WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu
(Sera, Uratibu, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu) Mhe. Jenista
Mhagama amepokea msaada wa hundi tatu zenye thamani ya sh. milioni 150
zilizotolewa na kampuni tatu zinazozalisha nguzo za umeme nchini kwa ajili ya
kusaidia mapambano dhidi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na virusi vya
Corona (COVID- 19).
Waziri amepokea michango hiyo kwa
niaba ya Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa leo tarehe 4 Mei, 2020 katika Ofisi
ya Waziri Mkuu Mlimwa, Jijini Dodoma. Michango hiyo imetolewa na kampuni Mufindi
Woodpoles Plant and Timber Ltd, Qwihaya General Enterprises Co Ltd na Poles (T)
Ltd ambapo kila kampuni imetoa sh. milioni 50.
Akizungumza wakati wa kupokea
michango hiyo Waziri Mhagama aliwapongeza viongozi wa kampuni hizo kwa kuunga
mkono jitihada za Serikali katika kuhakikisha inapambana na janga la ugonjwa wa
COVID-19.
“Nawashukuru sana kwa niaba ya
Serikali na hii inaonesha uzalendo, utayari na kuhakikisha kila Mtanzania
anakuwa ni sehemu ya mapambano hayo kwa vitendo,”alieleza Waziri Mhagama.
Pia, Waziri Mhagama alitumia fursa
hiyo kuwasihi wakandarasi wengine pamoja na Watanzania kuendelea kushirikiana
na Serikali kwa kujitolea kwa hali na mali ili kuwezesha katika kukabiliana na
janga hilo.
“Tunatoa wito kwa Watanzania wote
kuona umuhimu na kuguswa na janga hili kwa kuchangia kwa kadiri inavyofaa ili
kuendeleza uzalendo kwa hali ya kujali na kuonesha utayari ili kudumisha hali
ya utamaduni uliopo tangu awali wa umoja na mshikamano ,”alisema Waziri Mhagama.
Aliwahakikishia wadau hao kuwa,
michango hiyo itatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuwaeleza kuwa imefika
katika eneo salama.
Awali, Waziri wa Nishati Dkt. Medadi
Kalemani aliwapongeza viongozi wa kampuni hizo kwa michanga waliyoitoa kwa
Serikali ambayo inakwenda kuongeza nguvu katika kukabiliana na ugonjwa wa COVID-19.
“Niwapongeze wakandarasi hawa kwa
kuonesha nia ya kushiriki katika mapambano haya na wito wangu kila anayeguswa
na janga hili ni faraja kubwa mnayoitoa kwa Serikalini katika kuhudumia na
kusaidia katika kipindi hiki. Pia nawaomba wakandarasi wengine waige, ”alisema
Dkt. Kalemani.
No comments:
Post a Comment
Note: Only a member of this blog may post a comment.