya ufuatiliaji wa watu
waliokutana na mgonjwa huyu tangu aingie nchini na kuwaweka kwenye karantini ya
siku 14, na pia kuchukua sampuli kwa lengo la kubaini kama wameambukizwa virusi
hivi,” amesema.
Ugonjwa huu umeingia nchini baada ya Mtanzania
mwenye miaka 46 aliyesafiri kwenda nchi za Ubeligiji, Sweden na Denmark hivi
karibuni, kupimwa na kuthibitika kuwa na virusi vya Corona (COVID-19).
Akielezea hatua zaidi zinazochukuliwa, Waziri Mkuu amesema
licha ya hatua ambazo zimechukuliwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, Serikali itaimarisha ukaguzi na ufuatiliaji wa wasafiri
wanaoingia nchini kupitia viwanja vya ndege, bandari na mipaka ya nchi kavu ili
kuwabaini wasafiri wenye dalili za ugonjwa na viashiria vyenye hatari.
“Tutaimarisha uwezo wa kupima sampuli kwa watu
wanaohisiwa kuwa na viashiria au dalili za ugonjwa huu ambapo maabara yetu ya
Taifa kwa sasa inao uwezo wa kutoa majibu kwa haraka.”
Amesema Serikali inaendelea kuwajengea uwezo
(mafunzo) watumishi wa sekta ya afya katika kukabiliana na magonjwa ya milipuko
ikiwemo jinsi ya kutoa tiba, kuchukua sampuli, uelimishaji na kuzingatia kanuni
za afya.
“Serikali imetenga hospitali maalum za Mloganzila
(DSM), Kituo cha Buswelu (Mwanza) na Hospitali ya Mawenzi (Kilimanjaro), Mnazi Mmoja
(Zanzibar) na ChakeChake (Pemba) kwa ajili ya kutoa huduma kwa waathirika.”
Ameiagiza Wizara ya Afya ihakikishe vifaa vya kinga
ikiwemo vimiminika vya kudhibiti maambukizi (hand sanitizer) vinapatikana
katika maduka yote husika na kwa bei ya kawaida na kuongeza kwamba Serikali
itachukua hatua kwa wafanyabiashara watakaobainika kufanya ulanguzi wa vifaa
hivyo.
Amewataka Watanzania wazingatie ushauri unaotolewa
na Serikali na kupuuza taarifa za uzushi zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
“Watanzania tuache mzaha wa kutumia mitandao ya kijamii kufanya upotoshaji wa
tahadhari katika jambo hili,” ameonya.
Amewaomba
viongozi wa dini waendelee kushirikiana na Serikali katika kuwaelimisha waumini
wao wote kuzingatia tahadhari za ugonjwa huu. Pia amevitaka vyombo vyote vya habari vishirikiane na Serikali
katika utoaji wa elimu kwa umma kuhusu kujikinga na Corona bila kufanya
upotoshaji wala kuipa jamii hofu.
Amewataka wananchi watoe taarifa kuhusu uwepo wa
mgonjwa au kupata ufafanuzi kuhusu ugonjwa huu kupitia namba za bure za 0800110124,
0800110125 na 0800110037.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
JUMANNE, MACHI 17, 2020.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.