Ofisi ya Waziri Mkuu imefanya mafunzo ya kujenga uwezo wa kutekeleza majukumu waliyokasimiwa kwa maafisa 36 kutoka idara na vitengo vya ofisi hiyo. Mafunzo hayo ya wiki moja yamefanyika kuanzia tarehe 24 hadi 28 Agosti 2020, Jijini Dodoma, ambapo Wakala wa Serikali ya Mafunzo kwa Njia ya Mtandao (TaGLA) waliendesha mafunzo hayo kwa ufadhili wa Shirika la Chakula Duniani.
Lengo la mafunzo hayo lilikuwa ni kujenga uwezo kwa maafisa wake katika maeneo ya Uchambuzi wa Sera, Ufuatiliaji na Tathmini ya Sera na Uandishi wa taarifa. Mafunzo hayo pia yamewezesha maafisa hao kuongeza umahiri wa utekelezaji majukumu waliyokasimiwa kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977, Ibara 52, ambapo jukumu la msingi la Ofisi hiyo ni kuratibu na kusimamia shughuli za Serikali katika sekta zote na Bungeni pamoja na majukumu mengine yaliyoainishwa kwenye Tangazo la Serikali Na. 144 Aprili 2016, lililofanyiwa mabadiliko tarehe 7 Oktoba 2017.
Akiongea wakati akifunga rasmi mafunzo hayo, leo tarehe 28 Agosti jijini Dodoma, Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Rais TAMISEMI anayeshughulikia elimu, Gerald Mweli hakusita kueleza furaha yake juu ya utaratibu wa Ofisi ya Waziri Mkuu kuendesha mafunzo kwa watumishi yanayolenga kujenga uwezo wa kutekeleza majukumu waliyokasimiwa.
“Nimevutiwa sana na mbinu zilizotumika katika ufundishaji wa mafunzo haya. Nimeambiwa katika kuhakikisha mnapata mbinu na umahiri kwenye Tathmini na Ufuatiliaji wa Sera, mmepitia Mpango Jumuishi wa Kitaifa wa masuala ya Lishe. Naelewa Ofisi ya Waziri Mkuu ndiyo mratibu wa mpango huu na sisi TAMISEMI tunatekeleza. Nakusudia na mimi Kufanya mafunzo kama haya kwa watumishi wa wizara yangu” amesisitiza Mweli.
Kwa
upande wake, Katibu
Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Uwekezaji), Dorothy Mwaluko
amelishukuru Shirika la Chakula Duniani
kwa ufadhili wa mafunzo hayo, ambapo matokeo ya mafunzo hayo ni Ofisi hiyo kuwa na mfumo bora wa uratibu wa
shughuli za serikali kutokana na mamlaka
iliyonayo kikatiba ya kuratibu shughuli zote za Serikali pamoja na masuala
mtambuka ikiwemo masuala ya lishe.
“Mafunzo haya yatakuwa ni mwendelezo kwa maafisa wote na menejimenti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, lengo ni kuongeza umahiri kwa uchambuzi bora wa sera, ufuatiliaji na tathmini ya sera pamoja na kuwa na mfumo bora wa mawasiliano ya utekelezaji wa majukumu kwa idara zote ndani ya Ofisi, pia na mfumo bora wa uratibu wa shughuli za serikali” amesisitiza Mwaluko.
Awali
akiongea kabla ya kufungwa kwa mafunzo hayo, Kaimu mkurugenzi mkuu wa Wakala ya Mafunzo kwa njia ya mtandao (TaGLA),
Dickson Mwanyika amefafanua kuwa mafunzo hayo yaliyoendeshwa kwa utaratibu wa
mijadala washiriki walipata fursa ya kufahamu mbinu za kimkakati za
uchambuzi wa Sera na kanuni za uratibu wa Sera, njia za kufanya ufutiliaji na
tathmini, vigezo vya kuzingatia katika kufanya tathmini na ufuatiliaji pamoja
na namna ya kuandika taarifa na muundo
wa taarifa.
Wakiongea kwa nyakati tofauti kwenye mafunzo hayo, baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo, Frank Mwega na Elilanga Kaaya wamebainisha kuwa mafunzo hayo yamekuwa msaada mkubwa kwa washiriki katika kuwajengea uwezo. Aidha, wameshauri uendelevu wa mafunzo ya namna hiyo yenye kuwajengea uwezo watumishi kwenye maeneo ya utendaji.
MWISHO.