WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema
hadi leo, hapa nchini kuna wagonjwa
24 waliothibitika kuwa na ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu (COVID-19) ambapo
watatu kati yao, wamepona na kuruhusiwa kutoka hospitali, mmoja amefariki dunia
na wagonjwa 20 wanaendelea vema na matibabu.
“Serikali
imeendelea kuwafuatilia watu 685 waliokutana na wagonjwa hao ambapo watu 289
wamemaliza siku 14 za kufuatiliwa na vipimo vyao vimethibitisha kuwa hawana
maambukizi ya virusi vya Corona. Watu wengine 396 waliobaki wanaendelea
kufuatiliwa ili kujiridhisha iwapo hawana maambukizi ya virusi hivyo.
Waziri
Mkuu ameyasema hayo leo (Jumatatu, Aprili 6, 2019) Bungeni jijini Dodoma kwenye
mkutano wa 19 wakati akihitimisha hoja ya bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi
zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka 2020/2021.
Amesema
hatua zinazochukuliwa katika kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona ni
pamoja na kufanya ukaguzi (screening) kwa wageni wote wanaoingia nchini kutoka nje
pamoja na kuwaweka katika uangalizi kwa siku 14.
“Ndege
zetu tumezuia kufanya safari za nje, tumezuia wafanyakazi kwenda nje ya nchi,
tumeimarisha mipaka sambamba na kuhakikisha wasafiri wote wanaoingia nchini
wanalazimika kuwekwa chini ya uangalizi wa lazima kwa siku 14 kwa lengo la kudhibiti
mienendo ya wasafiri chini ya ulinzi wa masaa 24,” amesema.
Waziri
Mkuu amesema kutokana na umuhimu wa kuwatenga watu wanaofuatiliwa,
Serikali imeagiza mikoa yote nchini itenge maeneo maalumu kwa ajili ya
uangalizi na kujiridhisha iwapo hawana maambukizi.
“Hatua
hii ni muhimu katika kudhibiti kuenea zaidi kwa maambukizi ya virusi vya Corona.
Kayi ya hao, wengi ni wale waliotoka nje ya nchi. Maeneo hayo yametengwa kwa nia
njema na yako kwa viwango tofauti kulingana na uwezo wa kifedha wa wahusika.
Yako mabweni, ziko nyumba, na vyote vimewekwa kwa kuzingatia gharama mtu anayoweza
kumudu,” amesisitiza.
“Tunafanya
hivi ili kuondoa manung’uniko yaliyokuwepo kwamba watu wanapelekewa katika
maeneo ambayo hawawezi kumudu. Na baada ya kuchukua hatua hizo, sasa hivi
malalamiko hayo yamepungua.”
Akielezea
hatua mbalimbali ambazo zinachukuliwa hivi sasa, Waziri Mkuu amesema Serikali
inaimarisha maabara mbalimbali nchini ili ziweze kutoa huduma za upimaji ikiwemo
maabara zilizopo kwenye mikoa ya Arusha, Dodoma Kigoma, Mbeya, Morogoro,
Mwanza, Pwani na Tanga.
“Hospitali
za Rufaa za Kanda na Mikoa nazo zinaratibiwa kutoa huduma ya upimaji sambamba
na maeneo ya mipakani. Shughuli hizo za upimaji zinafanyika kwa usimamizi wa
Maabara Kuu ya Taifa ya Afya ya Jamii kwa lengo la kuthibitisha ubora wa vipimo
hivyo na kuratibu utoaji wa matokeo.”
“Nilishasema
atakayetoa taarifa za ugonjwa ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia,
Wazee na Watoto, na kama itabidi nitatoa mimi mwenyewe na kama italazimika sana
atatoa Makamu wa Rais au Mheshimiwa Rais mwenyewe. Hii hali ya Wakuu wa mikoa
na Wilaya kutoa matamko kama alivyosema Mheshimiwa Mbunge hapa, haiku sawa.”
Waziri
Mkuu amesema Tanzania imeendelea kushirikiana kwa
karibu na Shirika la Afya Duniani (WHO), Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) na
Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) katika kuweka mikakati ya
pamoja ya kuimarisha mapambano dhidi ya Ugonjwa wa Homa Kali ya Mapafu
(COVID-19) na kwamba itaendelea kufanya tathmini kuhusu changamoto zinazoweza
kusababishwa na ugonjwa huo na namna ya kuzitatua.
Bunge
lilikubali kupitisha sh. 312,802,520,000 kwa ajili ya Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi
zilizo chini yake kwa mwaka 2020/2021. Kati ya fedha hizo, sh. 88,429,156,000
ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na sh. 224,373,364,000 ni kwa ajili ya matumizi
ya maendeleo.
Vilevile,
Bunge liliidhinisha sh. 121,786,257,000 kwa ajili ya Mfuko wa Bunge ambapo kati
ya hizo, sh. 113,567,647,000 ni za matumizi ya kawaida na sh. 8,218,610,000 ni
kwa ajili ya matumizi ya maendeleo.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.